Presbyterorum Ordinis

Hati hiyo ilitolewa na Mtaguso wa pili wa Vatikano tarehe 7-12-1965, siku ya mwisho kabla ya kufunga, kwa kura 2390 dhidi ya 4 tu.

Jina lake kwa Kilatini ni "Presbyterorum Ordinis", maana yake "Daraja ya Mapadri".

Lengo lake ni kufafanua tena mambo kadhaa yaliyokwishaelezwa katika hati nyingine kuhusu viongozi wa daraja ya pili wa Kanisa Katoliki.

Sura ya kwanza hariri

Sura ya kwanza inahusu upadri katika utume wa Kanisa, jinsi unavyounganisha mapadri na maaskofu kwa ajili ya taifa la Mungu.

Sura ya pili hariri

Sura ya pili inaeleza kwanza zile kazi tatu za mapadri, yaani kufundisha, kutakasa na kuongoza.

Halafu inasisitiza uhusiano wao na askofu, kati yao, tena na walei.

Mwishowe inafikiria la kufanya ili kuwe na mapadri wa kutosha: hiyo haitegemei tu bidii kwa ajili ya miito, bali pia ugawaji mzuri wa watenda kazi katika shamba la Bwana.

Sura ya tatu hariri

Sura ya tatu inaingia zaidi katika maisha yao ikisisitiza wanavyopaswa kwa namna ya pekee kulenga utakatifu, na kuutafuta hasa kwa kutekeleza vema huduma zao na kuziunganisha katika kutimiza matakwa ya Baba kama Yesu alivyofanya.

Kati ya maadili wanayoyahitaji, hati inaeleza hasa mashauri ya Kiinjili ya utiifu, useja na ufukara ambayo kwao yanalenga ubora wa huduma za kipadri (tofauti na watawa wanaoyashika kwanza ili kujipatia utakatifu).

Kwa sababu hiyo, la kwanza kwa mapadri ni utiifu, kumbe useja si wa lazima (tunavyoona katika Kanisa la mwanzoni na katika Makanisa ya Mashariki mpaka leo).

Baada ya hapo hati inakabili suala la kuwasaidia kwa namna mbalimbali: kwanza katika maisha ya Kiroho, halafu kuhusu elimu hasa ya kidini, lakini pia kuhusu malipo ya haki na bima wasije wakahangaika.

Mwishoni mapadri wanatiwa moyo katika magumu yanayowakabili siku hizi, kwa kukumbusha kinachojulikana kwa imani tu, kwamba Mungu na Kanisa wapo pamoja nao.

Viungo vya nje hariri