Etimolojia (kutoka gir. ἐτυμολογία etimología, kupitia ing. etymology) ni elimu ya maana ya maneno na asili zao.

Maneno pamoja na matamshi na tahajia hubadilika polepole. Yanaweza kuunganishwa au kufupishwa. Maneno huhamia kutoka lugha moja hadi nyingine na hapo yanaweza kubadilisha maana. Maneno mapya yanabuniwa kwa vitu vipya visivyojulikana awali.

Kiswahili ni lugha ya Kibantu na hapo asili ya maneno mengi inaweza kutambuliwa kwa kulinganisha lugha mbalimbali ya Kibantu. Lakini Kiswahili ni pia lugha iliyopokea maneno mengi kutoka nje, hasa kutoka Kiarabu, baadaye kutoka Kireno na lugha za Kihindi na siku hizi kutoka Kiingereza. Ilhali lugha hizi zimepokea pia maneno kutoka asili nyingine wakati mwingine historia ya neno ni kama safari katika historia ya kibinadamu.

Mifano kadhaa hariri

  • "Etimolojia" imefika katika Kiswahili kutoka Kiingereza etymology lakini kiasili ni neno la Kigiriki cha Kale lililoundwa kuotokana maneno ya ἔτυμον etimon ("maana ya kweli") na -λογία -logia ("somo la..", "elimu kuhusu"). Neno hili la Kigiriki lilipokelewa katika Kilatini ambacho baadaye kilikuwa lugha ya elimu katika Ulaya ya MAgharibi wa karne nyingi na hivyo kuingia katika lugha nyingi za Ulaya.[1]
  • Kitabu ina asili ya Kiarabu ( كتاب, kitabun); inaonekana ni wafanyabiashara Waislamu waliotumia lugha ya Kiarabu waliopeleka kitu hiki katika mazingira yasiokuwa na maandishi kwa hiyo neno la kigeni likapokelewa moja kwa moja kwa kitu kigeni.
  • Samaki pia ni neno lenye asili ya Kiarabu (سمك samakun); bila shaka wenyeji wa Uswahilini walikuwa na neno la Kibantu kwa samaki na hapa kuna swali kwa nini waliaacha neno lao la kiasili kwa neno la nje; kuna hoja ya kwamba kule pwani samaki zilikuwa vyakula vilivyouzwa na wenyeji kwa wageni waliofika kwa jahazi na hivyo waliona faida wakitumia lugha ya wateja.
  • Muhindi kama jina la nafaka linatunza uhusiano na Uhindi ingawa uwzekano mkubwa ni imefika Afrika kutoka Amerika kupitia Wareno na Wahispania. Katika lugha za Ulaya mara nyingi iliitwa "nafaka ya Uhindi" (ing. Indian corn, far. ble de Inde) kwa sababu Kolumbus aliamini ya kwamba alifika Uhindini ya Asia na Wahispania pamoja na Wareno waliita nchi walizotawala katika Amerika "India" kwa karne zilizofuata. Hata hivyo kuna uwezekano ya kwamba nafaka hii ilifika pia kutoka Bara Hindi moja kwa moja kwa sababu kuna uwezekano ya kwamba ilijulikana pale kabla ya Kolumbus [2][3]. Inawezekana pia ya kwamba wenyeji wa pwani walitunga jina hilikwa kudokeza ni nafaka kutoka sehemu za mbali.[4][5]
  • Maneno kama Tanzania, UKIMWI au BAKITA yametungwa juzijuzi tu kwa unganisha sillabi ya majina mengine: TANganyika na ZANzibar kuwa Tanzania, Uhaba wa KInga MWIlini kuwa Ukimwi, BAraza ya KIswahili TAnzania kuwa Bakita.

Kamusi hariri

Kwa lugha nyingi kuna kamusi za pekee zinazoonyesha etimolojia ya maneno. Kati ya Kamusi za Kiswahili hadi sasa hakuna kamusi ya etimolojia hasa.

  • Kamusi ya Kiswahili Sanifu ya TUKI inadokeza kwa kifupi lugha asilia kama neno la Kiswahili lina asili kwa lugha ya nje.
  • Standard Swahili-English Dictionary ya Madan-Johnson inataja asili ya maneno kwa kirefu zaidi kiasi
  • Kamusi ya Kiswahili - Kifaransa iliyotolewa na Charles Sacleux mwaka 1939 hadi sasa ina maelezo bora na pana ya etimolojia ya maneno ya Kiswahili - lakini inatoa maana kwa Kifaransa tu.[6]

Marejeo hariri

  1. Malkiel, Yakov (1993). Etymology. Cambridge University Press. p. 223. ISBN 9780521311663. 
  2. Picha za zao linaloonekana kama mahindi zimegunduliwa pia kwenye uchongaji wa picha za ukutani katika hekalu za Uhindi ya zamani kabla ya Kolumbus hivyo kuna imani kati ya wachunguzi kadhaa kuwa muhindi imefika Bara Hindi kupitia Bahari ya Pasifiki ingawa historia hii haijulikani bado,linganisha makala ya "Maize in Pre-Columbian India" inayounwa hapa (tovuti ya Chuo Kikuu cha Ohio State. Jalada kutoka ya awali juu ya 2015-09-27. Iliwekwa mnamo 2015-06-21.
  3. Vivyo hivyo makala hii kwenye tovuti ya M. Kumar and J. K. S. Sachan kwenye tovuti ya Rajendra Agricultural University [1] Archived 30 Aprili 2011 at the Wayback Machine.
  4. Kuna mifano ya etimolojia ya aina hii kwa muhindi katika nchi za Ulaya: katika Ujerumani ya Kusini, Austria na Slovenia muhindi iliitwa "nafaka ya Kituruki" ("türk" au "Türkisch Weizen") ingawa haitokei kule, lakini jina limetokea kwa kutaja asili ya nchi ya mbali.
  5. Carl L. Johanessen, Maize diffused to India before Columbus came to America, Tovuti ya University of Oregon. Jalada kutoka ya awali juu ya 2016-03-07. Iliwekwa mnamo 2015-06-21.
  6. Inapatikana katika intaneti kwa upakuzi kwenye kwenye tovuti ya Chuo Kikuu cha Leipzig: Kamusi ya Sacleur[dead link]

Viungo vya Nje hariri

Kujisomea hariri