Angakaskazi (anga ya kaskazini, kwa Kiingereza "northern sky") ni sehemu za anga zinazoonekana kwa mtazamaji kwenye nusutufe ya kaskazini ya Dunia yetu. Ufafanuzi wake ni "sehemu ya anga upande wa kaskazini wa ikweta ya anga".

Dunia jinsi inavyojizungusha angani.
(Picha hii ina kosa dogo, ikionyesha ikweta ya anga mno upande wa kaskazini)
Angakaskazi jinsi inavyoonekana kwa mtazamaji aliyeko kwenye ncha ya kaskazini.

Iko kinyume cha angakusi.

Angakaskazi, angakusi hariri

Kusudi la kugawa anga nusu mbili za kusini na kaskazini ni tofauti kati ya nyota zinazoonekana kwa mtazamaji akiwa kwenye upande wa kusini au upande wa kaskazini wa Dunia. Tofauti hii huwa kubwa zaidi kadri mtazamaji yupo karibu na ncha za Dunia. Tofauti inapungua kadri mtazamaji yuko karibu na ikweta.

Mtu anayeangalia nyota akiwa upande wa kaskazini wa ikweta ya Dunia hawezi kuona sehemu za nyota zote zinazoonekana vema upande wa kusini. Kwa hiyo watu wa Ulaya hawawezi kuona kamwe nyota za Salibu (Southern Cross) zilizopo si mbali na ncha-anga ya kusini. Kinyume chake watu wengi waliopo Ulaya au Marekani hawawezi kuona kamwe nyota mashuhuri ya Kutubu (Polaris)

Mtazamaji katika Afrika ya Mashariki yupo karibu na ikweta, kwa hiyo anaweza kuona nyota nyingi za sehemu mbili zote za anga. Hata hivyo Kutubu haionekani Tanzania (iliyopo upande wa kusini wa ikweta) ikiweza kutazamwa kaskazini mwa Kenya.

Tabia za angakaskazi hariri

Katika mazingira yasiyo na machafuko ya hewa (ukungu, vumbi) au machafuko ya nuru kuna takriban nyota 2000 zinazoonekana vema kwa macho matupu. Mjini penye mianga mingi idadi inapungua kuwa 500 - 100 pekee.

Nyota angavu zaidi ni Simaki (Arcturus) kwenye kundinyota la Bakari (Bootes) yenye uang'avu wa mag -0.05, ikifuatwa na Vega kwenye Shaliaki (Lyra) yenye mag +0,03 na Ayuki (Capella) kwenye Hudhi (Auriga) yenye mag +0.1.

Nyota ya Kutubu ipo kwenye nafasi ya anga-ncha ya kaskazini; kwa hiyo haibadiliki mahali pake angani ikionekana ya kwamba nyota zote zinaizunguka.

Makundinyota mashuhuri ya angakaskazi ni Dubu Mkubwa hasa sehemu yake inayoitwa "gari kubwa", halafu Mke wa Kurusi (Cassiopeia).

  Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Angakaskazi kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.