Diglosia (kutoka neno la Kiingereza lenye asili ya Kigiriki linalomaanisha "lugha mbili") ni hali inayotokea mahali ambapo kuna aina mbili za lugha moja, kila lahaja ikitumika kwa mahitaji maalumu.

Kwa mfano Kiarabu: kuna aina mbili za lugha hiyo moja:

  1. Lugha ya Juu inayoitwa Al-fasaha na
  2. Lugha ya Chini inayoitwa Al-Hamiya.

Hivyo ni matumizi ya lugha mbili katika jamii moja ambapo lugha moja huwa na hadhi ya juu na ile nyingine huwa na hadhi ya chini. Dhana hii inahusishwa na Charles Ferguson (1959).

Mathooko, P. (2007:60), akimrejelea Fasold, anasema kwamba ni hali ambapo lugha mbili tofauti katika jamii yenye lugha nyingi hupewa majukumu tofauti.

Kwa mujibu wa Iribe Mwangi na Mukhwana A. (2011:85), diglosia ni hali katika jamii ambapo lugha au lahaja mbili zilizo na mahusiano ya karibu zinapewa vibandiko vya kuu na sio kuu. Ili kuipa lugha kibandiko cha lugha kuu na sio kuu, muktadha wa matumizi ya lugha ni muhimu kwa sababu muktadha utaidhihirisha lugha kama ilivyo na hadhi au la. Yaani lugha itakayotumika pale inahitaji kuwa na urasmi (lugha hadhi ya juu); au inahitajika kuwa bila urasmi (lugha ya hadhi ya chini).

Lugha kuu na ile ambayo si kuu huweza kutofautiana kisarufi, kifonolojia na kimsamiati. Kwa kuwa lugha kuu imepewa hadhi ya juu hufunzwa shuleni ilhali lugha ambayo sio kuu mwanalugha hujifunza nyumbani kama lugha ya kwanza na huendelea kuitumia katika maisha [[]]yake katika shughuli za kawaida kama vile kununua bidhaa sokoni.

Lugha kuu hutumika katika mazingira rasmi kama vile bungeni, mahakamani, kutoa mihadhara vyuoni, utangazaji na uhariri wa magazeti.

Makala hii kuhusu mambo ya lugha bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Diglosia kama historia yake, uenezi au maendeleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.