Gold Coast (kwa Kiswahili: Pwani ya Dhahabu) ilikuwa jina la koloni la Uingereza katika Afrika ya Magharibi kwenye mwambao wa Ghuba ya Guinea ambalo limekuwa nchi ya Ghana tangu uhuru wake (1957).

Koloni ya Gold Coast mnamo 1896
Vita kati ya Waingereza na Waashanti

Historia

hariri

Vyanzo kwenye pwani

hariri

Vyanzo vya koloni vilikuwa vituo vya wafanyabiashara kutoka Ulaya waliofika sehemu hii ya pwani tangu karne ya 15 kwa biashara ya dhahabu, watumwa, visu, vioo, pombe kali na silaha kama bunduki. Kituo cha kwanza kilikuwa boma la Elmina lililojengwa na Wareno.

Kuanzia mwaka 1800 milki ya Ashanti ilianza kupanuka hadi pwani. Hapo kulitokea vita kati ya Ashanti na milki za pwani. Ashanti ilidai kodi kutoka kwa hao wageni na mwaka 1817 shirika la wafanyabiashara Waingereza lilikubali malipo. Wakati ule Waingereza walianza kuchukua hatua za kukandamiza biashara ya watumwa wakiwa na makao makuu katika Sierra Leone na manowari za Kiingereza zilipita kwenye pwani.

Mwaka 1821 vituo vya Kiingereza kwenye Pwani ya Dhahabu viliwekwa chini ya gavana wa Sierra Leone. Wafanyabiashara na walowezi Waingereza waliomba pwani hii iwe koloni kabisa. Hapo walikuwa na matumaini ya ulinzi dhidi ya Ashanti wakidokeza ya kwamba Ashanti iliendelea kufanya biashara ya watumwa iliyowahi kupigwa marufuku na nchi za Ulaya katika Mkutano wa Vienna wa mwaka 1815. Lakini serikali ya London ilikataa kuanzisha koloni kamili kwa sababu waliona gharama za koloni zisingelingana na mapato. Vituo vya pwani viliwekwa chini ya usimamizi wa gavana wa Sierra Leone. Waingereza walipigania vita kuhusu vituo vyao na usalama wa falme za pwani dhidi ya Ashanti katika miaka 1823-1831 wakifaulu hatimaye kupanua eneo lao hadi km 120 kutoka pwani.

Maeneo lindwa na koloni tangu 1873

hariri

Wakati wa vita na baadaye Waingereza waliimarisha ushirikiano wao na falme za pwani. Tangu mkataba wa mwaka 1844 hali ya pwani ilikuwa kama mkusanyiko wa maeneo ya kulindwa chini ya Uingereza.

Baada ya vita vya 1872/1873 dhidi ya Ashanti Uingereza ilifuta mapatano ya 1844 na kutangaza maeneo yote kati ya pwani na Asante kuwa koloni kamili. Gavana Mwingereza alichukua boma la Christiansborg (Accra) kuwa makao makuu yake.

Miaka 1895/1896 ilitokea tena vita kati ya Waingereza na Ashanti. Waingereza waliona upanuzi wa makoloni ya Ufaransa na Ujerumani katika Afrika ya Magharibi wakadai Ashanti ikubali kuwa nchi lindwa ya Uingereza. Asantehene alipokataa Waingereza walishambulia wakachoma Kumasi. Ashanti ililazimishwa kusalimu amri na kuwa eneo lindwa.

Mnamo 1902 maeneo upande wa kaskazini wa Ashanti yaliongezwa kufuatana na mapatano na Ujerumani na Ufaransa. Kwa hiyo sehemu tatu za Gold Coast yenyewe, Ashanti na maeneo ya kaskazini yalikuwa koloni moja chini ya gavana wa Accra.

Gold Coast

hariri
 
Stempu ya posta ya mwaka 1953

Tangu 1919 gavana aliwajibika pia kwa sehemu ya Togo ya Kiingereza (maeneo ya Togo ya Kijerumani ya awali zilizokabidhiwa kwa Uingereza) iliyotawaliwa kama "Togo ng'ambo ya mto Volta". Wakati wa mwisho wa ukoloni wakazi wengi wa sehemu hiyo walipiga kura ya kujiunga na Gold Coast na sasa ni sehemu kamili ya Ghana.

Utawala ulikuwa mikononi mwa gavana. Lakini mapema sana gavana aliunda halmashauri mbili kuwa kamati za kushauriana. Mwanzoni aliita Wazungu pekee kuwa wanachama wa halmashauri lakini kuanzia mwaka 1900 Waafrika kadhaa waliungwa pia. Katika sehemu kubwa ya eneo Waingereza walitegemea mfumo wa utawala usio wa moja kwa moja yaani kupitia machifu wazalendo. Idadi ya Waafrika wenye elimu ya kisasa ilikua na tangu mwaka 1920 walianza kudai halmashauri ya kuchaguliwa, si ya kuteuliwa na gavana.

Kuelekea uhuru

hariri
 
Shule ya Ufundi katika maeneo ya kaskazini kabla ya uhuru 1957

Mwaka 1946 gavana mpya aliunda katiba ya koloni iliyowapa wajumbe wachaguliwa kura nyingi katika halmashauri kuu (legislative council). Harakati za kudai haki zaidi kwa wazalendo ziliendelea kupata nguvu. Chama cha United Gold Coast Convention (UGCC) kilidai haki ya kujitawala tangu mwaka 1947.

Miaka miwili baadaye, kwenye Juni 1949, chama kipya cha Convention People's Party (CPP) kiliundwa na Kwame Nkrumah. Madai yake yalikuwa makali zaidi, yaani serikali ya kuchaguliwa ianzishwe mara moja. Nkrumah alitumia mikutano ya hadhara, maandamano na migomo kwa kutangaza madai yake. Katika uchaguzi wa mwaka 1951 chama cha CPP kilishinda na Nrumah akawa waziri mkuu wa koloni.

Ndani ya koloni wawakilishi kutoka kaskazini na Ashanti walitaka kuwa mfumo wa shirikisho wakiogopa Nkrumah alilenga kukusanya mamlaka yote mikononi mwake. Hata hivyo, serikali ya Uingereza ilisimama upande wa CPP na hivyo koloni liliingia katika uhuru tarehe 6 Machi 1957 kwa jina la Ghana.

Marejeo

hariri
  • I Kimble, David (1963). A Political History of Ghana: The Rise of Gold Coast Nationalism, 1850–1928. Oxford: Clarendon Press.
  • McLaughlin, James L. and David Owusu-Ansah. "Historical Setting" (and sub-chapters). In A Country Study: Ghana (La Verle Berry, ed.). Library of Congress Federal Research Division (November 1994). This article incorporates text from this source, which is in the public domain.
  • Quartey, Seth (2007). Missionary Practices on the Gold Coast, 1832–1895: Discourse, Gaze and Gender in the Basel Mission in Pre-Colonial West Africa. Youngstown, New York: Cambria Press. ISBN 978-1-62499-043-4.
  • Gyasi, Yaa (2016). Homegoing. New York, NY: Knopf.
  Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Gold Coast kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.