Historia ya Afrika Kusini

Historia ya Afrika Kusini inahusu eneo la Kusini mwa Afrika ambalo wakazi wake leo wanaunda Jamhuri ya Afrika Kusini.

Historia ya kale hariri

Zamadamu waliishi katika eneo la Afrika Kusini tangu miaka milioni 3 iliyopita, inavyoshuhudiwa na akiolojia.

Binadamu wameishi huko kwa miaka 170,000 mfululizo.

Wakazi wa muda mrefu zaidi ni Wakhoikhoi na Wasani, ambao wote wanagumzumza lugha za jamii ya Khoi-San.

Katika karne ya 4 au ya 5 walifika Wabantu ambao waliwazidi nguvu hao wa kwanza.

Koloni la Waholanzi kwenye Rasi hariri

Chanzo cha Afrika Kusini kama nchi ni Koloni la Rasi iliyoundwa na Waholanzi katika eneo la Cape Town kuanzia mwaka 1652. Huko kabila jipya la Makaburu lilijitokeza kati ya walowezi Wazungu kutoka Uholanzi, Ufaransa na Ujerumani. Lugha yao ilikuwa Kiholanzi iliyoanza kuchukua maneno ya Kifaransa, Kiafrika na Kiingereza na kuendelea kuwa lugha ya pekee Kiafrikaans.

Karne za kwanza za koloni la Kiholanzi ziliona pia kufika kwa watumwa kutoka Indonesia walioletwa kama wafanyakazi wa Waholanzi na Makaburu. Hao Waindonesia walikuwa chanzo cha jumuiya ya Uislamu kwenye rasi.

Pia machotara walitokea kutokana na kuzaliana kati ya Makaburu na wanawake Waafrika na Waindonesia. Sehemu ya machotara hao wameingia katika jumuiya ya Makaburu na wengi wao wanapimwa kuwa na mababu Waafrika.

Katika miaka ya baadaye ubaguzi wa rangi uliongezeka na watoto machotara wa Wazungu na Waafrika mara nyingi hawakukubalika; walianza kuishi kama kundi la pekee kati ya Waafrika na Wazungu, nao ni chanzo cha hao walioitwa baadaye "Cape Coloreds".

Milki za Waafrika na Mfecane hariri

Sehemu kubwa ya eneo kaskazini kwa rasi ilikaliwa na makabila ya Waafrika.

Mnamo mwaka 1800 falme na milki zilianza kutokea hapa. Mwanzo wa karne ya 19 ni hasa Wazulu chini ya Shaka Zulu walioanza kuenea na kuwashambulia majirani katika vita vya Mfecane. Vita hivyo vilileta uharibifu mkubwa lakini vilisababisha pia kutokea kwa milki za Wasotho na Watswana na wengine walioiga mitindo ya Wazulu na kujenga madola yenye uwezo wa kijeshi.

Kuingia kwa Uingereza na jamhuri za Makaburu hariri

Mwaka 1814 Koloni la Rasi lilitwaliwa na Waingereza na kuwa sehemu ya Milki ya Uingereza.

Utawala wa Waingereza ulisababisha uhamisho wa nje wa sehemu ya Makaburu waliotokana na Wazungu kutoka Uholanzi, Ufaransa na Ujerumani; Makaburu hao walihama kwenda kaskazini wakaanzisha jamhuri ndogo kati ya maeneo ya Waafrika ama kwa njia ya mapatano au kwa njia ya vita.

Kati ya miaka 1840 na 1850 Waingereza waliwafuata Makaburu kwa kueneza maeneo yao hadi mto Oranje; waliteka jamhuri ya Kikaburu ya Natalia na kuanzisha koloni jipya la Natal.

Jamhuri mbili za Makaburu ziliweza kustawi kwa miaka kadhaa ambazo zilikuwa jamhuri ya Dola Huru la Oranje upande wa kaskazini wa mto Oranje na jamhuri ya Transvaal (ilijiita pia Jamhuri ya Kiafrika ya Kusini) upande wa kaskazini wa mto Vaal.

Waafrika, Waingereza na Makaburu waligongana hariri

Milki za Kiafrika zilitafuta njia zao kati ya himaya hizi za Wazungu ambao walikuwa na nguvu kutokana na silaha za kisasa. Wengine walitafuta uhusiano mzuri na Makaburu na kushikamana nao; wengine waliona Makaburu kama hatari wakatafuta uhusiano wa ulinzi na Waingereza.

Mikataba kati ya Waingereza na milki za Kiafrika iliunda nchi lindwa zinazoendelea hadi leo kama nchi huru kama vile Botswana (Bechuanaland), Lesotho (Basutoland) na Eswatini (Swaziland).

Katika miaka ya 1880 almasi na dhahabu zilipatikana kwa wingi katika jamhuri hizi na kusababisha kufika kwa wachimbamadini wengi, hasa Waingereza, waliotaka kutajirika; Makaburu walisita kuwapa haki za kiraia kwa sababu waliogopa wageni wengi. Tatizo hilo lilisababisha vita vya Makaburu dhidi ya Uingereza na jamhuri za Makaburu zilitwaliwa na jeshi la Kiingereza hadi mwaka 1902 zikawa makoloni.

Karne ya 20: Muungano wa Afrika Kusini hariri

Jitihada za kupatanisha Wazungu wa Afrika Kusini (yaani Waingereza na Makaburu) zilisababisha kuundwa kwa Muungano wa Afrika Kusini kama nchi ya kujitawala ndani ya Milki ya Uingereza. Waafrika kwa jumla hawakuwa na haki za kiraia katika nchi hiyo isipokuwa katika Jimbo la Rasi kama walikuwa na elimu na mapato ya kulipa kodi za kutosha.

Siasa ya Apartheid tangu 1948 hariri

Baada ya vita kuu ya pili ya dunia Chama cha National kilichofuata itikadi kali ilipata kura nyingi na kuchukua serikali ya Afrika Kusini. Hapo ilianzisha mfumo wa ubaguzi wa rangi kwa jina la apartheid.

Haki za wasio Wazungu zilipunguzwa zaidi. Maeneo ya Kiafrika yalitangazwa kuwa nchi za pekee chini ya usimamizi wa serikali ya Kizungu ya Afrika Kusini; kwa hiyo wananchi kutoka maeneo hayo hawakuwa tena na haki za kukata rufaa mbele ya mahakama; walipewa vibali vya muda tu kukaa kwenye miji. Waafrika walipaswa kutembea muda wote na pasipoti na vibali; ndoa na mapenzi kati ya watu wa rangi tofauti zilipigwa marufuku. Shule na makazi zilitenganishwa.

Siasa hiyo ilisababisha farakano kati ya nchi nyingi za dunia na Afrika Kusini. Upinzani kutoka Uingereza na Jumuiya ya Madola ulisababisha kuondoka kwa Afrika Kusini katika jumuiya hiyo na kutangazwa kwa Jamhuri ya Afrika Kusini.

Afrika Kusini mpya hariri

Mwaka 1990 Apartheid ilikwisha na serikali ya National Party ilipaswa kuendesha uchaguzi huru kwa wananchi wote na kukabidhi madaraka kwa serikali ya ANC chini ya Nelson Mandela.

  Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Afrika Kusini kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.