Historia ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Historia ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inahusu eneo la Afrika ya Kati, hasa katika beseni la mto Kongo, ambalo wakazi wake leo wanaunda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ni moja ya nchi zilizobarikiwa zaidi kwa madini, misitu, maziwa na mito.

Historia ya kale hariri

Wakazi wa kwanza huaminiwa kuwa wawindaji wa jamii ya Wasani na ya Wabilikimo.

Katika karne za BK walifika wahamiaji Wabantu wenye ujuzi wa kilimo na uhunzi.

Jina la Kongo lahusiana na mto Kongo unaopitia nchi yote na pia Ufalme wa Kongo uliopatikana zamani katika sehemu za magharibi za Angola na Kongo ya leo.

Mnamo karne ya 15, wakati wapelelezi wa kwanza Wareno walipofika kwenye pwani za Afrika, milki kubwa katika nchi ya Kongo ya magharibi pamoja na Angola ya kaskazini ilikuwa Ufalme wa Kongo. Wakati wa uenezaji mkuu ufalme huu ulianza kwenye mwambao wa Atlantiki na kuendelea hadi mto Kwango kwenye mashariki, halafu maeneo kutoka Pointe-Noire (leo: Jamhuri ya Kongo, upande wa kaskazini ya Cabinda) upande wa kaskazini hadi mto Loje (leo: mji wa Ambriz) katika kusini.

Mtawala alikuwa na cheo cha Manikongo na ufalme uligawiwa kwa majimbo sita. Baada ya kufika kwa Wareno wafalme na matabaka ya juu walikuwa Wakristo. Ufalme uliporomoka kutokana na vita vilivyosababishwa na biashara ya watumwa na kuingilia kwa wafanyabiashara ya watumwa katika siasa ya ndani. Hata hivyo, nasaba za watawala waliotumia cheo cha "Awenekongo" waliendelea kukaa katika mji mkuu wa kale M'banza-Kongo (iliyobadilishwa jina kuitwa San Salvador) hadi mwaka 1914 ambako Wareno walifuta mabaki ya uhuru na kufanya eneo lililobaki sehemu kamili ya koloni lao la Angola.

Upande wa kusini, kuanzia karne ya 17, kulikuwa na ufalme ulioitwa Dola la Kazembe.

Koloni binafsi la mfalme kuwa koloni la Ubelgiji hariri

 
Picha za watoto waliokatwa mikono kama adhabu chini ya Leopold II zilienea na kusababisha madai ya kumwondolea utawala wa Kongo.

Nchi jinsi ilivyo ilianzishwa kama Dola huru la Kongo likiwa mali binafsi ya mfalme Leopold II wa Ubelgiji. Historia yake ni ya aibu na ya ukatili kupindukia.

Utawala wa mfalme ulionekana kuwa wa kinyama na upinzani dhidi yake ulikua katika nchi nyingi za dunia.

Hatimaye alipaswa kukabidhi koloni lake binafsi mikononi mwa serikali ya Ubelgiji iliyomlipa fidia kwa mali aliyoacha.

Kati ya mwaka 1908 hadi 1960 ilikuwa koloni la Ubelgiji baada ya kuhamishiwa mikononi mwa serikali ya Ubelgiji.

Katika miaka 1925 hadi 1946 maeneo ya Rwanda na Burundi yalitawaliwa kama sehemu za Kongo ya Kibelgiji.

Siasa ya wakoloni hariri

Wabelgiji walijitahidi kuboresha hali ya maisha ya wenyeji baada ya miaka mibaya ya Leopold II. Nia ilichelewa kuonekana hali halisi kwa sababu utaratibu wa kulazimisha Waafrika kufanyia kazi kampuni na shirika kubwa iliendelea hata bila idhini ya serikali mpya ukadai vifo vingi.

Kwenye uwanja wa elimu, matibabu na mawasiliano jitihada za siasa mpya zilionekana zaidi. Kongo ilikuwa kati ya nchi chache ambako lugha za kienyeji zilifundishwa shuleni kwa sababu shule nyingi ziliendshwa na wamisionari.

Kwa upande mwingine ubaguzi wa rangi uliwaruhusu Waafrika wachache sana kufikia ngazi za juu za elimu.

Makampuni makubwa ya migodi kama vile "Société Générale" na "Union Minière du Haut Katanga" yalichimba madini hasa katika jimbo la Katanga. Makampuni haya yalikuwa na athira kubwa.

Katanga ilikuwa maarufu kwa shaba iliyochimbwa huko. halafu pia kwa uranium iliyotumiwa kwa mabomu ya kwanza ya kinyuklia ya Marekani mwaka 1945.

Upinzani hariri

Baada ya unyama wa miaka ya Leopold II upinzani dhidi ya utawala wa kikoloni ulikuwa hafifu. Kuanzia miaka ya 1920 Wakongo wengi walionyesha upinzani huo katika mahudhurio katika madhehebu mapya ya wafuasi wa Simon Kimbangu yaliyopigwa marufuku na Wabelgiji kuanzia mwaka 1926.

Tangu mwaka 1950 upinzani uliongezeka na kuonyesha pia uso wa kisiasa.

Wabelgiji ambao hawakujiandaa kwa madai hayo yalipaswa kukubali uchaguzi wa halmashauri za vijiji na miji mwaka 1957.

Mwaka 1958 vyama vya kisiasa vilikubaliwa. Harakati mbili muhimu kati ya hivi zilikuwa Abako (Alliance de Bakongo) chini ya Joseph Kasavubu na MNC (Mouvement National Congolais) chini ya Patrice Lumumba.

Mwaka 1959 mkutano wa wanasiasa Wakongo ulidai uhuru wa nchi.

Mwisho wa koloni na uhuru hariri

Wabelgiji walijaribu kuchelewesha harakati hizo lakini baada ya kutambua matatizo serikali ya Ubelgiji ilitangaza mnamo Januari 1960 kuwa uchaguzi utaendeshwa haraka na baada ya miezi sita Wabelgiji watakabidhi nchi kwa wenyeji.

Chama cha Patrice Lumumba kilishinda kwa kura nyingi naye akawa kiongozi wa kwanza wa nchi huru kama waziri mkuu.

Koloni la Kongo ya Kibelgiji lilipata uhuru tarehe 30 Juni 1960.

Kati ya 27 Oktoba 1971 na 17 Mei 1997, chini ya utawala wa dikteta Mobutu, nchi ilijulikana kwa jina la "Zaire".

Leo hii ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

  Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.