Malta

jimbo kuu la Kusini mwa Ulaya lililo kwenye visiwa katika Bahari ya Mediterania

Malta ni nchi ndogo kwenye funguvisiwa katikati ya bahari ya Mediteranea.

Malta
Ramani ya Malta
Malta kutoka angani

Malta iko km 93 kusini kwa kisiwa cha Sisilia (Italia), upande wa mashariki kwa Tunisia na kaskazini kwa Libya.

Jiografia hariri

Funguvisiwa la Malta lina visiwa saba. Visiwa vikubwa viwili ni Malta (km² 246) na Gozo (km² 70). Kuna kisiwa cha tatu kinachokaliwa na watu, ndicho Comino (km² 3). Vingine ni vidogo, havina watu. Jumla la eneo ni km² 316.

Visiwa vya Malta ni mabaki ya kanda la nchi kavu lililokuwa linaunganisha Afrika na Ulaya na lililokatwa na kupanda kwa usawa wa bahari tangu mwaka 11000 KK hivi.

 
Pwani ya Mellieħa Bay.

Sehemu za juu ni vilima vya Dingli Cliffs vyenye kimo cha mita 245 juu ya UB.

Tatizo kubwa la Malta ni uhaba wa maji baridi. Siku hizi vituo vinne vya kuondoa chumvi kwenye maji ya bahari kwa njia ya osmosi vinatengeneza maji ya kunywa. Maji machafu husafishwa na mvua kukusanywa.

Miji hariri

 
Valletta.

Miji mikubwa zaidi ni: St. Paul's Bay (29,097), Birkirkara (wakazi 21,676), Qormi (wakazi 18,230), Mosta (wakazi 17,789), Zabbar (wakazi 15,030), Victoria (wakazi 12,914) na San Gwann (wakazi 12,346).

Mji mkuu, Valletta, una wakazi 7,173 tu.

Historia hariri

Malta ilikaliwa na watu tangu milenia ya 4 KK. Kuna magofu ya hekalu la mwaka 3200 KK hivi.

Baadaye funguvisiwa lilitawaliwa na Wafinisia, Karthago na Dola la Roma.

Malta inatajwa katika Biblia kwa sababu Mtume Paulo aliponea huko baada ya kuzama kwa merikebu alimosafiri baharini kuelekea Roma (Mdo 27:39 n.k.).

Waarabu walivamia visiwa hivyo mwaka 870 na kuvitawala hadi 1091.

Baadaye vilitawaliwa na Wanormandi wa Italia Kusini, halafu na Wahispania chini ya mamlaka ya Dola Takatifu la Kiroma la Ujerumani.

Tangu mwaka 1530 visiwa vilikabidhiwa na Kaisari kwa askari wa Vita vya msalaba wa Chama cha Wanahospitali wa Mt. Yohane wa Yerusalemu.

Wanamisalaba hao walitawala visiwa hivyo hadi Napoleoni alipoteka Malta mwaka 1799 akiwa safarini kwenda Misri.

Uingereza ulitwaa visiwa kutoka kwa Ufaransa ukatawala Malta hadi uhuru wake tarehe 21 Septemba 1964.

Tarehe 13 Desemba 1974 Malta ikatangazwa kuwa jamhuri ndani ya Jumuiya ya Madola.

Tarehe 1 Mei 2004 nchi ikajiunga na Umoja wa Ulaya.

Watu hariri

Kwa jumla kuna wakazi 404,039: wa kiume 200,715 (49.7%) na wa kike 203,324 (50.3%). Msongamano wa watu ni 1,282 kwa kilomita ya mraba ambao ni msongamano mkubwa kati ya nchi zote za Ulaya. Katika karne ya 21 nchi imepokwa wahamiaji wengi, ambao kwa sasa ni 23.17% za wakazi wote.

Lugha ya Kimalta ni lugha ya pekee. Asili yake ni lahaja ya Kiarabu iliyopokea maneno mengi ya Kiitalia, Kisisili, Kiingereza, Kihispania na Kifaransa. Ni lugha pekee ya Kisemiti inayoandikwa rasmi kwa alfabeti ya Kilatini.

Lugha rasmi ya pili ni Kiingereza kutokana na miaka 150 ya ukoloni wa Uingereza. Wamalta wengi sana (66%) huelewa pia lugha ya nchi kubwa jirani, Italia.

wakazi wengi (90%) ni Wakristo, hasa wa Kanisa Katoliki (83%), ambalo imani yake ndiyo dini rasmi ya nchi. Waislamu ni asilimia 2.

Tazama pia hariri

Tanbihi hariri

Marejeo hariri

Viungo vya nje hariri

 
WikiMedia Commons
Wikimedia Commons ina media kuhusu:


Serikali
Taarifa za jumla
Vyombo vya habari
Safari


Nchi za Umoja wa Ulaya  
Austria | Bulgaria | Eire | Estonia | Hispania | Hungaria | Italia | Kroatia | Kupro | Latvia | Lituanya | Luxemburg | Malta | Polandi | Slovakia | Slovenia | Romania | Ubelgiji | Ucheki | Udeni | Ufaransa | Ufini | Ugiriki | Uholanzi | Ujerumani | Ureno | Uswidi
  Makala hii kuhusu maeneo ya Ulaya bado ni mbegu.
Je unajua kitu kuhusu Malta kama historia yake, biashara, taasisi zilizopo, watu au utamaduni?
Labda unaona habari katika wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.