Mzunguko

(Elekezwa kutoka Obiti)

Mzunguko ni njia mzingo inayotumiwa na gimba la angani linalozunguka gimba kubwa zaidi katika anga ya ulimwengu ambayo inashikwa na mvuto wa kani mvutano. Mfano wake ni mwendo wa sayari zinavyo zunguka Jua, au Mwezi unaovyo zunguka sayari yake ambayo ni Dunia, au satelaiti zinavyo zunguka Dunia.

Mzunguko wa gimba dogo (kama satelaiti) linalozunguka gimba kubwa (kama Dunia);
kani ya velositi "v" inataka kulipeleka mbele mbali na mahali pake; kani ya graviti "a" inalivuta kuelekea gimba kubwa; tokeo lake ni mzunguko.
Mfano wa "Mzinga wa Newton"

Uwiano wa kani katika mzunguko

Fizikia ya mzunguko inatazama kani au nguvu mbili.

  • Ya kwanza ni kasimwelekeo ya gimba dogo inayoelekea kwenda mbele mbali na mahali pake.
  • Ya pili ni uvutano unaovuta gimba dogo kuelekea gimba kubwa. Mzunguko upo pale ambako nguvu hizi mbili zinalingana. Kama kani ya velositi ikiwa kubwa zaidi gimba dogo lisingezunguka bali ingetoka. Kama kani ya graviti inakuwa kubwa zaidi gimba dogo litaanguka kwenye gimba kubwa.

Mfano wa "Mzinga wa Newton"

Mwanafizikia Isaac Newton aliwaza mfano unaoeleza vizuri kani zinazoathiri mzunguko. Aliwaza mfano wa (kanoni) uliowekwa juu ya mlima mrefu. Mzinga huu unaweza kurusha risasi kwa mwelekeo wa ulalo kwa kasi mbalimbali. Athari ya msuguano wa hewa kupunguza kasi dhidi ya risasi aliacha kando au kuwaza mlima mrefu kiasi cha kupenya juu ya angahewa ya dunia.

  • Kama mzinga unarusha risasi yake kwa velositi ndogo itaenda mbele kiasi halafu kuanguka chini (A).
  • Kama kasi au velositi inaongezwa itaanguka mbali zaidi(B).
  • Kasi ya risasi ikiongezeka zaidi kuna hali ambapo risasi haianguki tena inazunguka dunia na kumailisha mzunguko wa duara (C).
  • Kama kasi inaongezeka tena mzunguko unachukua umbo la duaradufu. Mahali pa periheli ambapo mzunguko upo jirani zaidi na dunia ni mahali pa kufyatuliwa na 180° kinyume chake upande wa pili ni afeli ambapo mzunguko uko mbali na Dunia. (D)
  • Kasi ya risasi ikiongezwa zaidi inafikia velositi ya kuweza kutoka katika graviti ya Dunia. (E).

Kwa hali halisi makadirio ya makombora ya kurusha satelaiti na vyombo vya angani vinafuata maelezo hapo juu. Kama kombora linatakiwa kubeba satelaiti kama vile satelaiti ya televisheni au ya mawasiliano ni lazima kukadiria velositi ya kombora kulingana na uzito wake na mahali panapotakiwa kufikia angani ili kuweza kupeleka satelaiti katika mzunguko aina ya (C) au (D).

Chombo cha angani kinapotakiwa kupelekwa safari ya kwenda mwezi au sayari nyingine sharti kufikia "velositi ya kutoka" katika graviti ya Dunia.

Historia ya utafiti wa mzunguko

Zamani watu walifikiri ya kwamba Jua linaizunguka Dunia kila siku jinsi inavyoonekana kwa macho: Jua linachomoza upande mmoja wa upeo wa anga wakati wa asubuhi na kuzama chini upande wa pili wakati wa jioni.

Kwa hiyo wataalamu Wagiriki wa Kale kama Klaudio Ptolemaio waliwaza jua na sayari kuzunguka dunia na mizunguko hii ilikuwa na umbo la duara kamili.

Kuanzia utafiti wa akina Koperniko na Galilei ilitambuliwa ya kwamba dunia ndiyo inayozunguka Jua pamoja na sayari nyingine, kila moja kwenye mzunguko wake. Ilionekana pia ya kwamba mizunguko hiyo si duara kamili lakini inalingana zaidi na duaradufu.

Kipindi cha mzunguko

Kipindi cha mzunguko ni muda unaotumiwa na gimba kama satelaiti, mwezi au sayari kuzunguka gimba mama.

Kwa mfano kipindi cha Dunia yetu kuzunguka Jua ni siku 365.25 na kipindi hiki tunaita "mwaka".

Kipindi cha mzunguko wa Mwezi ni siku 27; wakati huohuo unajizunguka mara moja kwenye mhimili wake na hii ndiyo sababu sisi tunaona upande uleule wa Mwezi muda wote.

  Makala hii kuhusu mambo ya fizikia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mzunguko kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.