Insha ya wasifu

Insha ya wasifu ni ile ya kutoa maelezo juu ya jinsi mtu au kitu kilivyo, tabia, vitendo na mandhari (sura ya mahali jinsi panavyoonekana).

Insha hizo zinaweza kuongelea kitu chochote kile, inaweza kuwa ni mnyama,mtu, shule, nchi n.k.

Mambo ya kuzingatia katika insha ya wasifu ni: sura, rangi, vipimo, tabia n.k.

Mfano wa insha ya wasifuEdit

SHULE YANGU Shule yangu inaitwa Shule ya Sekondari Shabaan Robert. Ni shule ya zamani iliyoanzishwa siku ya Ijumaa, tarehe 5 Agosti 1966 na Mheshimiwa Donna Matembele, aliyekuwa diwani wa kata ya Masuba.

Shule hii, ambayo ni maarufu sana, ipo katika Tarafa ya Mkunazini. Imejengwa katika uwanja wa hekta kumi na mbili. Ina madarasa kumi na mawili ya vidato vinne vya mikondo mitatu kila kimoja. Ina wanafunzi mia tano na wanne badala ya idadi halali ya wanafunzi mia nne themanini. Ni shule inayopendwa sana. Wanafunzi wa kike ni mia mbili na watatu na wa kiume ni mia tatu na mmoja. Walimu ni thelathini na mmoja. Jamii hii inapendana sana. Wanafunzi wana imani kubwa sana na walimu wao. Walimu huwahimiza wawe wanafanya bidii katika kazi na masomo kwa ujumla.

Wanafunzi hukadiria ugumu wa mazoezi wapewayo. Yale wayaonayo kuwa ni rahisi wao hujifanyia. Yale magumu kidogo hushughulikia kwa pamoja kwa kusaidiana wenyewe kwa wenyewe. Walimu hushirikishwa tu wakati wa mazoezi tata. Shule ya Sekondari ya Mwananchi ni ya kuvutia sana. Ina miti mingi sana ya matunda. Ina maua ya aina aina. Kutokana na nidhamu na uwajibikaji matunda hukomaa ndipo yatumiwe kwa mpango wakati wa chakula.

Heshima imethaminiwa mno na wanafunzi. Wanaheshimiana na kuwaheshimu walimu wao. Kwao heshima ni utiifu na uzingativu. Kutii na kuzingatia mambo waambiwayo na walimu ndicho kipimo cha heshima.

Katika shule yangu wanafunzi tuko kama paka. Paka hamtumi mtu nyama lakini atunukiwapo kipande hawezi kumruhusu yeyote kukigusa. Nasi tutunukiwapo nafasi yoyote ya kusoma hatumruhusu mtu yeyote kutupokonya nafasi hiyo.

Wanafunzi wa shule wana sare zao za kuvutia wazivaazo kiungwana kabisa. Sare hizo ni sweta ya bluu, shati au blauzi ya samawati, tai ya rangi ya damu ya mzee, suruali ndefu au sketi ya kijani kibichi, viatu vyeusi vya soli ndogo na visigino vifupi.

Katika shule yetu kuna uhusianao mwema baina ya walimu, wazazi, Chama cha Wazazi na Walimu (CHAWAWA) na Baraza la Shule. Kamati ya CHAWAWA na Baraza la Shule huanzisha miradi na kuitekeleza haraka kutokana na wazazi kuiunga mkono.

Kwa muda mrefu sasa matokeo ya mitihani yamekuwa ya kuridhisha kabisa. Na si hayo peke yake. Wanafunzi washirikipo katika michezo ya mpira, ya riadha na matamasha ya muziki takribani mara zote huibuka washindi.

Kwa ufupi shule yangu ni ya mafanikio mengi.

Mambo muhimu yaliyozingatiwa katika insha hii ya wasifuEdit

 • KICHWA (Shule yangu).
 • MAELEZO KAMILI yenye:
  • JINA la shule
  • HISTORIA ya shule
  • MAZINGIRA ya shule
  • IDADI ya wanafunzi na walimu
  • HALI ya wanafunzi
  • MAFANIKIO ya shule.
 • HITIMISHO lenye sifa ya jumla.
  Makala hii kuhusu mambo ya lugha bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Insha ya wasifu kama historia yake, uenezi au maendeleo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.