Abu Abdullah Muhammad Ibn Battuta (kwa Kiarabu: أبو عبد الله محمد بن بطوطة) alikuwa mpelelezi na mtaalamu Mwarabu wa karne ya 14. Kwa usafiri mgumu wa siku zile alitembelea nchi mbalimbali na kuvuka umbali mkubwa kushinda mtu yeyote wa siku zile anayejulikana. Kutoka kwake tunayo taarifa ya kwanza kuhusu mji wa Kilwa Kisiwani.

Maisha hariri

Alizaliwa tarehe 24 Februari 1304 mjini Tanger (Moroko).

Mwaka 1325 alihiji kwenda Makka na baada ya hajj hakurudi bali aliendelea kusafiri. Alitembelea karibu nchi zote zilizokaliwa na Waislamu. Kwa jumla alisafiri kwa miaka 30 akivuka umbali wa karibu km 120,000 (hii ni kama kuzunguka dunia yote mara tatu).

Habari zake zimepatikana katika taarifa yake aliyoiandika mwenyewe.

Katika safari yake ya kwanza alikwenda Makka kupitia Misri, Yerusalemu na Dameski. Baada ya kumaliza hajj akajiunga na msafara kwenda Baghdad akaona ufalme wa Khan wa Il na kutembelea Uajemi kabla ya kurudi Moroko.

Safari yake ya pili ilianza tena kama hajj na safari hii akaendelea kuangalia maeneo ya Bahari ya Shamu na pwani ya Afrika ya Mashariki. Akafika hadi Kilwa, kisha akarudi Makka kupitia Omani.

Baada ya kupumzika Makka alikata shauri kuona himaya ya Sultani wa Delhi (Uhindi).

Aliamua kujaribu njia kupita Uturuki kwa sababu alisikia ya kwamba palikuwa na misafara kati ya Waturuki Waseldjuki na Uhindi. Baada ya kuvuka Bahari Nyeusi alifika katika milki ya Kundi la Dhahabu akaendelea katika msafara wa Khan wa nchi. Alipofikia mji mkuu Astrakhan aliombwa na Khan wa Kundi la Dhahabu mwenyewe kumsindikiza mke wake aliyetaka kutembelea ndugu nyumbani kwake Konstantinopoli. Hivyo Ibn Battuta alifika kwa mara ya kwanza katika nchi nje ya zile za Kiislamu.

Mwishowe alifika Uhindi ambapo alipewa kazi ya qadi au hakimu.

Baada ya miaka kadhaa akatumwa kama balozi wa sultani kwenda China. Akisafiri kwa jahazi alipita nchi na visiwa vya Asia ya Kusini-Mashariki hadi China.

Kutoka hapa alirudi Moroko kupitia Makka.

Safari za baadaye zikampeleka hadi Afrika ya Magharibi alipotembelea ufalme wa Mali.

Ibn Battuta aliaga dunia mnamo 1377 huko Moroko.