Kipindi cha Pasaka : Tofauti kati ya masahihisho

Content deleted Content added
Ukurasa ulianzishwa kwa kuandika '{{Mwaka wa liturujia}} Wayahudi wanaadhimisha Pasaka ya kale, ukumbusho wa kuvuka pakavu kati ya bahari, kutoka utumwani kuelekea uhuru....'
(Hakuna tofauti)

Pitio la 09:14, 8 Oktoba 2012

Wayahudi wanaadhimisha Pasaka ya kale, ukumbusho wa kuvuka pakavu kati ya bahari, kutoka utumwani kuelekea uhuru. Wakristo wanaadhimisha Pasaka mpya, ukumbusho wa sadaka ya Agano Jipya la milele ambayo pamoja na Yesu wanavuka toka dunia hii kwenda kwa Baba: Kristo asingefufuka imani hii ingekuwa bure.

Mwaka wa liturujia
Magharibi
Mashariki

Maelezo yafuatayo yanatokana na mpango wa Kanisa Katoliki, lakini kwa kiasi kikubwa yanafaa pia kwa madhehebu mengine, kama vile Anglikana.

Wakati wa Pasaka hatusomi Agano la Kale kwa kuwa yaliyotabiriwa nalo yameshatimia katika Kristo. Badala yake tunasoma karibu mfululizo Matendo ya Mitume yanayoelekeza safari yote ya Kanisa. Masomo mengine, sala na nyimbo vinasema hasa juu ya Kristo kufufuka na kuwa nasi na juu ya paji la Roho Mtakatifu alilotupatia.

Katika maisha ya kawaida watu wanafanya sherehe mbalimbali, si za dini tu. Sikukuu yoyote inatokeza furaha ya kuishi: usipokuwa na mtazamo wa kuridhika na maisha, kumwaga pesa katika anasa hakuondoi huzuni ya kukata tamaa. Sikukuu yoyote ni adhimisho la pamoja: inatokana na watu kukubaliana katika kujali mambo fulanifulani au walau kuheshimiana; pia inajenga jamii kwa kurudisha furaha ya kuwa pamoja.

Kwa Wakristo sherehe kuu kuliko zote ni Pasaka: ndiyo sikukuu yenyewe ambayo inadumu siku hamsini mfululizo hadi Pentekoste na inaitwa Dominika kubwa. Kwa kweli Pasaka si sherehe mojawapo tu wala kipindi kimojawapo tu katika mwaka wa liturujia, bali ndiyo kiini chake, kama vile Dominika (Pasaka ndogo ya kila wiki) ilivyo kiini cha juma zima. Ni adhimisho la uzima mpya na wa milele aliotushirikisha Kristo mfufuka kwa njia ya sakramenti: ubatizo na kipaimara kwa Wakristo wachanga, kitubio kwa waliobatizwa zamani, hasa ekaristi kwa wote; humo hatumkumbuki tu Yesu, bali tunakutana naye, hai tena mtukufu. Adhimisho hilo ni la pamoja kwa sababu tumekuwa moyo mmoja na roho moja katika Kristo kwa kumiminiwa Roho Mtakatifu. Kwa kumega mkate mmoja tunaimarisha ushirika wetu na kuwajibika kumtambua Yesu katika wale wote tunaokutana nao, hasa maskini.

Mang’amuzi hayo ya imani yanatuchochea kuimba mfululizo, Aleluya! Bila ya shaka tunaimba tukiwa njiani kuelekea kwetu: hatujafikia pale tutakapoimba katika heri ya starehe ya milele. Tunaimba tusije tukalemewa na mzigo wetu wa maisha. Augustino wa Hippo anatuonya: “Imba anavyofanya msafiri. Imba lakini tembea, usahau uchovu wako kwa kuimba, lakini jihadhari na uvivu. Imba na tembea”. Aleluya inatokeza vizuri furaha na tumaini letu: ndiyo sababu tunaikariri sana. Pamoja na hayo, uhuru wetu unatudai tuushuhudie kwa matendo na hasa kwa kuwakomboa ndugu zetu wanaodhulumiwa.

Kristo amefufuka kweli na atatufufua sisi pia: tutaishi naye kwa Baba katika umoja wa Roho Mtakatifu. Hata sasa yu pamoja nasi (ndiyo maana ya mshumaa wa Pasaka). Tukiwa naye maisha yanatunogea, kwa kuwa yote yameinuliwa tena na kufanywa mapya. Tumekombolewa kutoka utumwa wa dhambi na mauti, tumekuwa wana wa Mungu na kuishi kwa uhuru wa upendo tukiongozwa na Roho Mtakatifu. Kristo amekuwa Bwana na anaendelea kueneza ufalme wake. Hatuwezi kuogopa chochote tena kwa kuwa historia ni yake yeye aliye Alfa na Omega.

Viungo vya nje