Puto ni chombo cha usafiri angani inatumia nguvu elezi ya gesi nyepesi kwa kubeba abiria na mizigo juu hewani. Inatembea kwa kusukumwa na upepo na njia ya pekee ya kuiongoza ni kuipandisha au kushusha. Ni tofauti na ndegeputo (purutangi) yenye injini inayoweza kulengwa na rubani yake.

Puto ya hewa joto inapashwa moto kwa kusudi la kujaza fuko yake kwa hewa A hot air balloon is prepared for flight by inflation of the envelope with propane burners.
Puto ya hewa joto inaelea
Puto nyingi wakati wa mashindano

Muundo wa puto hariri

Kimsingi puto ni fuko kubwa lenye ganda la kitambaa au plastiki lisilopenya gesi. Hujazwa ama gesi nyepesi kama heli au hidrojeni au hewa joto iliyo nyepesi kuliko hewa ya kawaida na kuelea juu.

Puto huelea kama uzito wake yaani jumla ya fuko, mzigo na gesi ndani ya fuko ni nyepesi kuliko jumla ya hewa inayosukumwa kando naye.

Historia ya puto hariri

Kuna taarifa ya kwamba Wachina walirusha puto kama alama za kijeshi tayari wakati wa karne ya 3 BK.

Mtu wa kwanza anayejulikana kupaa kwa msaada wa puto alikuwa padre Mreno Bartolomeu de Gusmão mnamo mwaka 1709 mjini Lisbon. Baada ya majaribio ya kurusha puto bila mzigo alifaulu kujipeleka kwa takriban kilomita moja lakini akaanguka chini baadaye.

Kaka wawili Montgolfier walifaulu kutengeneza fuko kubwa za hewa joto mnamo 1783 huko Ufaransa. Tar. 21 Novemba 1783 puto yao ilibeba rubani wawili kwa dakika 25 wakavuka umbali wa kilomita nane.

Siku chache baadaye profesa Jacques Charles alipaa kwa puto ya kwanza ya gesi iliyotumia hidrojeni. Alipaa hadi kimo cha mita 600 akavuka umbali wa 43 km katika muda wa masaa mawili.

Tar. 7 Januari 1785 Mfaransa Jean-Pierre Blanchard na Mwamerika John Jeffries walifaulu kuvuka mfereji wa Uingereza.

Ufaransa ilikuwa pia nchi ya kwanza iliyojaribu kutumia puto kijeshi kwa kusudi la kuangalia maadui kutoka juu na kuongoza mashambulio. Matumizi haya yaliendelea hadi vita kuu ya kwanza ya dunia wakati ambako puto zilishambuliwa kwa ndege za kijeshi.

Matumizi leo hariri

Kimichezo na kitalii hariri

Leo hii matumizi ya puto ni mara nyingi ya kimichezo na kitalii. Kwa mfano puto zabeba watalii kwenye mibuga ya wanyama Afrika na penginepo kwa sababu hazina makelele zinakaribia wanyama bila kuwashtusha.

Kisayansi hariri

Puto zina umuhimu kwa sayansi zikibebea vyombo vya upimaji juu kwenye angahewa vinapopima mnururisho, halijoto au shindikizo. Mwaka 1972 puto ya Marekani ilifikia kimo cha 51.8 km.