Ganimedi (Mshtarii)

(Elekezwa kutoka Ganymedi)

Ganimedi (ing. Ganymede) ni mwezi mkubwa zaidi wa Mshtarii (Jupiter) ambayo ni sayari ya tano kutoka kwa Jua na sayari kubwa katika mfumo wa Jua. Ni pia mwezi mkubwa katika mfumo wa Jua.

Picha ya Ganimedi

Kipenyo cha Ganimedi ni kilomita 5262 km hivyo ni kubwa kuliko sayari ya kwanza Utaridi (Mercury). Lakini ina nusu ya masi yake tu maana haina kiasi hiki cha densiti.

Ganimedi ni mmoja wa miezi ya Mshtarii iliyotambuliwa mnamo mwaka 1610 na Galileo Galilei aliyekuwa mtu wa kwanza kutazama nyota kwa kutumia darubini.

Jina la Ganymedi ilichaguliwa baadaye na wataalamu waliotaka kukumbuka jina la mtumishi wa mungu mkuu Jupiter katika mitholojia ya Kiroma.

Masi ya Ganimedi ni takriban nusu mwamba na nusu maji. Kwenye kitovu chake kuna kiini kidogo cha metali hasa chuma. Uso wake unafunikwa kote na barafu yenye unene wa kilomita mamia. Chini ya uso wa barafu iko bahari ya maji katika hali ya kiowevu[1]. Kuna makadirio ya kwamba kiasi cha maji kwenye Ganimedi kinazidi jumla ya maji Duniani.[2]

Uso wa Ganimedi umejaa kasoko kutokana na migongano ya asteroidi.

Marejeo

  1. NASA’s Hubble Observations Suggest Underground Ocean on Jupiter's Largest Moon, tovuti ya NASA tar. March 12, 2015, iliangaliwa Mei 2018
  2. Jupiter moon Ganymede could have ocean with more water than Earth – NASA , tovuti ya Russia Today ya 13 Mar, 2015, iliangaliwa Mei 2018