Panonia (kwa Kilatini Pannonia) ilikuwa jimbo la Dola la Roma kuanzia mwaka 9 KK hadi 433. Eneo lake lilipakana na milima ya Alpi upande wa magharibi na mto Danubi upande wa kaskazini na mashariki. Leo hii eneo lake lakaliwa na Hungaria ya magharibi, Burgenland ya Austria na sehemu za Kroatia, Serbia na Slovenia. Wakati wa Roma ya kale jimbo liligawiwa mara mbili na mwaka 433 lilikabidhiwa kwa mfalme Attila wa Wahunni.

Ulaya ya Mashariki-Kusini wakati wa Roma ya Kale - Panonia iko upande wa kushoto juu yenye mipaka ya rangi ya kijani.

Wakazi hariri

Leo hii sehemu kubwa hukaliwa na Wahungaria lakini mababu zao waliingia huku karne nyingi baada ya Attila. Wakati wa Waroma wakazi wengi walikuwa Wapanoni waliokuwa kabila lenye asili kati ya Wakelti. Baadaye viliingia vikundi vingi, hasa wakati wa uhamisho wa mataifa katika Ulaya katika karne ya 3 hadi ya 10.

Historia hariri

Waroma wa Kale walieneza milki yao huku chini ya kaisari Augusto aliyesukuma mpaka wa Dola la Roma hadi mto Danubi. Mwaka 6 BK wazalendo walijaribu kuwafukuza Waroma lakini walishindwa na mwaka 9 jimbo la Panonia liliundwa. Waroma walijenga maboma mengi kando ya mto Danubi kama vituo vya ulinzi dhidi ya makabila makatili yaliyokalia upande mwingine wa mto.

Katika karne ya 5 uwezo na nguvu ya Dola la Roma ilififia mbele ya mashambulio ya makabila mengi kutoka mashariki na kaskazini. Mfululizo wa vita mbalimbali uliharibu nchi na wakazi wengi Waroma waliondoka wakahamia sehemu zenye usalama zaidi. Hivyo Kaisari Thedosio II aliondoa legioni zake kutoka Panonia akakabidhi nchi yote kwa Wahunni chini ya mfalme Attila.

Baada ya kifo cha Attila utawala wa Wahunni ukaporomoka na makabila ya Kigermanik yalitawala yakifuatwa na Waslavi mbalimbali.

Tangu mwaka 900 Wahungaria walifika wakaanza kutawala nchi na wakazi wengi polepole wakapokea lugha yao.

Baadaye watawala wa Habsburg kutoka Austria na Waislamu wa Milki ya Osmani walishindania utawala wa eneo lililokuwa sehemu ya Milki ya Austria-Hungaria hadi 1918. Mwaka ule eneo likagawiwa kwa Austria, Hungaria na Ufalme wa Yugoslavia.