Dalufnin (Delphinus kwa Kilatini na Kiingereza) [1]. ni jina la kundinyota ndogo ya angakaskazi.

Nyota za kundinyota Dalufnin (Delphinus) katika sehemu yao ya angani
Ramani la kundinyota Dalufnin - Delphinus (kwa macho ya mtazamaji kwenye nusutufe ya kaskazini ya Dunia)

Mahali pake

Dalufnin inapakana na makundinyota jirani ya Mbweha (Vulpecula), Sagita (Sagitta), Ukabu (Aquila), Dalu (Ndoo) (Aquarius), Mwanafarasi (Equuleus) na Farasi (Pegasus).

Jina

Dalufnin ilijulikana kwa jina hili kwa miaka mingi kati ya mabaharia Waswahili waliotumia nyota kutafuta njia baharini wakati wa usiku.[2]

Jina la Dalufnin linatokana na Kiarabu دلفين dulfiin ambalo ni umbo la jina asilia la Kigiriki δελφίς delfis (baadaye delphinus kwa tahajia ya Kilatini[3]) ambayo ni jina kwa nyangumi mdogo mwenye meno anayeitwa pomboo kwa Kiswahili.

Wagiriki wa Kale waliwatazama akina pomboo kama wasaidizi wa mabaharia[4] na viumbe watakatifu wa miungu kama Poseidon (mungu wa bahari). Imani hii ilileta hadithi mbalimbali katika mitholojia ya Kigiriki ambako pomboo walitekeleza shughuli kwa niaba ya miungu yao. [5]

Delphinus - Dalufnin ni kati ya makundinyota yaliyotajwa tayari na Klaudio Ptolemaio katika karne ya 2 BK. Iko pia katika orodha ya makundinyota 88 ya Umoja wa Kimataifa wa Astronomia kwa jina la Delphinus. Kifupi chake rasmi kufuatana na UKIA ni 'Del'. [6]

Nyota

Nyota za Dalufnin kwa jumla ni dhaifu; angavu zaidi ni Alfa, Beta, Gamma na Delta zinazofanya pembenne kama trapeza iliyoitwa pia „jeneza ya Ayubu“ [7]. Jina hili liliingia pia katika wimbo "Job's Coffin" wa mwimbaji Tory Amos.

Nyota za Alfa na Beta zina majina ya ajabu yaani Rotanev na Sualocin. Ukisoma majina haya kinyume unapata jina la "Nicolaus Venator" amabalo ni umbo la Kilatini la "Niccolò Cacciatore"[8] aliyekuwa msaidizi wa mwanaastronomia Mwitalia Guiseppe Piazzi[9].

Jina la
(Bayer)
Namba ya
Flamsteed
Jina
(Ukia)
Mwangaza
unaoonekana
Umbali
(miaka nuru)
Aina ya spektra
β 6 Rotanev 3,63m 80 F5 IV
α 9 Sualocin 3,77m 240 B9 IV
γ 12 3,9m K1 IV + F7 V
ε 2 Deneb Dulfim 4,03m 358 B6 III
δ 11 4,43m 223 F1 V

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Delphinus" katika lugha ya Kilatini ni " Delphini " na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Delphini, nk.
  2. ling. Knappert 1993
  3. Shina la δελφίς delfis ni δελφιν- delfin- jinsi inavyoonekana katika uhusika milikishi wake δελφινις delfinis na kutoka hapa umbo ndefu zaidi liliingia katika Kilatini
  4. Kuna hadithi nyingi kuhusu pomboo waliosaidia mabaharia walioanguka baharini na kuwabeba hadi mwambao, ling. Allen uk. 200
  5. ing. Allen, Star-Names and their Meanings, 199
  6. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Oktoba 2017
  7. Asili yake haijulikani, linganisha ling. Ridpath, Stars of Delphinus
  8. ling. Ian Ridpath, Stars of Delphinus
  9. Rotanev, tovuti ya Prof Jim Kaler, University of Illinois, iliangaliwa Oktoba 2017

Viungo vya Nje

Marejeo

  • Richard Hinckley Allen: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, “Delphinus” ukurasa 321 ff (online hapa kwenye archive.org)
  • Jan Knappert, 1993: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331