Mahekalu ya Abu Simbel

Mahekalu ya Abu Simbel ni mahekalu mawili makubwa yaliyojengwa zamani za Misri ya Kale. Yanapatikana upande wa magharibi wa Ziwa Nasser katika Nubia, Misri ya Kusini.

Mahekalu ya Abu Simbel baada ya uhamisho

Ni maarufu kutokana na uzuri wake na pia kwa sababu yalihamishwa mwaka 1968 kutoka mahali pa awali kando ya mto Nile kwenda mahali pa juu kilimani kwa sababu ya kujaza kwa Ziwa Nasser nyuma ya lambo la Aswan kwa shabaha ya kuyatunza kutoka maji ya ziwa jipya.

Masanamu ya Ramse kwenye hekalu la Abu Simbel yaliyohamishwa kwasababu ya mafuriko mnamo mwaka 1967.

Pamoja na mahekalu mengine ya Nubia yameingizwa katika orodha ya urithi wa dunia ya UNESCO.[1]

Ujenzi hariri

 
Hekalu dogo, sanamu za farao na malkia pamoja na mwandishi wa hiroglifi

Mahekalu yalijengwa wakati wa utawala wa Farao Ramses II katika karne ya 13 KK. Mfalme huyo aliagiza ujenzi baada ya ushindi wake katika mapigano ya Kadesh kama kumbukumbu kwa ajili yake mwenyewe na malkia yake Nefertari.

Ujenzi ulianza mnamo mwaka 1264 KK ukaendelea takriban kwa miaka 20. Jina la jengo kuu lilikuwa "Hekalu la Ramses mpendwa wa mungu Amun". Kusudi la kujenga kwenye mpaka wa kusini wa milki ilikuwa kuwaonyesha majirani ukubwa na nguvu ya farao. Ilisaidia pia kusambaza dini ya Misri katika maeneo ya kusini.

Mahekalu yalijengwa kwenye mtelemko mkali wa mwamba. Ukumbi ulikatwa kama pango ndani ya mwamba. Uso wa nje ulipambwa kwa sanamu zilizochongwa kutoka mwamba wenyewe. Hekalu kubwa lilijengwa kwa heshima ya miungu Ra-Harakhty, Ptah na Amun. Ina sanamu nne kubwa za Ramses II. Hekalu dogo lilikuwa kwa heshima ya mungu wa kike Hathor aliyechongwa kwa uso wa malkia Nefertari.

Upotevu na kutambuliwa upya hariri

 
Ukumbi wa hekalu kubwa wenye nguzo 8 zilizochongwa kwa kumwonyesha mungu Osiris

Katika mwendo wa karne nyingi dini ya Misri ilibadilika na mahekalu hayakutumiwa tena. Mnamo karne ya 6 BK mchanga wa jangwa lilishafunika sanamu usoni mwa hekalu hadi magoti. Baadaye hapakuwa na taarifa tena, na mahekalu yalisahauliwa.

Mwaka 1813 Mswisi Jean-Louis Burckhardt aliona sehemu za mawe ya paa zilizotokeza juu ya mchanga. Alimwambia Mwitalia Giovanni Belzoni juu ya mahali, lakini huyu akichimba alishindwa kukuta geti la kuingia.

Mwaka 1817 alirudi akachimba upya akaweza kuingia ndani. Mnamo mwaka 1825 Mwingereza Edward William Lane alichora picha na kuiweka katika kitabu chake cha mwongozo wa Misri.

Jina la Abu Simbel linasemekana lilikuwa jina la kijana mwenyeji aliyewaongoza hao wapelelezi Wazungu hadi mahali pa hekalu.

Uhamisho hariri

 
Vipande vya sanamu za Ramses ziliunganishwa mahali mpya

Tangu mwaka 1960 lambo la Aswan lilianza kujengwa na kuzuia mwendo wa mto Nile. Ilionekana ya kwamba maji ya Ziwa Nasser yalielekea kufunika mahekalu. Wataalamu kutoka nchi nyingi walianza kukusanya pesa kwa uhamisho wa majengo.

Kazi iliyogharamia dola za Marekani milioni 40 ilianza mwaka 1964 iliyotekelezwa na kundi la kimataifa ya wanaakiolojia na wahandisi chini ya usimamizi wa UNESCO. Mwamba ya mahekalu ulikatwa katika vipande vikubwa vya tani 20-30 vilivyopelekwa mahali pa juu na kuunganishwa tena mita 65 za juu na mita 200 kutoka maji.[2]

Leo hii kuna mamia ya watalii wanaotembelea mahekalu kila siku kwa meli au kwa ndege wakitumia kiwanja cha ndege kilichojengwa.

Picha hariri

Tazama pia hariri

Marejeo hariri

  1. Nubian Monuments from Abu Simbel to Philae - UNESCO World Heritage Centre
  2. The race to save Abu Simbel is won, Spencer, Terence (1966). The Race to Save Abu Simbel Is Won. Life magazine, December 2, 1966. Ilitazamiwa Januari 2017

Tovuti za nje hariri

 
Wikimedia Commons ina media kuhusu: