Khorezmia (pia: Chorasmia) ni eneo la kihistoria upande wa kusini wa Ziwa Aral. Kiini chake ni oasisi kubwa kwenye delta ya mto Amu Darya unapoingia Ziwa Aral. Upande wa mashariki kuna jangwa la Kyzylkum na upande wa magharibi nyanda za juu za Ustyurt. Leo hii eneo limegawiwa kati ya nchi za Uzbekistan, Kazakhstan na Turkmenistan.

Eneo la Khorezmia leo.

Wakazi wake walikuwa watu wenye lugha karibu na Kiajemi lakini tangu zama za Kati makabila ya Kituruki yaliingia huko hadi Kiajemi kilipotea.

Historia hariri

Katika historia tangu karne ya 6 KK Khorezmia ilikuwa kitovu wa falme mbalimbali. Ni pamoja pa mahali panapotajwa kama sehemu ambako dini ya Uzoroasta ilianzishwa. Msingi wa nguvu yake ilikuwa maji ya mto katika mazingira ya jangwa, rutuba ya ardhi na kilimo cha umwagiliaji.

Tangu mfalme Koreshi Mkuu ilitawaliwa kama jimbo la Uajemi lakini iliweza kurudisha uhuru wake. Tangu uvamizi wa Waarabu mwaka 712 ilikuwa chini ya utawala wa Kiislamu na polepole watu wake walipata kuwa Waislamu. Uvamizi wa Wamongolia ulileta uharibifu mwingi.

Tangu karne ya 16 Khorezmia ilipata tena kitovu cha kisiasa katika Dola la Khiva lililoendelea hadi mwaka 1920 ilipoingizwa katika Umoja wa Kisovyeti.