Bendera
Bendera ni kitambaa chenye rangi mbalimbali. Mara nyingi ina umbo la pembenne, pia la mraba au pembetatu. Ina kazi ya kitambulisho au alama ya mawasiliano.
Bendera kama kitambulisho
haririMara nyingi bendera ni alama ya kitambulisho cha taifa au jumuiya nyingine.
Nchi inweka bendera yake kwa kuonyesha: hapa eneo letu linaanza; au: leo tunaonyesha bendera kwa sababu ni sikukuu ya taifa. Serikali zinaweza kuweka bendera mbele ya majengo rasmi ikonyesha: hapa ndipo jengo rasmi kama kituo cha polisi, shule, nyumba ya wizara na kadhalika.
Mji una bendera ukiitumia kama serikali ya nchi katika eneo lake.
Klabu ya soka inaweza kuwa na bendera. Bendera ya klabu inaonyeshwa na wafuasi wake uwanjani kwa kusidi la kuwaonyesha wachezaji kuwa wenzao wako.
Bendera vitani
haririBendera zilikuwa kati ya alama muhimu vitani. Vikosi mbalimbali vilikuwa na bendera zao zilizowasaidia wanajeshi kutambua jeshi lao liko sehemu gani kama walitengwa na wenzao wengine katika mapigano ya watu maelfu.
Bendera kama alama ya mawasiliano
haririMatumizi ya kale kabisa ya mabendera ni kuwasilisha habari. Matumizi haya yanahitaji uelewano kuhusu maana ya rangi zinazoonyeshwa. Rangi mbalimbali pamoja zinaweza kumaanisha maneno, herufi au amri. Bendera zenye rangi hizi zinaonekana kwa umbali wa wastani unaotegemea ukubwa wa bendera. Utaratibu huu uliwahi kutumika kati ya meli baharini tangu karne nyingi.
Hadi leo meli zinatumia mawasiliano ya bendera hata siku hizi za simu na redio. Lakini bendera zinasaidia kama mitambo imeharibika au kama meli mbili zinakutana zisizojua marudio ya redio ya meli nyingine.
Matumizi haya ni kawaida pia katika michezo fulani, kwa mfano mshika bendera kwenye soka au alama ya mwanzo mbioni.