Uvuvio (kutoka kitenzi kuvuvia; kwa Kiingereza: inspiration) ni tukio la Kimungu linaloaminiwa na Wakristo kuhusu uandishi wa Biblia. Yaani ni hali ya Kimungu ambayo iliwatokea watu kadhaa wa zamani ili kutunga, kuboresha na kukamilisha maandiko matakatifu kwa uwezo wa Roho Mtakatifu.

Ni kwamba kadiri ya imani hiyo Mungu aliwavuvia Roho Mtakatifu baadhi ya watu ili kuwaongoza katika kuchangia kwa namna yoyote uandishi huo ili hatimaye maandishi yaliyokusanywa na Kanisa katika Biblia ya Kikristo yastahili kuitwa Neno la Mungu, si la binadamu tu.

Hata hivyo madhehebu ya Kikristo yanatofautiana kuhusu namna ya kuelewa uvuvio, tena katika historia ya Kanisa yamejitokeza mabadiliko ya mitazamo kadiri ya maendeleo ya utaalamu n.k.

Imani ya namna hiyo inafanana na ile ya Wayahudi kuhusu Biblia ya Kiebrania, ingawa katika lugha asili za Biblia hiyo hakukuwa na msamiati maalumu.

Kumbe katika Agano Jipya neno uvuvio linapatikana katika 2Tim 3:14-16 ilipoandikwa kuwa Andiko lote (la Biblia) limevuviwa na Mungu (θεόπνευστος theopneustòs).

Halafu 2Pet 1:20-21 inaeleza kuwa waandishi (wa Biblia) kwa kusukumwa na Roho Mtakatifu walisema kwa niaba ya Mungu.

Kwa kuwa Agano Jipya linaonyesha kuwa Biblia iliandikwa na watu lakini chini ya uongozi wa pekee ya Mungu, imani kwake inadai kila mtu asadiki ukweli wa yote yaliyomo, ingawa madhehebu yanatofautiana tena kuhusu jambo hilo. Kwa mfano, Kanisa Katoliki linadai waamini wakubali ukweli wa yale yote yaliyoandikwa kuhusu wokovu, si kuhusu fani mbalimbali za elimu ya kidunia, kama vile sayansi, jiografia n.k. Hii ni kwa kuzingatia upande mmoja lengo la Mungu katika kujifunua, upande mwingine hali ya ujuzi wa binadamu aliyechangia uandishi karne nyingi zilizopita, elimu ilipokuwa mdogo sana kulingana na ile ya leo na ya kesho.

Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Uvuvio kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.