Chama cha Kijani cha Ujerumani

Chama cha Kijani cha Ujerumani (Kiing. Green Party, jina rasmi la Kijerumani Bündnis 90/Die Grünen) ni chama cha kisiasa nchini Ujerumani. Mara nyingi huitwa tu "Wakijani" (Kiing. The Greens, Kijer. Die Grünen).

Nembo ya Chama cha Kijani cha Ujerumani

Kilianzishwa mwaka 1992 kwa maungano ya chama cha Ujerumani Magharibi Die Grünen na chama cha Ujerumani Mashariki Bündnis '90. Chama kinakazia hifadhi ya mazingira na ekolojia, haki za kiraia, usawa kati ya wanaume na wanawake na nafasi za wahamiaji katika jamii ya Ujerumani.

Historia hariri

Katika miaka ya 1970, kulikuwa na maandamano mengi dhidi ya upanuzi wa nishati ya nyuklia nchini Ujerumani. Waandamanaji hawakuwa na uungwaji mkono katika vyama vya siasa nchini Ujerumani hivyo wakapata wazo la kuunda chama chao[1].

Chama hicho kilianzishwa kwa jina la "Die Grünen" ("Wakijani", kwa maana ya wanaekolojia) huko Karlsruhe tarehe 13 Januari 1980.

Harakati hizo kwa haki za kiraia na ekolojia ziliungana na mwendo dhidi ya kuongezeka kwa silaha za nyuklia wakati wa vita baridi baina ya nchi za NATO na nchi za kikomunisti (Mapatano ya Warshawa). Greens walikuwa wapinzanivita wakapinga silaha za nyuklia. Walitaka kufikia Ulaya isiyo na jeshi. Baada ya muda mfupi baadhi ya watu wa mrengo wa kulia walihama chama, hivyo wakawa chama cha mrengo wa kati. Chama kina mirengo ya kati na kushoto.

Mnamo mwaka 1983 Wakijani walifaulu mara ya kwanza kupata asilimia 5 za kura katika uchaguzi mkuu wakaingia katika Bundestag wakarudishwa mwaka 1987 kwa 8,3%. Lakini baada ya muungano wa Kijerumani mwaka 1990 walishindwa kurudi bungeni.

Wakijani katika mashariki ya Ujerumani hariri

Mnamo 1990, wakati wa mwisho wa ukomunisti katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Ujerumani, vyama vipya viliundwa katika mashariki ya Ujerumani pamoja na Chama cha Kibichi na vyama vya kupigania haki za kiraia. Kwa ajili ya uchaguzi wa kwanza baada ya maungano ya Ujerumani viliungana pamoja kwa jina la "Bündnis 90" yaani "Maungano ya 1990".

Ilhali Chama cha kibichi cha magharibi ilishindwa kupata asilima 5 za kura na hivyo hakikuingia katika bunge, maungano ya mashariki yalipita 8% na kuingia bungeni.

Maungano ya vyama na kuingia serikalini hariri

Mara baada ya uchaguzi, vyama vya Kibichi vya mashariki na magharibi viliungana[2].

Mwaka 1994 chama kiliweza kurudi bungeni ambako kimeendelea kuwa na kundi la wabunge.

Mwaka 1998 kiliingia katika serikali ya ushirikiano na chama cha SPD chini ya chansela Gerhard Schröder. Wakijani walipata mawaziri watatu. Katika kipindi hicho waliona changamoto kutokana na vita ya Kosovo iliyotokea baada ya kuporomoka kwa Yugoslavia. Mawaziri wao walitaka jeshi la Ujerumani lijiunge na vikosi vya NATO vilivyotetea Kosovo dhidi ya Serbia ambayo ilikuwa kinyume cha upinzani-vita. Wanachama walianza kutoka kwenye chama, na kura zilipungua kwenye chaguzi za vieneo.

Lakini makubaliano ya kuondoka kwa Ujerumani katika nishati ya kinyuklia pamoja na kukataa kwa serikali ya kujiunga na Vita ya pili ya Ghuba dhidi ya Iraki yaliimarisha chama tena. Serikali haikuweza kuendelea baada ya uchaguzi wa mwaka 2005 kwa sababu ya kushuka kwa kura za SPD.

Upinzani kitaifa na serikali kijimbo hariri

Katika miaka iliyofuata Chama cha kijani kiliendelea kuwa upande wa upinzani katika bunge la shirikisho lakini kilingia katika serikali mbalimbali kwenye ngazi ya majimbo[3].

Mwaka 2011 kilifaulu kuwa chama kikubwa zaidi katika bunge la Baden-Württemberg na kushika nafasi ya waziri mkuu anayeongoza serikali ya jimbo katika ushirikiano na chama kidogo zaidi[4].

Serikalini tangu 2021 hariri

Mwaka 2021 chama kilifaulu pia katika uchaguzi mkuu na kuwa chama cha tatu kwenye Bundestag. Kikaingia katika serikali ya ushirikiano na SPD chini ya chansella Olaf Scholz na pamoja na chama cha liberali FDP[5].

Matokeo ya uchaguzi hariri

Yafuatayo ni matokeo ya Wakijani kwenye uchaguzi wa Bundestag, bunge la kitaifa.

Uchaguzi mkuu Kura kwenye majimbo ya uchaguzi Kura za chama kitaifa Wabunge
(Kijani/wabunge wote)
+/– Nafasi
Kura % Kura %
1980 732,619 1.0 (#5) 569,589 1.5 (#5) 0/497 (nje ya bunge)
1983 1,609,855 4.1 (#5) 2,167,431 5.6 (#5) 27/498   27 Upinzani
1987 2,649,459 7.0 (#4) 3,126,256 8.3 (#5) 42/497   15 Upinzani
1990[6] 2,589,912 5.6 (#5) 2,347,407 5.0 (#4) 8/662   36 Upinzani
1994 3,037,902 6.5 (#4) 3,424,315 7.3 (#4) 49/672   41 Upinzani
1998 2,448,162 5.0 (#4) 3,301,624 6.7 (#4) 47/669   2 Serikalini na SPD
2002 2,693,794 5.6 (#5) 4,108,314 8.6 (#4) 55/603   8 Serikalini na SPD
2005 2,538,913 5.4 (#5) 3,838,326 8.1 (#5) 51/614   4 Upinzani
2009 3,974,803 9.2 (#5) 4,641,197 10.7 (#5) 68/622   17 Upinzani
2013 3,177,269 7.3 (#5) 3,690,314 8.4 (#4) 63/630   5 Upinzani
2017 3,717,436 8.0 (#6) 4,157,564 8.9 (#6) 67/709   4 Upinzani
2021 6,465,502 14.0 (#3) 6,848,215 14.8 (#3) 118/735   51 Serikalini na SPD na FDP

Marejeo hariri

  1. Kaelberer, Matthias (September 1998). "Party competition, social movements and postmaterialist values: Exploring the rise of green parties in France and Germany". Contemporary Politics (in English) 4 (3): 299–315. ISSN 1356-9775. doi:10.1080/13569779808449970. 
  2. "Greens, E. German Leftists Join Election Forces". 
  3. Jungjohann, Arne (2017). German Greens in Coalition Governments. A Political Analysis. Heinrich-Böll-Stiftung European Union and Green European Foundation.
  4. Kulish, Nicholas. "Greens Gain in Germany, and the World Takes Notice", 2011-09-01. 
  5. Connolly, Kate. "German parties agree coalition deal to make Olaf Scholz chancellor", The Guardian, 24 November 2021. Retrieved on 24 November 2021. 
  6. uchaguzi wa 1990 ulihesabiwa katika magharibi na mashariki pekee; upande wa magharibi Wakijani walibaki chini ya 5%, uhivyo hawakuingiapande wa mashariki walifikia 8% wakapata wabunge

Viungo vya Nje hariri