Ardhi adimu (pia: metali za ardhi adimu; kwa Kiingereza: rare earth elements, rare earth metals) ni jumla ya elementi 17 za kikemia zikiwa lanthanidi 15 pamoja na Skandi na Ytri. [2] Skandi na Ytri zinahesabiwa kati ya ardhi adimu ka sababu mara nyingi hupatikana katika amana za mbale zilezile pamoja na lanthanidi, pia zina tabia za kufanana.

Kutoka fungu la juu kwa kuiga mishale ya saa: praseodymium, cerium, lanthanum, neodymium, samarium, na gadolinium . [1]

Ardhi adimu zote ni metali.

Matumizi hariri

Ardhi adimu hazikujulikana zamani hivyo hazikuwa na matumizi. Tangu kutambuliwa kuna njia nyingi za kuzitumia katika teknolojia ya kisasa, hasa vifaa elektroniki kama kompyuta, simu za mkononi, vyombo vya tiba na silaha za kisasa. Tabia zake za kupitisha umeme zimeruhusu kuunda sumaku ndogo zenye nguvu, jambo lililowezesha kuunda vifaa vidogo kama kompyuta ndani ya simu zetu.

Kutokana na upanuzi wa vifaa vya elektroniki umuhimu wa ardhi adimu huongezeka. Kwa mfano Europi inahitajika kwa kuonyesha rangi nyekundu katika skrini za runinga na kompyuta. Neodimi ni lazima kwa sumaku ndogo za kudumu katika kompyuta, injini za umeme na jenereta za rafadha.

Uthabiti wake ni muhimu katika aloi za metali zinazowezesha kutengeneza injini zenye mwendo mkubwa.

Zinatumiwa katika betri za kuchajisha upya na hivyo mahitaji yake ni makubwa kutokana na upanuzi za magari ya umeme na simu za mkononi, lakini pia jitihada za kuhifadhi umeme jua na umeme upepo.

Upatikanaji hariri

Hata kama zinaitwa "ardhi adimu", hakuna uhaba wa elementi hizi duniani. Zilipokea jina la ardhi kwa sababu mwanzoni zilitambuliwa tu kwa umbo la oksidi ambazo kwa jumla zilitajwa pia kama "ardhi" katika miaka ya kwanza ya kemia ya kisasa. Zilitwa adimu au haba, kwa sababu ziliweza kutambuliwa mwanzoni kwa viwango vidogo tu, tena kwa matatizo. Seri, moja ya elementi hizo, ina nafasi ya 25 ukipanga elementi zote kufuatana na wingi wa akiba zake katika ganda la Dunia.

Lakini ardhi adimu hupatikana tu kwa hali ya mchanganyiko na elementi nyingine za aina hiyo, zinazofanana zote kikemia na kwa hiyo huhitaji jitihada kubwa za kuzitenganisha na kuzisafisha.

Siku hizi mzalishaji mkubwa duniani ni China iliyotoa asilimia 80 za mahitaji ya Dunia [3], ikifuatwa na Australia na 15% [4].

Serikali mbalimbali zimeona tatizo la kutegemea nchi 1 tu kwa malighafi muhimu kwa vifaa vya elektroniki, pia kulikuwa na hofu ya mahitaji kupita uzalishaji wa sasa, hivyo jitihada za kugundua akiba mbadala zilikaziwa[5].

Changamoto na hatari za kimazingira hariri

Njia ya kawaida ni matumizi ya asidi mbalimbali zinazoacha matope ya sumu kwa viumbehai. Michakato hiyo ni ghali na kama haisimamiwi ipasavyo inaweza pia kuleta hatari kwa mazingira na afya.

Mara nyingi ardhi adimu hupatikana pamoja na elementi nururifu kama urani na thori; mchakato wa kuzichimba ardhini, kuzisafisha na kukoleza unaongeza mnururisho katika mazingira ya shughuli hizo pamoja na hatari kwa afya ya wafanyakazi na watu walio jirani[6].

Nchini Kenya akiba kubwa ya Neodimi imetambuliwa katika Kilima cha Mrima.

Orodha ya ardhi adimu hariri

Jedwali linaorodhesha elementi 17 za ardhi adimu, namba atomia, ishara ya kikemia, asili ya majina yake, na mifano ya matumizi yake. Baadhi ya ardhi adimu zilipokea majina kutokana na wataalamu waliozigundua, na nyingine zilitajwa kwa kutegemea mahali zilipogunduliwa.

Z Alama Jina Asili ya jina Mifano ya matumizi
21 Sc Skandi kutoka Skandinavia, ambapo mtapo wake uligunduliwa mara ya kwanza Aloi nyepesi ya alumini-skandi inatumika kwa vijenzi vya eropleni. Pia ni nyongeza katika balbu za taa fulani. [7]
39 Y Ytri kufuatana na kijiji cha Ytterby, Uswidi, ambapo iligunduliwa. Yttrium hutumiwa katika leza fulani na runinga. Pia kwa kipitishi bora vya joto, na mikrowevu, na balbu zinazotumia nishati kidogo sana </ref>
57 La Lanthani kutoka kwa Kigiriki "lanthanein", ikimaanisha kufichwa. glasi za kipeo mchepuko, utunzaji wa hidrojeni, elektrodi za beteri, lenzi za kamera, vichocheo kwa mwatuko wa mafuta ya petroli.
58 Ce Ceri kufuatana na sayari kibete Ceres, iliyopewa jina la mungu wa Kiroma wa kilimo.

[dawa la kuoksidisha, unga wa kusafishia, rangi ya njano katika glasi na kauri, kichocheo cha kujisafishia oveni, vichocheo kwa mwatuko wa mafuta ya petroli.

59 Pr Praseodimi kutoka kwa Kigiriki "prasios" kijani , na "didymos" mapacha . sumaku za ardhi adimu, leza, inahitajika kwa taa za aki, rangi, nyongeza katika glasi miwani kwa kuchomelea vyuma
60 Nd Neodimi kutoka kwa Kigiriki "neos" mpya , na "didymos" mapacha . Sumaku za ardhi adimu, leza, rangi ya hudhurungi kwenye glasi na kauri, vijazi vya kauri
61 Pm Promethi kutoka kwa Prometheus wa mitholjia ya Kigiriki, ambaye alileta moto kwa wanadamu. beteri nyuklia
62 Sm Samari kutokana na Vasili Samarsky-Bykhovets, aliyegundua mtapo wake Sumaku za ardhi adimu, leza,
63 Eu Europi kutokana na bara la Ulaya (Europe), leza, taa za zebaki,
64 Gd Gadolini kutokana na Johan Gadolin (1760-1852), kuheshimu uchunguzi wake wa ardhi adimu. Sumaku za ardhi adimu, glasi za pekee, leza, machine za eksirei, kumbukumbu ya kompyuta, teknolojia ya neutroni , MRI
65 Tb Terbi kutokana na kijiji cha Ytterby, Uswidi. Fosifori kijani, leza, taa mulikaji
66 Dy Dysprosi kutoka kwa Kigiriki "dysprositos" kwa maana vigumu kupatikana . Sumaku za ardhi adimu, leza
67 Ho Holmi kutokana na Stockholm, mji muuwa Uswidi na mji wa asili wa mmoja wa wagunduzi wake. Leza
68 Er Erbi kutokana na kijiji cha Ytterby, Uswidi. Leza, feleji ya vanadi
69 Tm Thuli kutokana na nchi ya [Thule]] katika mitholojia ya Skandinavia. mashine za eksirei
70 Yb Ytterbi kutokana na kijiji cha Ytterby, Uswidi. leza za infraredi, wakala nakisishi katika kemia
71 Lu Luteti kutokana na Lutetia, jina la kale la Paris (Ufaransa). Vifaa vya tiba, glasi za kipeo mchepuko

Tanbihi hariri

  1. "News and events". US Department of Agriculture. Ilihifadhi kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2012-04-22. Iliwekwa mnamo 2012-03-13. 
  2. Connelly N.G. et al., mhariri (2005). Nomenclature of inorganic chemistry: IUPAC recommendations 2005. Cambridge: RSC Publ. ISBN 0-85404-438-8. Ilihifadhi kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2008-05-27. Iliwekwa mnamo 2012-03-13. 
  3. China's Rare Earth Dominance, Wikinvest. Retrieved on 11 Aug 2010.
  4. Gambogi, Joseph (January 2018). "Rare Earths". Mineral Commodity Summaries. U.S. Geological Survey. ku. 132–133. Iliwekwa mnamo 14 February 2018.  Check date values in: |date=, |accessdate= (help)
  5. "As hybrid cars gobble rare metals, shortage looms". Reuters. August 31, 2009. Retrieved Aug 31, 2009.
  6. Boom in Mining Rare Earths Poses Mounting Toxic Risks, tovuti ya yale.edu, iliangaliwa Novemba 2019
  7. C. R. Hammond, "Sehemu ya 4; Vipengele", katika CRC Handbook of Chemistry and Fizikia, 89th Edition (Internet Version 2009), David R. Lide, ed., CRC Press / Taylor na Francis, Boca Raton, FL.

Viungo vya Nje hariri

 
Wikimedia Commons ina media kuhusu: