MESSENGER (kifupi cha "MErcury Surface, Space ENvironment, GEochemistry and Ranging", yaani "uso, maziringa ya anga, jiokemia na upimaji rada za Utaridi") ilikuwa kipimaanga kutoka nchini Marekani chenye kazi ya kuzunguka sayari Utaridi na kukusanya data juu yake.[1] Kiliingia katika obiti ya sayari hii tarehe 18 Machi 2011 kikaendelea kutekeleza kazi zake hadi kuanguka kwenye uso wa sayari tarehe 30 Aprili 2015.[2]

Uchoraji wa MESSENGER juu ya sayari Utaridi
Njia ya MESSENGER kuelekea Utaridi

MESSENGER ilipelekwa angani tarehe 3 Agosti 2004[1][3] kutoka Cape Canaveral.

Njia ya chombo cha angani haikuelekea moja kwa moja kwenda Utaridi kwa sababu hii ingehitaji fueli nyingi mno. Kwa hiyo MESSENGER ilizunguka Jua na sayari mbalimbali mara kadhaa hadi kufikia umbali na Utaridi ambako ilishikwa na graviti ya sayari katika njia imara.

Kwa ujumla MESSENGER ilielea kilomita bilioni 8 hadi kufikia njia yake ya kuzunguka sayari ya Utaridi. Kwa kusudi la kupunguza matumizi ya fueli chombo kilipita karibu kwenye sayari za Dunia (2 Agosti 2005) na Zuhura (5 Juni 2007) hadi kukaribia Utaridi mara ya kwanza 14 Januari 2008. Halafu ilipita Utaridi mara tatu kwenye njia ambako graviti ya sayari inachelewesha mwendo wa chombo cha angani yaani mpito wa "swing-by".

Tarehe 18 Machi 2011 MESSENGER iliifikia njia imara ya kuzunguka Utaridi. Baadaye ilipangwa kuzunguka sayari yake kwenye kimo cha kilomita 200 hadi 15,000 kwa muda wa mwaka moja. Mwaka 2015 ilianguka kwa uso wa Utaridi baada ya kuishia fueli yake.

Marejeo

  1. 1.0 1.1 How it Works (Imagine Publishing) (23), 2011-07-14: 48-49  Missing or empty |title= (help)
  2. Messenger’s Collision Course With Mercury, NASA’s Messenger spacecraft crashed into Mercury on Thursday, taarifa ya New York Times April 30, 2015, tovuti iliangaliwa Mei 2018
  3. "Launch Coverage: MESSENGER Mission". NASA. Ilihifadhi kwenye nyaraka kutoka chanzo mnamo 2011-08-04. Iliwekwa mnamo 2011-07-30.