Pentekoste ni sikukuu ya dini za Uyahudi na Ukristo ambayo huadhimishwa wiki 7 za siku 7 baada ya Pasaka, hivyo siku ya 50 baada yake.

Pentekoste ya Mitume ilivyochorwa mnamo mwaka 586 katika Biblia ya Rabbula nchini Iraki.
Mwaka wa Kanisa kadiri ya kalenda ya liturujia ya Roma kama kielelezo cha kawaida kwa Ukristo wa magharibi.
Mwaka wa liturujia
Magharibi
Mashariki

Jina hariri

Jina hili lilianza kutumika kwa sababu kwa lugha ya Kigiriki lina maana ya namba 50. Hivyo "πεντηκοστή [ἡμέρα]" (pentekostē [hēmera]) ni "(siku ya) hamsini".

Shavuot ya Kiyahudi hariri

Sikukuu ya Kiyahudi ya Pentekoste inaadhimishwa siku ya hamsini baada ya Pasaka ya Kiyahudi. Sikukuu hii husherehekewa na Wayahudi pia kwa jina asili la Kiebrania חג השבועות, Hag ha Shavuot, yaani Sikukuu ya Majuma, kwa kifupi "shavuot" ("majuma") jinsi ilivyoamriwa katika kitabu cha Mambo ya Walawi 23:16.

Ilikuwa sikukuu ya mavuno kama vile Pasaka ilivyohusiana na malimbuko.

Pentekoste ya Kikristo hariri

Kwa wafuasi wa Yesu Kristo ni ukumbusho wa umwagaji wa Roho Mtakatifu juu ya mitume na wanafunzi wengine wa Yesu na kuanzishwa kwa Kanisa siku ya 50 baada ya Pasaka ya Kikristo au ufufuko wa Yesu.

Inawezekana kusema ya kuwa baada ya kifo na ufufuko wa Yesu wanafunzi wake - ambao walikuwa wote Wayahudi - walikutana kwenye sikukuu ya Kiyahudi ya Shavuot wakati ambapo Wayahudi kutoka nchi mbalimbali walipotembelea Yerusalemu kwa hija kwenye nafasi ya sikukuu ile.

Tangu kuachana kwa kalenda ya Kikristo na kalenda ya Kiyahudi sikukuu zake kwa kawaida haziangukii siku ileile tena.

Pentekoste ya Mitume hariri

Maelezo juu ya Pentekoste ya kwanza ya Kanisa hupatikana katika sura ya pili ya kitabu cha Matendo ya Mitume cha Agano Jipya katika Biblia ya Kikristo.

Humo Mwinjili Luka anasimulia jinsi wanafunzi wa Yesu walivyokutana katika mji wa Yerusalemu siku ile ya "Pentekoste" na kupokea paji la Roho Mtakatifu. Baadaye walitoka nje ya nyumba ya ghorofa walimokaa, wakianza mara kuhubiri juu ya Yesu Kristo mbele ya watu wengi, wakiwa wakazi wa mji huo pamoja na wageni kutoka nchi nyingi.

Kufuatana na taarifa yake siku hiyo watu takriban 3,000 walibatizwa kwa jina la Yesu na kuongezeka katika kile kikundi. Ndiyo maana Pentekoste inahesabiwa kuwa kuzaliwa kwa Kanisa.

Tarehe ya Pentekoste hariri

Husherehekewa jumapili ya 7 baada ya Pasaka.

Katika madhehebu ya Ukristo yanayofuata kalenda ya Gregori Pentekoste itasherehekewa kwenye tarehe zifuatazo:

  • 2015: 24 Mei
  • 2016: 15 Mei
  • 2017: 4 Juni
  • 2018: 20 Mei
  • 2019: 9 Juni
  • 2020: 31 Mei

Makanisa ya Kiorthodoksi yanayofuata kalenda ya Juliasi huwa na tarehe tofauti.

Madhehebu ya Kipentekoste hariri

Kuanzia mwaka 1907, katika Ukristo limejitokeza tapo la kiroho linalosisitiza umuhimu wa karama kama zilivyojitokeza siku ya Pentekoste na mwanzoni mwa Kanisa. Ndiyo sababu waumini wake wanaitwa Wapentekoste.

  Makala hii kuhusu mambo ya Biblia bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Pentekoste kama historia yake au athari wake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.