Haki za watoto
Haki za watoto ni kimoja kati ya vifungu vya haki za binadamu[1] ambacho kinalenga hasa watoto[2].
Mapatano ya kimataifa juu ya Haki za Watoto yamekubaliwa na wanachama wa Umoja wa Mataifa. Watoto wanafafanuliwa kuwa "mtu yeyote mwenye umri chini ya miaka kumi na nane"[3].
Haki za watoto zinajumuisha haki ya kushirikiana na wazazi wote wawili, kutambuliwa kibinadamu na mahitaji ya msingi ya ulinzi wa mwili, chakula, elimu, huduma ya afya, na sheria zinazofaa kwa ukuaji wa mtoto, haki za kiraia za mtoto, uhuru wa kutokubaguliwa kutokana na rangi, jinsia, asili ya kitaifa, ulemavu, dini, kabila au sifa nyingine. Vile vile tafsiri ya haki za watoto zinalenga zaidi kuwapa watoto kuwa huru kimwili, kiakili na kimihemko kutokana na dhuluma na unyanyasaji. tafsiri nyingine ni pamoja na malezi na utunzaji wa mtoto.
"Haki za vijana" (Kiing. Youth Rights) zinajadiliwa pekee lakini hakuna mapatano ya kimataifa.
Haki ya kuishi
Hii inaanza pale mama anapopata ujauzito. Kukua vizuri kwa mimba kunategemea afya, lishe na mazingira anamoishi mama. Pia kuishi kwa mtoto baada ya kuzaliwa kunategemea upatikanaji wa mahitaji ya msingi, ambayo ni chakula cha kutosha na chenye ubora unaotakiwa, huduma bora za afya na ulinzi toka kwa wazazi, jamii na Serikali. Vifo vya watoto wadogo hutokana na ukosefu wa moja ya mahitaji tajwa hapo juu.
Haki ya kuendelezwa
Kwa mujibu wa Sera ya Maendeleo ya Mtoto Tanzania, maendeleo ya mtoto yanahusiana na mtoto kuwa na kiwango kinachokidhi makuzi kimwili, kiakili, kiroho, kimaadili na kijamii. Ili mtoto aweze kukua vizuri anahitaji kutunzwa, kuongozwa na kulelewa katika misingi mizuri. Mathalani, kuendelezwa kwa mtoto kimwili ni kukua kimaumbile na uzito kwa uwiano wa umri. Hali hii inategemea lishe na huduma bora za afya ikiwemo kupatiwa chanjo zote muhimu na upatikanaji wa viinilishe vyote muhimu. Maendeleo ya mtoto yanahitaji jitihada toka kwa mzazi, jamii na Serikali kwa pamoja.
Haki ya kulindwa
Inahusu kuzuia vitendo viovu wanavyofanyiwa watoto katika hatua za ukuaji wao, kabla na baada ya kuzaliwa. Mathalani, mtoto anahitaji ulinzi dhidi ya kazi nzito zisizowiana na umri wake, kudhulumiwa mali hasa kwa watoto yatima, kutupwa au kutelekezwa na wazazi, utoaji mimba wa makusudi, kuonewa nk. Sera ya Maendeleo ya Mtoto Tanzania pia inasisitiza juu ya ulinzi dhidi ya unyanyasaji wa mtoto ikiwemo kukeketwa, kulazimisha kuolewa/kuoa katika umri mdogo, ubakaji, nk.
Haki ya kushiriki
Ushiriki wa mtoto unapatikana pale mtoto anapopewa nafasi kikamilifu katika kutoa mawazo, kushiriki katika maamuzi ya masuala yanayohusu maendeleo yake, nk. katika hatua mbalimbali za ukuaji wake. Kitaalamu hatua za ushiriki wa mtoto huanza rasmi kuanzia umri wa miaka mitatu hadi anapokuwa mtu mzima. Misingi ya ushiriki wa mtoto huzingatia umri na aina ya masuala anayopaswa kushirikishwa.
Haki ya kutobaguliwa
Ubaguzi wa mtoto umegawanyika katika makundi mbalimbali, katika yote yapo makundi makuu mawili. Ubaguzi wa kijinsia ambao mtoto wa kike au wa kiume anaweza kubaguliwa na wazazi, walezi au jamii. Upo ubaguzi unaotokana na hali yake ya kimaisha kama vile utajiri au umasikini, ulemavu, ugonjwa, uyatima na jinsi anavyoonekana mbele za watu. Mfano wa kuumiza ni ubaguzi wa kimfumo ambapo hapa kwetu takwimu zinaonyesha kwamba ni asilimia moja tu ya watoto wenye ulemavu wanoandikishwa kujiunga na elimu ya msingi. Hii inaathiriwa na mtazamo wa kijamii dhidi ya watoto hawa kwani wazazi huwafungia ndani ili kuficha aibu na hivyo kuwanyima fursa ya kupata elimu.
Marejeo
Makala hii kuhusu mambo ya sheria bado ni mbegu. Je, unajua kitu kuhusu Haki za watoto kama historia yake au uhusiano wake na mada nyingine? Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa? Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari. |