Laterano (kwa Kilatini Lateranus) ni mtaa wa Roma maarufu hasa kwa sababu kulikuwa na ikulu mojawapo la Kaisari Konstantino Mkuu.

Uso wa basilika ya Laterani

Baada ya yeye kuruhusu Ukristo katika Dola la Roma (Hati ya Milano, 313) ikulu liligeuzwa kuwa kanisa ambalo liliwekwa wakfu na Papa Melkiades (314), na mpaka leo linaheshimiwa na Kanisa Katoliki kama kanisa kuu la jimbo la Roma na la ulimwengu mzima.

Tofauti na wanavyodhani wengi, ukulu wa Papa ni katika kanisa hilo, si katika Basilika la Mt. Petro huko Vatikano.

Jina rasmi ni kanisa la Kristo Mkombozi, lakini watu wanaliita kwa kawaida kanisa la Mt. Yohane (Mbatizaji) kwa kuwa nyuma yake ipo batizio kuu, tena juu ya ukuta wake wa mbele kandokando ya sanamu ya marumaru ya Yesu, zipo zile za Yohane Mbatizaji na Mtume Yohane.

Ndani, juu ya altare kuu yanatunzwa mafuvu ya vichwa vya Mtume Petro na Mtume Paulo.

Ndani ya kanisa hilo mara tano ulifanyika mtaguso ambao kila mmoja unahesabiwa na Kanisa Katoliki kuwa Mtaguso Mkuu.

Mpaka uhamisho wa Avignon (karne ya 14) mapapa waliishi karibu na kanisa hilo, na mpaka leo seminari kuu ya jimbo (pamoja na chuo kikuu cha Kipapa cha Laterano) iko nyuma yake.

Eneo lote ni nje ya mamlaka ya nchi ya Italia na linahesabiwa kuwa sehemu ya nchi huru ya Vatikano.