Dèng Xiǎopíng (22 Agosti 1904 – 19 Februari 1997) alikuwa mwanamapinduzi, mwanasiasa na mwanamageuzi muhimu wa China. Alikuwa kiongozi wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC).

Deng hakupata kamwe kuwa na cheo cha mkuu wa nchi au kiongozi wa serikali, lakini hali halisi alikuwa kiongozi mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China kutoka mwaka 1978 hadi miaka ya 1990. Anatazamwa kuwa kiongozi aliyeachana na ukomunisti mkali wa Mao Zedong na kuweka msingi kwa China kutoka kwenye umaskini kwa kuruhusu mali binafsi na uchumi wa soko huria.

Deng alizaliwa Guang'an, Sichuan. Alikufa kwa maambukizi na ugonjwa wa Parkinson huko Beijing, mwenye umri wa miaka 92.

Maisha ya mapema na familia hariri

Baba yake, Deng Wenming, alimiliki mashamba yaliyolimwa kwa msaada wa wafanyakazi. Mwenyewew aliwahi kusoma sheria alifundisha pia katika shule aliyoanzisha. Alitaka watoto wake waweze kusoma. Mama yake Deng alikufa mapema katika maisha yake. Deng alikuwa na kaka watatu na dada watatu. [1]

Mke wa kwanza wa Deng alikuwa mmoja wa wanafunzi wenzake kutoka Moscow. Alifariki akiwa na umri wa miaka 24 siku chache baada ya kujifungua mtoto wa kwanza wa Deng, ambaye alikuwa wa kike. Binti huyu naye alifariki. Mke wake wa pili alikuwa Jin Weiying. Jin alimwacha baada ya Deng kushambuliwa katika siasa 1933. Mkewe wa tatu Zhuo Lin alikuwa binti wa mfanyabiashara wa viwanda katika mkoa wa Yunnan. Alikuwa mwanachama wa Chama cha Kikomunisti mnamo 1938. Yeye na Deng walifunga ndoa mwaka wa 1939 mbele ya pango la nyumba ya Mao huko Yan'an. Walikuwa na watoto watano: mabinti watatu (Deng Lin, Deng Nan na Deng Rong) na wavulana wawili (Deng Pufang na Deng Zhifang).

Elimu hariri

Mwaka 1919 Deng Xiaoping alihitimu kutoka Shule ya Chongqing. Pamoja na wanafunzi wenzake 80 walipokewa katika mradi wa kusoma Ufaransa wakasafiri pamoja kwa meli. Walikuwa sehemu ya programu ya masomo na kazi iliyofadhiliwa. Deng alikuwa kijana kati ya wanafunzi wote wenzake kutoka China akiwa na umri wa miaka 15. [2] Baba ya Deng aliunga mkono sana mpango wa mwanawe kufanya kazi ya kusoma nje ya nchi. Deng alimwambia baba yake alitaka "kujifunza maarifa na ukweli kutoka Magharibi ili kuokoa China." Deng alijua kuwa Uchina inateseka. Alifikiri watu wa China lazima wawe na elimu ya kisasa ili kuokoa nchi yao. [3]

Muda mfupi baada ya kufika, taasisi iliyofadhili masomo ya Deng ilifilisika. Deng alijikuta bila msaada wowote alipaswa kutafuta kazi na kukubali shughuli za duni kabisa kwa malipo madogo. Wanafunzi hao kutoka China walitoka kwenye familia za wenye hela lakini hapa walijikuta sasa kwenye ngazi ya chini kabisa. Walishikamana kati yao wakajiunga na harakati ya kisiasa na baadaye chama cha kikomunisti. Kule Ufaransa Deng alikutana na watu wangi walioendelea baadaye kuwa viongozi China: Zhou Enlai, Nie Rongzhen, Cai Hesen, Zhao Shiyan na Li Wenhai. Deng aliendelea kuwa mmoja wa viongozi wa umoja wa vijana wa chama hicho katika Ulaya.

Mnamo 1926, Deng alisafiri kwenda Umoja wa Kisovyeti akasoma kwenye Chuo Kikuu cha Sun Yat-sen mjini Moscow. Mmoja wa wanafunzi wenzake alikuwa Chiang Ching-kuo, mwana wa Chiang Kai-shek . [4]

Kurudi China hariri

Mnamo Machi 1927, Deng alisafiri kutoka Moscow hadi Xi'an kwenye kaskazini-magharibi mwa China.

Wakati ule, wakomunisti Warusi waliunga mkono wa ushirikiano wa Wakomunisti Wachina na Mwelekeo wa kizalendo wa Kuomintang. Deng alitumwa kumsaidia mmoja wa majemadari wazalendo akifundisha katika chuo cha kijeshi. Lakini mwaka huohuo ushirikiano wa wazalendo na wakomunisti ukavunjika na Wakomunisti wote walipaswa kuondoka.

Vyanzo vya ukomunisti hariri

Deng alikwenda Wuhan alipopata ajira kwenye ofisi ya chama cha kikomunisti. Hapa alikutana tena na Zhou Enlai aliyemfahamu kutoka Ufaransa na pia mara ya kwanza na Mao Dzedong.

Kwenye Oktoba 1927 ofisi ilihamishwa Shanghai na Deng aliendelea kufanya kazi ya kiofisi. Wakati huo alianza kupanda ngazi ndani ya chama akifahamika na kuheshimiwa na wengi. Hapa alioa mara ya kwanza, mke wake alikuwa Zhang Xiyuan aliyemfahamu kutoka wakati wake huko Moscow.

Mnamo 1929 Deng aliongoza Maasi ya Baise katika jimbo la Guangxi dhidi ya serikali ya Kuomintang (KMT). Maasi hayo yalishindwa, na Deng akaenda eneo la Sovieti ya Kati katika jimbo la Jiangxi.

Kazi ya kisiasa hariri

Deng alienda kwenye Long March na Mao. Wakati wa Uvamizi wa Kijapani wa Uchina, alijiunga na Jeshi la Njia ya Nane lililoongozwa na Liu Bocheng . Baada ya Vita Kuu ya II alikuwa sehemu ya mazungumzo ya amani kati ya Wakomunisti na Kuomintang. Mazungumzo haya yameshindwa. Tarehe 1 Oktoba 1949, Deng alikuwa katika kutangaza Jamhuri ya Watu wa China huko Beijing. Deng alikua meya wa Chongqing na alikaa huko hadi 1952. Kuanzia 1952 hadi mwanzoni mwa miaka ya 1960 Deng alikuwa na nyadhifa nyingi za nguvu serikalini huko Beijing. Lakini, akawa mlengwa wa mikondo miwili ya kisiasa: Mapinduzi ya Kitamaduni na Kampeni ya Kumkosoa Deng mnamo 1976. Deng alisema kuwa Mapinduzi ya Utamaduni yalikuwa mabaya kwa China mwaka 1977 na kuanza "Beijing Spring." China ilianza kufungua zaidi mwaka 1978-79. Deng alifanya kazi kurekebisha uchumi wa China na kuongeza mauzo ya nje katika miaka ya 1980. Maandamano ya Tiananmen Square mwaka 1989 yalimdhoofisha. Alistaafu siasa mwaka 1992.

Nukuu maarufu hariri

  1. ⎡ 不管黑猫白猫,能捉老鼠就是好猫。⎦ Usijali kama ni paka mweusi au paka mweupe; muda mrefu kama ni uwezo wa kukamata panya, ni paka nzuri.
  2. ⎡ 摸着石頭過河。⎦Tafsiri: Ili kuvuka mto wenye kina kifupi, ni lazima mtu afuate mawe chini ya maji.
  3. ⎡小朋友不聴话,該打打屁股了。⎦ Tafsiri: Ni wakati wa kupiga chini kabisa watoto wadogo wasiotii. (Alipomjulisha rais Jimmy Carter wakati wa ziara yake nchini Marekani, kwamba China ilikuwa tayari kuingia vitani na Vietnam . )

Marejeo hariri

  1. Deng Xiaoping – Childhood. China.org.cn. Iliwekwa mnamo 14 May 2010.
  2. Spence 1999, 310
  3. Stewart, Whitney, Deng Xiaoping: Leader in a Changing China, 2001
  4. Exiled son who saved the state. Times Higher Education (22 March 2002). Iliwekwa mnamo 2 December 2010.

Viungo vya nje hariri