Yohane Krisostomo, kwa Kigiriki χρυσόστομος, khrysóstomos, yaani «Mdomo wa dhahabu» alivyoitwa kutokana na ubora wa mahubiri yake, (Antiokia wa Siria, leo Antakya,nchini Uturuki, 347 hivi - Comana Pontica, Uturuki, 14 Septemba 407) alikuwa Patriarki wa Konstantinopoli.

Yohane Krisostomo (karne XI.
Yohane Krisostomo na Gregori wa Nazianzo katika picha ya Kirusi ya karne XVIII.

Ari yake ilisababisha apendwe na vilevile achukiwe sana. Hatimaye alifukuzwa na Kaisari na kufa uhamishoni.

Tangu zamani anaheshimiwa kama mtakatifu na babu wa Kanisa.

Mwaka 1568 Papa Pius V alimuongezea sifa ya mwalimu wa Kanisa.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 13 Septemba[1].

Maisha hariri

Asili na ujana hariri

Yohane alizaliwa Antiokia wa Siria katika familia tajiri ya Kikristo mwaka 347 hivi. Wakati huo mji huo ulikuwa unamfuata Konstantinopoli na Aleksandria tu kwa umuhimu upande wa mashariki wa Dola la Roma.

Katika karne IV huko zilitokea vurugu nyingi kwa msingi wa dini. Mjini kulikuwa na maaskofu wawili walioshindana: Melesyo na Paulino. Yohane aliishi ujana wake katika mazingira hayo, akikosa utulivu, akipenda vyakula na maigizo.

Baba yake, Sekundo, aliyekuwa askari kiongozi, alifariki mapema na kumuacha mtoto mdogo pamoja na dada yake kwa mama yao, Anthusa, mwenye umri wa miaka 22 tu ambaye alimlea vizuri sana upande wa utu na wa imani vilevile.

Baada ya masomo yote, alifundishwa tena na Libanio, mhubiri maarufu kuliko wote wa wakati ule ingawa Mpagani, ambaye alisema juu yake, «Angekuwa kati ya wanafunzi wangu bora, kama Kanisa lisingeniibia». Kumbe Yohane akaja kumzidi, ila upande wa kuhubiri Neno la Mungu.

Alipofikia miaka 18 anni alikutana na askofu Melesyo akamuomba ubatizo (alioupata mwaka 368) akaanza kufuata kozi za Diodoro wa Tarso, maarufu kwa ufafanuzi wa maneno yenyewe ya Biblia usiofuata sana maana ya kiroho.

Kupewa daraja hariri

Alipomaliza masomo hayo (367-372) na kupewa daraja ndogo akajifungia upwekeni miaka minne akasoma teolojia, hasa Injili na Nyaraka za Mtume Paulo. Katika pango alimoishi miaka miwili tena, afya yake ikawa mbovu ikamrudisha Antiokia kwenye wito wake halisi: uchungaji. Uzoefu wa kutafakari Neno la Mungu upwekeni ulikuwa umestawisha ndani yake msukumo mkubwa wa kushirikisha wengine kwa kuhubiri Injili.

Alitunga kitabu juu ya upadri kilichoathiriwa sana na Gregori wa Nazianzo. Humo alieleza kuwa umonaki si njia pekee ya kulenga ukamilifu; bali kutoa huduma za kipadri kwa faida ya waamini kati ya vishawishi vingi vya ulimwengu ndiyo njia bora ya kumtumikia Mungu. Aliandika kwamba angetakiwa kuchagua kati ya matatizo ya kuongoza Kanisa na utulivu wa maisha ya kimonaki angechagua mara elfu huduma ya kichungaji.

Miezi ya baridi kati ya miaka 380381 alipewa na Melesyo daraja ya ushemasi mwaka 386 na miaka michache baadaye akawa kasisi na msaidizi mkuu wa askofu Flaviano, akihubiri katika kanisa muhimu zaidi la Antiokia.

Wakati huo alisema, “Anatosha mtu mmoja mwenye ari kwa kubadilisha mwenendo wa umati”. Maneno hayo yakawa kaulimbiu yake kama mchungaji na kiongozi wa kiroho wa watu wake akiwatia moyo kufuata maadili.

Sifa yake kama mhubiri iliongezeka, hasa Antiokia ilipokabili ghadhabu ya Kaisari kwa uasi wa mwaka 387, hata wasikilizaji wakaanza kujiandikia kumbukumbu za maneno yake.

Pamoja na hayo mwenyewe aliendelea kutunga vitabu mbalimbali.

Mwaka 397 Patriarki Nektario alipofariki, kulikuwa na ushindani mkubwa kwa kushika nafasi yake, mpaka Kaisari Arcadio, kinyume cha matarajio ya wote, alipomchagua Yohane, ambaye hakuwa na hamu hiyo.

Alihamia huko kwa kutumiwa tu nguvu na udanganyifu, bila kujua namna ya kuhusiana na vigogo.

Askofu hariri

Huko Konstantinopoli aliongoza Kanisa kwa bidii nyingi ili kulirekebisha, akishambulia ufisadi na anasa ya viongozi, akijipatia hivyo maadui wengi kwenye ikulu. Hivyo maisha yake hayakuwa na amani, tofauti na hamu ya moyo wake mpole.

Mwenyewe aliishi kwa usahili, unyenyekevu na uchangamfu kama kielelezo kwa wote, akitumikia watu na kutumia mali zake kwa ajili ya mafukara na wagonjwa.

Aliendelea kushika maisha magumu na kudai wasaidizi wake pia wafanye vilevile. Kwa usimamizi wake mzuri alianzisha na kuendesha miundo mbalimbali ya misaada, hata akaitwa “Mtoasadaka”.

Isitoshe, katika mahubiri yake alipendekeza Kanisa la Konstantinopoli lifuate kielelezo cha lile la kwanza la Yerusalemu na hivyo lichangie ujenzi wa jamii mpya ambapo wote waishi kama ndugu: hakuna wa kuachwa nyuma, kwa kuwa kila mmoja ni muhimu, si jamii tu. Hivyo alichangia sana mafundisho ya Kanisa kuhusu masuala ya jamii.

Kama mchungaji halisi, aliwatendea wote kwa wema, akiheshimu wanawake kwa namna ya pekee na kuwajibika kwa ustawi wa ndoa na familia.

Alihimiza waamini washiriki katika liturujia, aliyoipamba kwa ubunifu izidi kupendeza.

Alipambana kwa nguvu na uzushi na kuleta nidhamu katika majimbo yaliyo chini yake, akiwafukuza mapadri wengi wasiofaa, na hata askofu wa Efeso na wengine watano waliopata madaraka kwa dhambi ya usimoni. Kwa hilo alilaumiwa kuwa alitumia mamlaka nje ya mipaka yake.

Pia alilazimisha wamonaki wazururaji warudi katika monasteri zao, ila alipokea wengine kutoka Misri waliokuwa wametengwa na Kanisa kwa uamuzi wa Patriarki Teofilo wa Aleksandria, ambaye alichukia hilo pia.

Mwanzoni alitegemezwa na ikulu, lakini baada ya kumlaumu malkia Eudoksia kwa kujipatia mali ya mjane na kuishi kwa anasa, uhusiano uliharibika, akazidi kusingiziwa na kutukanwa.

Mwaka 402 maadui wake wengi, wakiwemo maaskofu, waliomba msaada wa patriarki Teofilo wa Aleksandria, ambaye Kanisa lake lilikuwa na ushindani na yale ya Konstantinopoli na Antiokia. Teofilo mwenyewe alikuwa amelazimika kujitetea katika sinodi iliyoongozwa na Yohane kuhusu mashtaka ya wamonaki dhidi yake.

Basi, mwaka 203 katika sinodi ya Mwaloni, karibu na Kalsedonia, Teofilo alifika pamoja na maaskofu saba wa Misri na wengine 29 waliokuwa wote upande wake, akamfanya Yohane afukuzwe na Kaisari, ila kesho yake malkia alimrudisha baada ya umati kudai hivyo kwa nguvu.

Miezi miwili baadaye uhusiano wa Yohane na Eudoksia ulichafuka tena, askofu alipolaumu ujenzi wa sanamu ya malkia karibu na kanisa, hata alisema maadhimisho kwa ajili yake yalikuwa ya kipagani akamfananisha na Herodia mwenye hamu na kichwa cha Yohane Mbatizaji.

Hivyo masingizio na njama viliendelea hata aliomba msaada wa Papa Inosenti I na maaskofu wengine muhimu wa magharibi, lakini huo haukuweza kuwahi: mtaguso, uliotakiwa na Kanisa la Roma ili kupatanisha pande mbili za Dola na makanisa yake yote, haukuweza kufanyika.

Uhamishoni hariri

Basi, tarehe 9 Juni 404 Yohane alifukuzwa jimboni moja kwa moja. Kwa miaka mitatu aliishi Kukuso, kwenye milima ya Armenia, akitenda kazi kubwa hata kwa kuandika barua nyingi ili kuwatia moyo wafuasi wake waliodhulumiwa vilevile.

Halafu mwaka 407, kutokana na wingi wa watu waliomtembelea, alihamishwa tena aende mahali pagumu zaidi, huko Pitiunte, mashariki kabisa kwa Bahari Nyeusi, lakini tarehe 14 Septemba 407 alifariki huko Comana Pontica akiwa njiani.

Maneno yake ya mwisho yalikuwa: "Utukufu kwa Mungu kwa yote. (Doxa to Theo pantôn eneke)."

Mwaka 438 Kaisari mwingine, Theodosi II alirudisha masalia yake Konstantinopoli ambako yalipokewa na umati kwa shangwe.

Maandishi yake ni mengi sana, kuliko ya mababu wengine wote wa Kigiriki. Sehemu kubwa ni mahubiri (zaidi ya 700) aliyoyatoa kwa kawaida wakati wa liturujia, vitabu vya ufafanuzi wa Biblia, vya teoloja n.k. mbali ya barua 241 zilizotufikia.

Teolojia yake hariri

Kama alivyopendekeza mwenyewe kwa waamini wake baada ya yeye kupelekwa uhamishoni, tunaweza kujilisha maandishi yake badala ya kumsikia akihubiri.

Kwa jumla hakuwa mwanateolojia mwenye mwelekeo wa nadharia, bali wa kichungaji, akilenga daima maisha yaendane na mawazo na maneno. Ndiyo mada kuu ya katekesi zake bora kwa waliojiandaa kubatizwa. Akikaribia kifo, aliandika kwamba thamani ya binadamu inategemea “ujuzi sahihi wa mafundisho ya kweli na unyofu wa maisha”: hayo mawili yanatakiwa kuendana.

Aliendeleza mapokeo ya Kanisa na kutoa mafundisho ya kuaminika wakati wa fujo kuhusu imani.

Alifundisha “kujua viumbe kuanzia Muumba”, ili viwe kama ngazi ya kumfikia. Zaidi ya hayo, kwa kuwa kwetu ni vigumu kufanya hivyo, Mungu mwenyewe alijishusha akatupa Maandiko matakatifu kama barua inayokamilisha ujuzi wetu juu yake. Isitoshe, alitwaa mwili akawa kweli “Mungu pamoja nasi”, ndugu yetu hata kifo chake msalabani. Hatimaye yeye anaingia maisha yetu kwa njia ya Roho Mtakatifu ili kutugeuza kwa ndani.

Kuhusu Kristo, Yohane alimkiri Mwana kuwa na hali moja na Baba. Pia kwamba alizaliwa na Maria, bikira kabla ya kujifungua, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua.

Anaitwa pia “Mwalimu wa Ekaristi” kutokana na upana na utajiri wa mafundisho yake kuhusu sakramenti ya Mwili na Damu ya Kristo.

Tanbihi hariri

Tazama pia hariri

Vyanzo hariri

  • Allen, Pauline and Mayer, Wendy (2000). John Chrysostom. Routledge. ISBN 0-415-18252-2
  • Attwater, Donald (1960). St. John Chrysostom: Pastor and Preacher. London: Catholic Book Club.
  • Blamires, Harry (1996). The New Bloomsday Book: A Guide Through Ulysses. London: Routledge. ISBN 0-15-3858-.
  • Brändle, R., V. Jegher-Bucher, and Johannes Chrysostomus (1995). Acht Reden gegen Juden (Bibliothek der griechischen Literatur 41), Stuttgart: Hiersemann.
  • Brustein, William I. (2003). Roots of Hate: Anti-Semitism in Europe before the Holocaust. Cambridge University Press. ISBN 0-521-77308-3
  • Carter, Robert (1962). "The Chronology of St. John Chrysostom's Early Life." Traditio 18:357–64.
  • Chrysostom, John (1979). Discourses Against Judaizing Christians, trans. Paul W. Harkins. The Fathers of the Church; v. 68. Washington: Catholic University of America Press.
  • Dumortier, Jean (1951). "La valeur historique du dialogue de Palladius et la chronologie de saint Jean Chrysostome." Mélanges de science religieuse, 8, 51–56.
  • Hartney, Aideen (2004). John Chrysostom and the Transformation of the City. London: Duckworth. ISBN 0-520-04757-5.
  • Joyce, James (1961). Ulysses. New York: The Modern Library.
  • Kelly, John Norman Davidson (1995). Golden Mouth: The Story of John Chrysostom-Ascetic, Preacher, Bishop. Ithica, New York: Cornell University Press. ISBN 0-8014-3189-1.
  • Laqueur, Walter (2006). The Changing Face of Antisemitism: From Ancient Times To The Present Day. Oxford University Press. ISBN 0-19-530429-2.
  • Liebeschuetz, J.H.W.G. (1990) Barbarians and Bishops: Army, Church and State in the Age of Arcadius and Chrysostom. Oxford: Clarendon Press. ISBN 0-19-814886-0.
  • Lewy, Yohanan [Hans] (1997). "John Chrysostom". Encyclopaedia Judaica (CD-ROM Edition Version 1.0). Ed. Cecil Roth. Keter Publishing House. ISBN 965-07-0665-8.
  • Meeks, Wayne A., and Robert L. Wilken (1978). Jews and Christians in Antioch in the First Four Centuries of the Common Era (The Society of Biblical Literature, Number 13). Missoula: Scholars Press. ISBN 0-89130-229-8.
  • Palladius, Bishop of Aspuna. Palladius on the Life And Times of St. John Chrysostom, transl. and edited by Robert T. Meyer. New York: Newman Press, 1985. ISBN 0-8091-0358-3.
  • Parks, James (1969). Prelude to Dialogue. London.
  • Parry, David; David Melling (editors) (2001). The Blackwell Dictionary of Eastern Christianity. Oxford: Blackwell. ISBN 0631189661. 
  • Pradels, W. (2002). "Lesbos Cod. Gr. 27 : The Tale of a Discovery", Zeitschrift für Antikes Christentum 6, pp. 81–89.
  • Pradels, W., R. Brändle, and M. Heimgartner (2001). "Das bisher vermisste Textstück in Johannes Chrysostomus, Adversus Judaeos, Oratio 2", Zeitschrift für Antikes Christentum 5, pp. 23–49.
  • Pradels, W., R. Brändle, and M. Heimgartner (2002). "The sequence and dating of the series of John Chrysostom's eight discourses Adversus Judaeos", Zeitschrift für Antikes Christentum 6, 90-116.
  • Schaff, Philip, and Henry Wace (eds.) (1890). Socrates, Sozomenus: Church Histories (A Select Library of Nicene and post-Nicene Fathers of the Christian Church, second series, vol. II). New York: The Christian Literature Company.
  • Stark, Rodney (1997). The Rise of Christianity. How the Obscure, Marginal Jesus Movement Became the Dominant Religious Force in the Western World in a Few Centuries. Princeton University Press.
  • Stephens, W.R.W. (1883). Saint John Chrysostom, His Life and Times. London: John Murray.
  • Stow, Kenneth (2006). Jewish Dogs, An Imagine and Its Interpreters: Continiuity in the Catholic-Jewish Encounter. Stanford: Stanford University Press. ISBN 0-8047-5281-8.
  • Wilken, Robert Louis (1983). John Chrysostom and the Jews: Rhetoric and Reality in the Late Fourth Century. Berkeley: University of California Press.
  • Willey, John H. (1906). Chrysostom: The Orator. Cincinnati: Jennings and Graham.
  • Woods, Thomas (2005). How the Catholic Church Built Western Civilization. Washington, D.C.: Regenery. ISBN 0-89526-038-7

Viungo vya nje hariri

Maandishi yake hariri

Mengineyo hariri