Al-Masudi (kwa Kiarabu المسعودي, jina kamili أبو الحسن علي بن الحسين بن علي المسعودى , Abu Hassan'Alī ibn al-Husayn bin al-al-Mas'ūdī; 896 hivi - 956) alikuwa mwanahistoria, mwanajiografia na mpelelezi Mwarabu. Wakati mwingine huitwa "Herodoti wa Waarabu". [1] [2]

Sanamu ya Al-Masudi (ya kisasa), kwenye paa ya makumbusho ya Historia ya Viumbe, Vienna (Austria)

Al-Masudi alikuwa mwandishi mashuhuri kwa kuunganisha historia na jiografia ya kitaalamu katika kitabu chake kikubwa "Malisho ya Dhahabu na Migodi ya Almasi" (kwa Kiarabu مروج الذهب و معادن الجوهر‎, muruj adh-dhahab wa ma'adin al-jawhar) alimolenga kutoa taarifa ya historia ya dunia. Alitunga kwa jumla zaidi ya vitabu 20 kuhusu mada za kidini na utaalamu wa jumla pamoja na historia, jiografia, sayansi, falsafa na dini.[3]

Maisha, safari na maandiko hariri

Maakuna habari zaidi kuhusu Al-Masudi bali na zile anazotaja mwenyewe katika maandiko yake. Alizaliwa huko Baghdad akitoka katika ukoo wa Abdullah Ibn Mas'ud sahaba wa Mtume Muhammad . Al-Masudi alitaja majina ya wataalamu wengi aliofahamu kwenye safari zake katika nchi nyingi. Watafiti wengine wanaonyesha mashaka kama taarifa zote kuhusu safari zake ni kweli lakini inakubaliwa ya kwamba aliona nchi nyingi.

"Alitumia sehemu kubwa ya maisha kwa safari zake kuanzia mnamo 903/915 BK hadi mwisho wa maisha yake. Alisafiri katika Uajemi (Iran), Armenia, Georgia na nchi za Bahari Kaspi pamoja na Uarabuni, Syria na Misri. Alipita katika sehemu za Bara Hindi hasa kwenye pwani la magharibi akasafiri mara kadhaa hadi Afrika ya Mashariki. Kwa jahazi alivuka Bahari Hindi, Bahari ya Shamu, Ghuba la Uajemi na Bahari Mediteranea."

Wakati mwingine Sri Lanka na China hutajwa kati ya nchi alizotembelea lakini tunajua ya kwamba habari alizotoa kuhusu China aliwahi kupokea kutoka kwa Abu Zaid al-Sirafi ambaye alikutana nayd kwenye Ghuba la Uajemi. [4] Nchini Syria al-Masudi alikutana na Leo wa Tripoli, mwanajeshi kutoka Bizanti aliyewahi kubadilisha dini na kuwa Mwislamu. Kutoka huyu aliweza kujifunza mengi kuhusu milki ya Bizanti. Miaka yake ya mwisho al-Masudi aliishi Misri.

Haijulikani jinsi alivyoweza kugharamia safari zake. Hivyo wengi wanafikiri ya kwamba aliendesha shughuli za biashara. [5]

Elimu katika mazingira ya Al-Masudi hariri

Wanahistoria Lunde na Stone wanaeleza mazingira alimoishi al-Masudi:

"Aliishi wakati ambapo vitabu vilipatikana kwa urahisi na kwa bei nafuu. Miji mikubwa kama Baghdad ilikuwa na maktaba maarufu. Lakini hata watu wengi pamoja na marafiki wa Masuudi walikuwa na maktaba ya kibinafsi, mara nyingi yaliyo na maelfu ya maandiko. Kuenea kwa vitabu kwa bei ya chini kulikuwa tokeo la kufika kwa uzalishaji wa karatasi katika nchi za Waislam baada ya kukamatwa kwa mafundi wa karatasi kutoka China katika mapigano ya Talas kwenye mwaka 751. Miaka michache baada ya mapigano haya viwanda vya karatasi vilianza kupatikana katika miji mikubwa. Kupatikana kwa karatasi kulitokea wakati nasaba ya Wabbasi ilianza kutawala. Hakuna shaka kuwa upatikanaji wa vifaa vya kuandika kwa bei nafuu nafuu ulichangia kwenye mfumo wa utawala wa Wabbasi, huduma ya posta, na upanuzi wa elimu.[6]"

Wanahistoria wanaona ya kwamba Masudi mara nyingi anawawahimiza wasomaji wake kusoma pia vitabu vingine ambavyo aliandika, akitarajia kuwa hivi vnapatikana kwa wasomaji wake. Mazingira haya ambako vitabu viipatikana bila matatizo yalikuwa tofauti sana na hali ya elimu huko Ulaya wakati ule.

Al-Masudi alikuwa mwanafunzi au mwalimu pamoja na wataalamu maarufu, ikiwa ni pamoja na wanaisimu al-Zajjaj, Ibn Duraid , Niftawayh na Ibn Anbari. Alikufahamiana na washairi maarufu kama Kashajim, ambaye labda alikutana naye huko Aleppo . Alijua vizuri sana maandiko ya wanafalsafa kama al-Kindi na al-Razi , mafundisho ya al-Farabi (aliyefuata itikadi ya Aristoteli) na maandiko ya Plato yaliyotafsiriwa kwa Kiarabu.

Alifahamu pia maandiko ya Galenos kuhusu matibabu, ya Ptolemaio kuhusu astronomia, jiografia ya Marinus na vitabu vya wataalamu Waislamu kuhusu jiografia na astronomia.

Al-Masudi aliingiza pia habari za ustaarabu wa kale uliowahi kupatikana kwenye nchi ambako Uislam ulienea baadaye. Alitaja Waashuri , Wababeli , Wamisri na Waajemi pamoja na mataifa mengine ya kale.

Safari katika nchi nje ya Uislam hariri

 
Ramani ya dunia ya Al-Masudi ya dunia (iligeuzwa kwa picha hii; kiasili ilionyesha kusi ni juu, jinsi inavyoonekana kwenye maandishi yake ya Kiarabu)

Al-Masudi alikuwa tofauti na wataalamu wa wakati wake kwa kutafuta pia habari za nchi na watu nje ya Uislamu. Alieleza hali ya nchi nyingi zilizokuwa nje ya Ukhalifa wa Wabbasi pamoja na utamaduni na dini zao.

Hata alikusanya habari kadhaa kuhusu watu walioishi mbali sana kama Urusi na Uingereza ambako hakuwahi kufika. Alitaja Paris kuwa mjji mkuu wa Wafranki (baadaye Ufaransa).

Al-Masudi alikusanya pia habari za Afrika. Alitaja yale aliyosikia kuhusu Afrika ya Magharibu na milki za Zagawa, Kawkaw na Ghana ya Kale. Afrika ya Mashariki alitembelea mwenyewe akakusanya habari watu wake waliotwa Zanj.

Matoleo na tasiri ya maandiko yake hariri

Tafsiri kamili ya Kifaransa ya "Malisho ya Dhahabu " ilichapishwa pamoja na matini ya Kiarabu katika Paris na Societe Asiatique kwenye vitabu tisa kati ya 1861 na 1877. Barbier de Meynard na Pavet de Courteille walikuwa wafasiri wa Kifaransa kwa toleo hili. Karne moja baadaye, kati ya 1966 na 1974, Charles Pellat alirekebisha matini ya Kiarabu kwenye toleo sahihi zaidi iliyochapishwa kwenye vitabu tano na Chuo Kikuu cha Lebanoni huko Beirut.

Aloys Sprenger alitoa tafsiri ya Kiingereza ya sehemu ya kwanza ya "Meadows of Gold and Mines of Gems" mwaka 1841 mjini London [7]

Tafsiri ya Lunde na Stone kwa Kiingereza ya maelezo kuhusu Wabbasi iliotolewa mwaka 1989.

Sifa zake kati ya Waislamu hariri

Wasunni mara nyingi wanamkosolea kwa sababu wanaona aliathiriwa na Washia na Wamutazila. Kwa mfano, Ibn Hajar anaandika kuhusu al-Masudi kwamba "vitabu vyake havikufahamika kwa sababu alikuwa Shi'a na Mu'tazila." . [8] Adh-Dhahabi [9] na Taj al-Din kama-Subki pia walithibitisha kwamba walimwona kuwa Mu'tazila. [10]

Marejeo hariri

  1. "Al Masudi". History of Islam. 
  2. Ter-Ghevondyan, Aram N. (1965). Արաբական Ամիրայությունները Բագրատունյաց Հայաստանում (The Arab Emirates in Bagratuni Armenia) (kwa Kiarmenia). Yerevan, Armenian SSR: Armenian Academy of Sciences. uk. 15. 
  3. John L. Esposito (ed.), Dictionary ya Oxford ya Uislamu , Oxford University Press (2004), p. 195
  4. Masudi. Meadows of Gold, the Abbasids . Paul Lunde na Caroline Stone, Kegan Paul. London and New York, 1989, p. 11.
  5. Mas‘udi. The Meadows of Gold, The Abbasids. Transl. Paul Lunde and Caroline Stone, Kegan Paul. London and New York, 1989, p. 11.
  6. Mas'udi. The Meadows of Gold, The Abbasids, p. 14.
  7. https://archive.org/details/historicalencycl00masrich Meadows of Gold and Mines of Gems Vol 1
  8. Lisan al-Mizan [258-256 / 4]
  9. Siyar A'alam al-Nubala [Tabaqa al-'Ishroon / al-Mas'oodi]
  10. Tabaqat al-Shafi'iyyah al-Kubra [Wasifu: 226]