Waiyaki wa Hinga : Tofauti kati ya masahihisho

Content deleted Content added
kuanzisha ukurasa
(Hakuna tofauti)

Pitio la 13:52, 17 Oktoba 2018

Waiyaki wa Hinga alikuwa mpiganaji na kiongozi wa Wakikuyu (mũthamaki) katika Kabete ya kale[1]. Aliongoza vita dhidi ya Wamasai na uasi dhidi ya wakoloni[2]. Alikufa mwaka 1982, akiwa mikononi mwa wakoloni.

Maisha

Hijulikani bayana mahali alipotoka au wakati alipozaliwa. Baadhi ya vizazi vyake husema kuwa alikuwa wa nasaba ya Wakikuyu ilhali baadhi ya wanahistoria wanaamini kuwa alikuwa Mmasai kutoka Ngong aliyekuwa amehama hadi Dagoretti kwa sababu ya maafa asilia[3]. Waiyaki alipewa jina Hinga, maana yake ikiwa mnafiki, kwa sababu hakuwa na uwazi na alikisiwa kuwa jasusi kutoka kwa Wamasai. Wamasai pia hawakumwamini kwa kuwa alikuwa ameongoza vita dhidi yao na kuteka ng'ombe wengi. Jina Waiyaki linaaminika kutokana na neno Koiyaki kutoka Kimaasai[4].

Alikuwa tajiri aliyekuwa ameoa wanawake kumi. Kama kiongozi, alikuwa kabaila mwenye ushawishi mkuu. Makazi pake palikuwa na vijumba tofauti, vya bibi zake na kimoja cha wageni. Hapo ndipo walipatana na Frederick Lugard Oktoba 10, Mwaka 1890[3][2].

Uasi na kifo

Lugard alikuwa na jukumu la kuhakikisha ushawishi wa Uingereza na usalama wa misafara ya wafanyabiashara katika Afrika ya Mashariki. Kwa sababu hiyo, alikuwa akitengeneza mikataba na makabila tofauti katika ziara ya kwenda Uganda. Kampuni aliyokuwa akifanyia kazi, IBEAC, ilikuwa ikiasisi ngome njiani[5]. Waiyaki alikubali ngome, ambayo pia ilikuwa kituo cha misafara ya Waingereza, ijengwe katika ardhi aliyoitoa. Lugard alijenga ngome, mahali ambapo Kanisa la P.C.E.A la Kihumo limejengwa[6][3]. Ili apatiwe shamba, Lugard alifanya mkataba na Waiyaki kwa njia ya uchale. Walikubaliana kwamba wazungu hawangenyakua ardhi au mali yoyote kutoka kwa Wakikuyu[2].

Mwezi mmoja baada ya Lugard kuendelea na safari yake, askari na wachukuzi walioachwa chini ya usimamizi wa George Wilson walianza kuvamia mashamba ya wenyeji na kuiba mazao ya shamba, mifugo na hata kuwanyanyasa wanawake[3][5]. Matukio hayo yaliwakasirisha sana wenyeji. Waiyaki aliongoza shambulizi katika ngome hiyo, mwaka 1891. Walipofika katika ngome, walipata kuwa George na wadogo wake walikuwa wametoroka kwa kuwa walikuwa wameonywa kuhusu shambulio hilo. Washambuliaji waliichoma ngome[5][3].

Mwaka 1892, msafara uliokuwa umeongozwa na Erick Smith ulitumwa Kabete. Smith alijenga ngome nyingine ambayo iliitwa Ngome ya Smith (ing: Fort Smith). Kulikuwa na vuta nikuvute kati ya wageni na wenyeji. Waingereza walikuwa wametumwa kulipiza kisasi kwa kushambulia kijiji cha Riuki, Githunguri. Waiyaki aliwaonya wanakijiji, na wakaweza kuondoka pamoja na mifugo yao kabla ya shambulizi kutendwa. Waingereza walichoma vijiji 30 na kuharibu mazao ya mashamba[1]. Waiyaki alipoenda kulalamikia Ngome ya Smith, alipatana na W. P. Purkis. Purkis alidai kuwa Waiyaki alikuwa amejaribu kumvamia kutumia kisu na kwa hivyo, Waiyaki akakamatwa[7]. Baada ya kuteswa, alipelekwa katika mahakama ya muda, iliyokuwa kando ya ngome[1]. Mahakama ilimpata kuwa na kosa na akahukumiwa kuhamishiwa Pwani.

Kuzikwa

Haijulikani bayana kilichomfanyikia alipokuwa katika msafara, ila tu hakuweza kuendelea na safari alipofika Kibwezi. Baadhi ya vyanzo husema kuwa msafara ulipofika Kibwezi, Waiyaki hangeweza kuendelea kwa kuwa alikuwa na majeraha mabaya kichwani[7]. Wengine husema kuwa alipigwa risasi. Rekodi rasmi zinaonyesha kuwa aliachwa katika hospitali ya misheni ambapo alifariki na akazikwa makaburini ya hospitali hiyo[5][1]. Vyanzo vingine husema kuwa alizikwa hai, Agosti 17, mwaka 1891[3][7][8].

Marejeo

  1. 1.0 1.1 1.2 1.3 122 years later, family seeks hero’s burial for Waiyaki wa Hinga (en). nation.co.ke. Iliwekwa mnamo 2018-10-17.
  2. 2.0 2.1 2.2 Jestice, Phyllis G. (2004). Holy People of the World: A Cross-cultural Encyclopedia (in English). ABC-CLIO. pp. 905–906. ISBN 9781576073551. 
  3. 3.0 3.1 3.2 3.3 3.4 3.5 Standard, The, "How legend was buried alive for resisting takeover", The Standard (in English), retrieved 2018-10-17 
  4. PressReader.com - Connecting People Through News. www.pressreader.com. Iliwekwa mnamo 2018-10-17.
  5. 5.0 5.1 5.2 5.3 Oldest edifice of colonial era left to rot in Kikuyu. www.businessdailyafrica.com. Iliwekwa mnamo 2018-10-17.
  6. Wanjohi Mutunga. How pioneers set the pace (PDF). The Torch bearer.
  7. 7.0 7.1 7.2 History and Government Form 2 (in English). East African Publishers. p. 53. ISBN 9789966253330. 
  8. Worger, William H.; Clark, Nancy L.; Alpers, Edward A. (2010). Africa and the West: From colonialism to independence, 1875 to the present (in English). Oxford University Press. p. 119. ISBN 9780195373134.