Mialekundu

(Elekezwa kutoka Infraredi)

Mialekundu[1] (pia: infraredi, inforedi) ni aina ya nuru isiyoonekana kwa macho ya kibinadamu lakini kuna wanyama wanaoweza kuiona. Inasikika kama joto. Kifizikia ni aina ya mnururisho sumakuumeme mwenye mawimbi marefu kuliko nuru ambayo inaonekana kwa binadamu na mawimbi ambayo ni mafupi kuliko mawimbi mikro.

Kwa kutumia kamera na filamu za pekee zinazoshika mialekundu inawezekana kupiga picha ya watu hata gizani

Historia ya utambuzi

Mialekundu ilitambuliwa mara ya kwanza na mwanaastronomia Friedrich Wilhelm Herschel aliyefanya utafiti wa nuru ya Jua. Alipitisha nuru ya Jua kwenye prisma akapata spektra ya nuru hii. Alianza kupima halijoto za rangi mbalimbali za spektra. Hapo aliona akiweka themomita nje ya sehemu nyekundu ya spektra joto lilipanda tena. [2][3] Hivyo alitambua ya kwamba spektra ya nuru inaendelea nje ya sehemu aliyoweza kuona kwa macho yake.

 
Samaki hii ya aina Pelvicachromis taeniatus inatambua mialekundu kwa macho yake
 
Popo ya Desmodus ananyonya damu ya mamalia anaopata gizani kwa kutambua joto la mwili

Wanyama wenye uwezo wa kuona mialekundu

Kuna wanyama mbalimbali wenye uwezo wa kuona mialekundu. Nyoka mbalimbali huwa na milango ya fahamu ya pekee inayowawezesha kutambua tofauti za halijoto katika mazingira yao hivyo kutambua windo la karibu hata gizani.

Kuna pia popo ya Desmodus rotundus hujo Amerika Kusini mwenye mlango wa fahamu wa kutambua windo lake.

Kua pia aina za wadudu wenye milango fahamu za pekee kwa kutofautisha joto.

Kwa wanyama wachache imeonekana ya kwamba wanatumia macho kwa kazi hiyo, kwa mfano samaki za Afrika ya Magharibi aina ya Pelvicachromis taeniatus.

Binadamu hutambua joto kupitia neva za pekee kwenye ngozi laini haziwezi kutofautisha sehemu ja joto tofautitofauti isipokuwa kwa karibu sana.

Mitambo inayotumia mialekundu

Kuna njia ya kufanya picha za mialekundu kwa kutumia kamera, filamu na mitambo ya pekee.

Kamera zinaweza kutumia vichujio kali viinavyozuia nuru ya kawaida isiingie ndani, na pamoja na filamu za pekee zinaweza kushika picha kama ile ya wasichana hapo juu kwenye ukurasa huu.

Ilhali picha hizi zinaweza kupigwa hata penye giza kabisa kunamatumizi mengi katika teknolojia ya usalama na upelelezi kwa picha za aina hii.

 
Mwanajeshi anayetumia mtambo wa kuona gizani anaotazama kwa jicho moja

Siku hizi kuna kamera kwa ajili ya kompyuta zinazopima mawimbi ya mialekundu. Teknolojia hii ina matumizi makubwa kwa ajili matumizi ya jeshi na polisi.

Askari wanatumia mitambo midogo inayowawezesha kuona kwenye usiku. Mtu huwa na halijoto tofauti na mazingira yake hivyo anaonekana pia katika giza. Injini za motokaa kama ni joto inaonekana sana gizani kwa mialekundu hata kama injini ilizimishwa.

Makombora ya kisasa ya kupiga ndege hutumia "jicho la mialekundu" kwa kulenga kwa injini ya ndege nyingine. Hapo ndege za kijeshi wanatumia mabomu madogo yanayolipuka nje ya ndege yenyewe kwa kusudi la kuipa kombora mahali pa joto kali zaidi itakapolenga badala ya ndege yenyewe.

Marejeo

  1. https://webb.nasa.gov/content/features/keyFactsInternational/postcards/postcard_swahili.pdf
  2. "Herschel discovers Infrared light". Ilihifadhi kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2012-02-25. Iliwekwa mnamo 2015-04-05. 
  3. "William Herschel and the discovery of infrared light". Ilihifadhi kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2015-03-27. Iliwekwa mnamo 2015-04-05. 

Tovuti za Nje