Somalia ya Kiitalia

Somalia ya Kiitalia ilikuwa koloni la Italia kwenye eneo la Somalia tangu miaka ya 1880 hadi 1960, mwaka wa uhuru.

Somalia ya Kiitalia ndani ya Somalia ya leo.

Kuanzia mwaka 1888 Italia ilijipatia mikataba ya ulinzi na masultani mbalimbali waliotawala maeneo madogo kwenye Pembe ya Afrika. Walitangulia 1889 na sultani ya bandari ya Hobyo na mtawala wa usultani wa Majerteen.

Mwaka 1892 Usultani wa Zanzibar ulikodisha bandari ya Banadir kati ya Mogadishu hadi Brava kwa Italia. Mwaka 1905 Italia ilinunua eneo hili kutoka Zanzibar na kulitangaza kuwa koloni na Mogadishu kuwa mji mkuu.

Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia Waitalia walikabidhiwa na Uingereza eneo la Kismayu. Walilitawala kwa jina la "Oltre Giuba" (ng'ambo ya mto Juba) na kuliunganisha na Somalia ya Kiitalia tarehe 30 Juni 1926.

Wakati uleule waliamua kumaliza hali ya sultani za Majarteen na Hobyo kuwa nchi lindwa na kuzifanya sehemu kamili za koloni. Mipango hiyo ilisababisha vita kali ya miaka miwili kwa sababu masultani waliona mikataba yao ya ulinzi ilivunjwa wakapinga jeshi la Italia.

Mwaka 1936 Somalia ikaunganishwa na Ethiopia kuwa sehemu ya Afrika ya Mashariki ya Kiitalia.

Wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia makoloni ya Italia yalivamiwa na Uingereza uliotawala Somalia tangu 1941.

Mwaka 1949 Somalia ilirudishwa mikononi mwa Italia ilisimamie kwa niaba ya Umoja wa Mataifa.

Mwaka 1960 utawala wa kikoloni ulikwisha na Somalia ikapata uhuru wake.