Darajani Chawl, Zanzibar

Darajani Chawl (pia: Jumba la treni) ni jengo la kihistoria lenye usanifu wa kutoka India [1] ambalo liko Darajani, Mji Mkongwe huko Zanzibar. [2]

Majina

hariri

Neno Chawl linatokana na moja kati ya lugha za Kihindi (Kimarathi) likihusika zaidi na mtindo wa ujenzi wa jengo lenyewe, kawaida huwa ni marefu yenye urefu wa ghorofa 4 mpaka 5.[3]

Watu wa Zanzibar wameliita Jumba la treni kutokana na muonekano wa umbile lake ambalo ni kama treni.[3]

Historia

hariri

Ujenzi wa jengo la Darajani Chawl uliamuliwa na Barghash bin Said aliyekuwa sultani wa tatu wa Zanzibar mnamo 1880 kwa jaribio la kutaka kuongeza mapato kwa serikali yake. Hivyo, ghorofa ya chini ilibuniwa kwa ajili ya maduka na stoo na ghorofa ya kwanza kwa ajili ya makazi ya Wahindi. Mpaka mnamo 1900 familia 160 zilikuwa zikiishi hapo.[1] [4]

Serikali ya mapinduzi ililitaifisha mnamo 1964 mara baada ya mapinduzi na kuliweka chini ya wizara iliyohusika na nyumba katika Idara ya mamlaka ya Mji Mkongwe.[3]

Darajani Chawl siku hizi

hariri

Hapo awali jengo lilitumika kwa ajili ya biashara na makazi, lakini kutokana na uchakavu wa jengo lenyewe mnamo 2016 shughuli zote katika jengo hilo zilisimamishwa kupisha ukarabati chini ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa Zanzibar (ZSSF). Matengenezo na maboresho yaliyofanywa yalikuwa na madhumuni yaleyale ya kuwa chanzo cha mapato ili kukuza uchumi wa wananchi na nchi kwa ujumla.[3]

Mnamo Agosti 2018, jengo lilifunguliwa rasmi na aliyekuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Mohamed Ali Shein na kuwekwa chini ya ZSSF kukodisha nafasi za kufanyia biashara.

Jumba lina nafasi kwa ajili ya maduka 52 ya biashara, sehemu 2 za "ATM", eneo la kusalia kwa wanawake, nyumba 10 za kuishi, mgahawa, sehemu za kufanyia mazoezi ya mwili na duka la mahitaji mbalimbali "Supermarket".[3] [5]

Tazama pia

hariri

Marejeo

hariri
  1. 1.0 1.1 https://www.slideshare.net/MbarakaSaidi/final-zanzibar-documentaion-project1
  2. "Nakala iliyohifadhiwa". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2021-05-10. Iliwekwa mnamo 2021-05-10.
  3. 3.0 3.1 3.2 3.3 3.4 "Nakala iliyohifadhiwa". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2021-05-10. Iliwekwa mnamo 2021-05-10.
  4. "Nakala iliyohifadhiwa". Ilihifadhiwa kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2021-05-12. Iliwekwa mnamo 2021-05-10.
  5. http://www.zanzinews.com/2018/08/ufunguzi-wa-jengo-la-chawl-building.html