Historia ya Uganda

Historia ya Uganda inahusu eneo la Afrika Mashariki ambalo wakazi wake leo wanaunda Jamhuri ya Uganda.

Historia ya kale hariri

Wakazi wa kwanza huaminiwa kuwa wawindaji wa jamii ya Wasani.

Katika karne za kwanza BK walifika wahamiaji Wabantu wenye ujuzi wa kilimo na uhunzi. Kutoka kaskazini walifika Waniloti kwa mfano Waluo na baadaye Karimojong.

Tangu karne ya 15 himaya mbalimbali zilianza kujengwa na kati ya hizo ni hasa falme za Buganda, Ankole, Bunyoro Toro zilizoendelea kuwa muhimu hadi kuja kwa ukoloni na kwa kiasi fulani kama urithi wa kiutamaduni hata katika Uganda ya kisasa.

Ukoloni hariri

Karne ya 19 iliona kufika kwanza kwa Waarabu na baadaye kwa Wazungu. Katika mashindano juu ya Afrika ya Kati Waingereza walifaulu katika kushindana na Waarabu, Wafaransa na Wajerumani. Walienea kwa mapatano na Buganda wakisaidiana kukomesha upinzani kutoka falme za jirani.

Ni kwamba kila mkoloni alileta dini yake yaani Uislamu na Ukristo wa Kikatoliki na wa Kianglikana.

Wamisionari Wakatoliki kutoka Ufaransa na Waanglikana kutoka Uingereza walishindana na Waislamu kwenye ikulu ya Kabaka Mutesa I wa Buganda (18561884) kati yao na dhidi ya wafuasi wa dini za jadi. Mashindano hayo yalisababisha kutokea kwa vyama mbalimbali vilivyoleta nchi katika hali ya vurugu.

Mnamo 1890 Mjerumani Karl Peters alifaulu kupata mkataba wa ushirikiano na Kabaka lakini serikali za Ujerumani na Uingereza zilipatana katika mkataba wa Helgoland-Zanzibar nchi iwe eneo la athari ya Uingereza. Mwakilishi Mwingereza Frederick Lugard aliingilia kijeshi kati ya mapigano ya vikundi ndani ya Buganda na kuhakikisha utawala wa Kabaka Mwanga aliyehesabiwa kuwa upande wa Waanglikana, hivyo karibu na Uingereza.

Baadaye Waingereza walikuwa na nguvu ya kutosha kuamua hata mambo ya ndani ya Buganda wakatangaza Uganda wote kuwa nchi lindwa tangu mwaka 1894. Mwaka huo Kabaka alikubali mkataba wa ushirikiano na Uingereza ambao machoni mwake ulikuwa mapatano ya hiari lakini hali halisi Buganda ikawa nchi ya kulindwa chini ya Uingereza.

Polepole utawala wa Kiingereza ilibadilisha hali ya Buganda hadi kuwa sehemu tu ya Uganda yote.

Wakati wa uhuru Waganda walishindwa kupata hali ya ufalme kuwa sehemu ya nchi inayojitawala lakini Kabaka Sir Edward Mutesa II alikuwa Rais wa Taifa pamoja na waziri mkuu Milton Obote.

Mwaka 1967 Obote alibadilisha katiba akamfukuza Kabaka nchini. Kwa muda wa miaka 30 ufalme wa Buganda ulifutwa kisheria. Kabaka Edward Mutesa II alikufa ng'ambo Uingereza.

Mwaka 1986 serikali mpya ya Yoweri Museveni ilimkaribisha Ronald Muwenda Mutebi, mtoto wa Kabaka marehemu, arudi Kampala. Baada ya Bunge la Uganda kurudisha falme za kihistoria ndani ya Uganda za Banyoro, Ankole na Toro pamoja na Buganda, Mutebi alifanywa Kabaka mpya mwaka 1993.

Baada ya uhuru hariri

Uganda ilipata uhuru wake tarehe 9 Oktoba 1962 kwa katiba ya jamhuri yenye serikali ya kibunge.

Rais wa kwanza alikuwa Kabaka Sir Edward Mutesa II na waziri mkuu Milton Obote.

Mwaka 1967 Obote alibadilisha katiba akamfukuza Kabaka nchini.

Serikali ya Obote ilipinduliwa na mkuu wa jeshi Idi Amini mwaka 1971. Utawala wake ulikuwa kipindi cha udikteta ulioharibu uchumi wa nchi na misingi ya dola. Takriban watu 300,000 waliuawa chini ya Amin ama wapinzani wa siasa yake ama watu wa makabila yaliyotazamwa kuwa maadui wa serikali. Raia wenye asili ya Asia walifukuzwa katika nchi na mali yao yote kutwaliwa na serikali.

Mwaka 1978 vikosi vya jeshi la Uganda viliingia Tanzania na kuvamia maeneo ya mpakani kaskazini kwa mto Kagera. Mwaka 1979 Tanzania ilijibu kwa njia ya vita na jeshi lake pamoja na wapinzani wa Uganda walishinda jeshi la Amin na kumfukuza dikteta nchini. Rais wa baadaye Yoweri Museveni alikuwako kati ya wanamgambo waliosaidiana na Watanzania.

Uchaguzi wa mwaka 1980 ulimrudisha madarakani Milton Obote aliyeanzisha upya udikteta na kuua watu ovyo. Wapinzani wake wakiongozwa na Museveni walirudi porini wakashika silaha. Katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kundi la Museveni likashinda na kutwaa serikali tangu mwaka 1986.

Museveni alichaguliwa rais katika kura bila vyama vya upinzani za 1996 na 2001.

Mwaka 2005 ulikuwa na uchaguzi wa vyama vingi wa kwanza. Museveni alipata kibali cha bunge kwa badiliko la katiba lililomruhusu kugombea urais tena mwaka 2006 akachaguliwa mara ya tatu.

Tanbihi hariri

Marejeo hariri

Marejeo mengine hariri

  Makala hii kuhusu mambo ya kihistoria bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Historia ya Uganda kama enzi zake au matokeo yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.