Dahomey ilikuwa jina la jamhuri ya Benin hadi mwaka 1975 lakini hasa jina la ufalme wa Afrika ya Magharibi katika eneo la Benin ya kusini ya leo.

Mwanzo wa Ufalme wa Dahomey hariri

 
Askari wa kike wa Mfalme wa Dahomey ("Waamazoni").

Dahomey ilianzishwa na Waaja baada ya uhamisho wao kutoka Togo kuja Benin ya leo. Jina la Dahomey linasemekana kuwa limetokana na neno la Kifon la "dan" lenye maana ya "nyoka" - dokezo la ibada ya nyoka kusini mwa nchi.

Jina la mfalme wa kwanza ni Do Aklin aliyekuwa mmoja wa wana watatu wa mfalme wa Ardra waliogawanya ufalme kati yao mnamo 1625 BK. Do Aklin aliunda mji wa Abomey ukawa mji mkuu wa Dahomey.

Waaja wa Abomey walichanganyikana na wenyeji wakawa kabila jipya la Wafon au Wadahomey. Waliratibu ufalme wao kwa kuupa serikali ya mfalme mwenye nguvu, wakaunda jeshi la kudumu.

Hasa mfalme Wegbadja aliweka utaratibu kwa vizazi vilivyofuata: mfalme alikuwa mtawala mkuu, mkoani au majimboni hapana watawala wa kieneo bali watumishi wake tu.

Ardhi yote ilitazamwa kuwa mali ya mfalme mwenyewe, mafundisho yaliyohakikisha malipo ya kodi kutoka kwa wakulima waliokubali ya kwamba nchi waliyoilima ni mali ya mfalme.

Mamlaka ya mfalme yalihakikisha nguvu ya Dahomey katika mazingira yake. Jeshi la kudumu lilimpatia chombo muhimu. Ndani ya jeshi hilo kulikuwa na kikosi kimoja cha pekee ambacho kilikuwa kikosi cha wanawake.

Wasafiri wa Ulaya walikiita kikosi hiki "Waamazoni" kutokana na askari wa kike katika masimulizi ya Wagiriki wa Kale.

Wegbadja na wafuasi wake walikaza pia umuhimu wa ibada za pamoja. Wafalme wenyewe na mizimu yao walipewa nafasi muhimu. Sadaka zilienda na kila nafasi, hasa sadaka kwa mizimu ya wafalme.

Dahomey na biashara ya watumwa hariri

Ufalme uliongezeka nguvu ya kiuchumi kutokana na biashara ya watumwa. Kupaa kwa nguvu ya Dahomey kulikwenda sambamba na kuenea kwa wafanyabiashara Wazungu kwenye pwani za Afrika ya Magharibi walionunua watumwa kwa ajili ya safari ya Marekani, wakiuza silaha na bidhaa kutoka Ulaya.

Katika karne tatu za historia yake Dahomey ilikuwa kati ya wafanyabiashara wakuu wa watumwa. Jeshi la Dahomey lilikuwa na bunduki zilizonunuliwa kwa Wazungu wakiwauzia watumwa; silaha hizo zilitumika kwa ajili ya kupiga vita dhidi ya majirani na kujipatia wafungwa waliouzwa kama watumwa. Mapato kutoka biashara hiyo yaliwezesha wafalme wa Dahomey kununua silaha mpya.

Wafalme wa Dahomey hariri

  Makala hii kuhusu maeneo ya Afrika bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Dahomey kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.