Vulgata (kwa Kilatini ya umati yaani tafsiri ya kawaida) ni tafsiri maarufu zaidi ya Biblia ya Kikristo katika lugha ya Kilatini.

Ilitolewa kuanzia mwaka 382 hadi 405 na Hieronimo kwa agizo la Papa Damaso I ili ichukue nafasi ya tafsiri mbalimbali zilizotangulia ambazo hazikuridhisha.

Kuanzia karne ya 8 hadi 9 ilikuwa Biblia ya kawaida katika maeneo yaliyokuwa chini ya Kanisa Katoliki ikitazamwa kuwa toleo pekee lililostahili kutumiwa.

Matengenezo ya Kiprotestanti yalichukua jukumu la kusambaza Biblia katika lugha yoyote yakitegemea makala za zamani katika lugha asili, yaani Kiebrania, Kiaramu na Kigiriki.

Lakini makala zilizojulikana hazikuwa za zamani kuliko zile alizozitumia Hieronimo kutengenezea Vulgata; hivyo zilikuwa na makosa mengi ambayo yakaja kurekebishwa hasa katika karne ya 20 kutokana na maendeleo ya utaalamu.

Upande wa Kanisa Katoliki Mtaguso wa Trento ulitangaza Vulgata kuwa tafsiri rasmi ya Biblia na kuwa haina makosa upande wa imani na maadili. Tamko hilo halikuwa na maana ya kuwa tafsiri hiyo haiwezi kuboreshwa.

Kwa kuwa mtaguso huo ulisisitiza kuwa "toleo la kale la Vulgata, lililokubaliwa na Kanisa lenyewe kwa kulitumia tangu karne nyingi, linatakiwa kutazamwa toleo rasmi kwa usomaji wa hadhara, mabishano, mahubiri na ufafanuzi" ikawa desturi kwa Wakatoliki kutoa tafsiri rasmi katika lugha mbalimbali kutokana na Vulgata badala ya kutumia lugha asili.

Hivyo Wakatoliki walijikuta wanatumia tafsiri zinazolingana na makala ya kale zaidi kuliko tafsiri za Waprotestanti, ingawa hawa wa pili walikuwa na utaalamu mkubwa zaidi.

Mwaka 1943 Papa Pius XII alihimiza Wakatoliki kutoa tafsiri mpya kutoka lugha hizo, kama zile zilizofanywa na Wakristo wengine tangu zamani.

Mtaguso wa Pili wa Vatikani uliamua tafsiri hiyo iangaliwe upya na tangu 1979 "Nova Vulgata (yaani Vulgata Mpya) imetolewa.

Viungo vya Nje hariri