Alice Lakwena (pia: Alice Auma; 1956 - 17 Januari 2007) alikuwa kiongozi wa kiroho kati ya Waacholi wa Uganda aliyeanzisha kundi la "Harakati ya Roho Mtakatifu" (Holy Spirit Movement) na kuendesha vita vya msituni dhidi ya serikali ya rais Yoweri Museveni kuanzia Agosti 1986 hadi Novemba 1987.

Alice Auma Lakwena katika kitabu juu yake.
Eneo la Acholi katika Uganda.

Maisha hariri

Alizaliwa kwa jina la Alice Auma. Baada ya ndoa mbili zilizotengwa alikuwa Mkatoliki. Tarehe 25 Mei 1985 alishikwa na mapepo akaonekana kama kichaa. Baada ya kupotea kwa siku 40 akarudi kama mganga wa kienyeji akiwa na kipaji cha kuwasiliana na mizimu kufuatana na utamaduni wa Kiacholi.

Pepo aliyesema mara nyingi kutoka mwake akajiita "Lakwena" na kutambulishwa kuwa roho ya afisa wa kijeshi wa Italia.

Wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe wa 1986 nchini Uganda Alice alitangaza kwamba aliambiwa na Lakwena kuanzisha Harakati ya Roho Mtakatifu na kuwaita Waacholi wachukue silaha kumaliza vita na umwagaji wa damu. Wamisionari katika eneo walipewa barua iliyosema:

"Mungu Bwana aliyemtuma Lakwena aliamua kubadilisha kazi yake kutoka mganga kuwa kiongozi wa kijeshi. Haina maana kumpona mtu leo akiuawa kesho. Hivyo Lakwena hana budi kumaliza umwagaji wa damu kabla ya kuendelea kama mganga."

Akapata wafuasi na kushambulia jeshi la serikali akashinda mara kadhaa na kuwaongoza wafuasi wake kuelekea Kampala. Akawaambia waumini kwamba risasi hazitawadhuru, zitageuka kuwa maji tu. Baada ya kushindwa, kabla ya kufikia mji mkuu, Lakwena akaondoka kutoka katika Alice. Alice akakimbilia Kenya akakaa katika kambi la wakimbizi la Daadab.

Mdogo wake Joseph Kony alikusanya baadaye mabaki ya kikosi chake na kuunda kundi jipya la "Lord's Resistance Army".

Alice alifariki huko Daadab tarehe 17 Januari]2007 kutokana na ugonjwa usioeleweka.