Mashauri ya Kiinjili

Mashauri ya Kiinjili ni maelekezo ambayo yanapatikana katika Injili lakini hayamlazimishi mfuasi wa Yesu kuyafuata.

Fransisko wa Asizi akijinyima mali yote: mfano wake ulivuta wengi kufuata mashauri ya Kiinjili, hasa ufukara wa hiari.

Yanategemea maisha na mafundisho yake kadiri ya Agano Jipya.

Yanatolewa kwa hiari ya mtu atakayevutiwa nayo moyoni mwake kutokana na Roho Mtakatifu kumjalia karama ya namna hiyo.

Maarufu zaidi ni yale matatu ambayo ni kiini cha maisha ya utawa hasa katika Kanisa Katoliki: useja mtakatifu, ufukara na utiifu (ufafanuzi wake kwa mashirika yote unatolewa katika Mkusanyo wa Sheria za Kanisa la Kilatini, kanuni 599–601).

Mashauri ya Kiinjili katika maisha ya Kiroho hariri

Wakristo wote wanapaswa kulenga upendo kamili; kutokana na amri kuu, huo ni wajibu wa kila mmoja kadiri ya hali yake maishani. Lakini hawawezi kuufikia wakiishi duniani kana kwamba ndiyo maskani ya milele, pasipo roho ya mashauri ya Kiinjili, ambayo ni kutoambatana na malimwengu. Kutokana na wito wa pekee, baadhi wana wajibu maalumu wa kulenga ukamilifu kufuatana na nadhiri za kutekeleza mashauri ya ufukara, useja na utiifu[1][2].

Mashauri ya Kiinjili na madonda ya roho hariri

Yesu alipomualika tajiri akauze vyote ili kumfuata katika ukamilifu, “yule kijana alipolisikia neno lile, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi” (Math 19:22). Kutekeleza kwa vitendo mashauri ya Kiinjili si wajibu wala si sharti la kufikia ukamilifu tunaopaswa kuulenga, ila ni njia inayofaa kulifikia lengo hilo kwa hakika na kasi zaidi. Katika huyo aliyeshindwa tunaona ni vigumu kuwa na roho ya kutoambatana na malimwengu tusipoitekeleza kwa vitendo. Anayeishi ulimwenguni yuko katika hatari ya kuzamia mahangaiko ya kujipatia nafasi nzuri au kuwatafutia ndugu zake, hata akasahau kwamba anapaswa kuelekea mbinguni, na kwamba ili aifikie anahitaji si akili kuhusu shughuli za kidunia, bali msaada wa Mungu (ambao ajiombee) na tunda la neema (yaani stahili). Katika maisha ya kifamilia anaelekea kukwama katika mafungamano yanayomtimizia haja ya mapendo, hata akasahau wajibu wa kumpenda Mungu kuliko wote; mara nyingi upendo wake si mwali hai unaomuinukia Mungu ukihuisha mapendo mengine yote, bali ni kama kaa dogo linalozidi kuzimika chini ya majivu: ndiyo sababu anaweza akatenda dhambi kwa urahisi, asifikirie anasaliti urafiki na Mungu. Hatimaye yuko katika hatari ya kufuata matakwa yake na, baada ya sala fupi, kupanga maisha yake upande wa maumbile tu, akiathiriwa na umimi, mawazo ya kibinadamu na madai ya mazingira. Hapo anahangaikia masuala ya kidunia na pengine michezo, halafu yakitokea matatizo makubwa yanayohitaji nguvu nyingi za Kiroho anakuja kutambua imani yake ni haba mno: kwake kweli kuu za imani hazina nguvu kiutendaji, ziko mbali angani zisiingie rohoni mwake. Anakosa imani yenye vitendo inayoleta nuru ya mafumbo ya wokovu katika maisha ya kila siku.

Ndizo hatari zinazomkabili Mkristo asipozingatia mashauri ya Kiinjili kadiri anavyoweza. Akiteleza kwenye mteremko huo, anapotea na kuzidiwa na mambo matatu yanayopingana moja kwa moja na hayo mashauri matatu: “Kila kilichomo duniani, yaani tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia” (1Yoh 2:16). Hayo ni madondandugu matatu yanayoziathiri roho na kuziua kwa kuzisogeza mbali na Mungu. Madonda hayo yameenea ulimwenguni kufuatana na dhambi ya mtu wa kwanza pamoja na dhambi zetu tulizozirudiarudia. Ili tuelewe ubaya wake tunapaswa kukumbuka hayo yameshika nafasi ya ule ulinganifu uliokuwepo katika hali ya uadilifu asili pande zote tatu.

Mtu alipoumbwa kulikuwa na ulinganifu kamili kati ya Mungu na roho, kati ya roho na mwili, tena kati ya mwili na vitu vya nje. Kulikuwa na ulinganifu kati ya Mungu na roho, kwa sababu roho imeumbwa ili kumjua, kumpenda na kumtumikia, na hivyo kupata uzima wa milele. Mtu wa kwanza, aliyeumbwa katika utakatifu na uadilifu, alikuwa mwanasala mwenye kuongea kirafiki na Mungu akijilisha hasa mambo ya Kimungu, akizingatia yote katika mwanga huo na kumtii. Kutokana na ulinganifu huo wa juu kulikuwa na ule kati ya roho na mwili, ulioumbwa ili utumikie roho. Roho ikiwa chini ya Mungu kikamilifu iliutawala mwili wake, huku maono na maelekeo ya hisi yakifuata kwa makini uongozi wa akili (yenye busara na imani) na msukumo wa utashi (uliohuishwa na upendo). Hatimaye kulikuwa na ulinganifu kati ya mwili na vitu vya nje, dunia ikizaa yenyewe pasipo haja ya kuilima kwa jasho la uso; vilevile wanyama walikuwa wakimtii mtu aliyepewa kuwatawala, au walau hawakumdhuru.

Dhambi ilivuruga ulinganifu huo wote ikiangamiza ule wa juu: mtu aliasi sheria ya Mungu, na tangu hapo roho yake inaelekea kiburi na kukariri, “Sitatii”. Imeacha kujilisha ukweli wa Kimungu ijitungie mawazo finyu, danganyifu, geugeu, na kujiongoza kwa kuiwekea mipaka mamlaka ya Mungu, badala ya kufuata maongozi yake ambayo tu yanafikishia uzima. Kwa kumkaidi Mungu, roho imepoteza utawala wake juu ya mwili na juu ya maono yake yaliyokusudiwa kutii akili na utashi. Tena mara nyingi imejifanya mtumwa wa mwili na hamu zake za kinyama: ndizo tamaa za mwili. Watu wasio na idadi wanasahau lengo lao la Kimungu na kushughulikia kutwa kucha mwili wao kama mungu wao. Maono yanaitawala roho hata isipotaka, kwa kuwa ndani yake pendo, wivu, hasira na chuki vinajitokeza vikipambana na kuipeleka huko na huko kama farasi wasiokubali lijamu wala hatamu. Hatimaye mwili, badala ya kufaidika na vitu vya nje, umekuwa mtumwa wa vitu hivyo: unajichosha ili kuvipata kwa wingi, unajizungushia fahari ya bure kwa hasara ya maskini wenye njaa, unajiona anahitaji vile vyote vinavyong’aa na kuthaminika: ndizo tamaa za macho. Kisha kujilimbikizia vitu, hangaiko la kuvidumisha na kuvizidisha tena linakuwa wazo kuu la umati wa watu ambao, kama watumwa wa shughuli hizo, hawana kamwe muda wa kusali na kusoma Injili ili kujilisha rohoni; wanajijenga duniani kana kwamba wataishi hapa milele yote, wasiwazie wokovu wao. Utumwa huo wa pande tatu ni kinyume cha utaratibu. Mwokozi alikuja kuurudisha ulinganifu wa asili pande zote tatu, na kwa ajili hiyo ametupatia mashauri matatu.

Mashauri ya Kiinjili na kurudia ulinganifu wa asili hariri

Yesu katika utu wake ndiye kielelezo cha maadili yote, mfano bora wa utakatifu. Kutokana na umoja wake na Nafsi ya Neno, aliwekwa wakfu kwa Mungu tangu achukuliwe mimba; alipokea utakatifu wa kuzaliwa nao, usioumbwa. Haiwezekani kuwaza muungano na Mungu ulio wa ndani na wa kudumu kuliko huo unaounganisha utu na umungu katika Nafsi ya Neno aliyefanyika mwili. Kutokana nao utu wa Mwokozi umewekwa wakfu pamoja na vipawa vyake vyote na matendo yake yote, hata akili yake isiweze kudanganyika, utashi wake usiweze kufanya kosa na hisi zake safi zisiweze kuvurugwa na lolote. Matendo yake yote ni ya Mungu, yanatokana na Mungu na kumuelekea Mungu; utawala wa Aliye Juu hauwezi kutimia kikamilifu hivyo popote pengine. Kwa kuwa utu wa Yesu umewekwa wakfu namna hiyo bora, ukuu wake umemtenga na roho ya ulimwengu na yale yote yaliyo maovu au yasiyo mema tu, naye akatolewa kwa ulimwengu ili kuukomboa kutoka upofu wa tamaa na kiburi.

Kwa ukuu huo wa asili, Yesu alitenganika na mali, heshima, shughuli za kidunia: kielelezo cha ufukara, hakuwa na mahali “pa kujilaza kichwa chake” (Lk 9:58). Kwa ukuu huohuo, hakuambatana na furaha za dunia, alikuwa huru kuhusu madai ya familia ili aiunde nyingine ya kimataifa, yaani Kanisa: hivyo ni kielelezo cha useja mtakatifu, wenye uzazi wa Kiroho usio na mipaka. Hatimaye, kwa ukuu wake upitao maumbile, Yesu hakuambatana na matakwa yake yoyote: akiwa na umri wa miaka kumi na miwili alitamka, ”imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu” (Lk 2:49), halafu “akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba” (Fil 2:8).

Kwa kuwa Mwokozi alitoka juu, hakuwa wa ulimwengu huu, bali alitolewa auokoe, ukuu wake wenyewe ulimtenga na mambo yote ya chini aweze kuufanyia kazi ulimwengu kutoka juu ili kazi hiyo ifike popote na ipenye zaidi, kama vile jua likifikia kilele cha mzunguko wake. Kwa kuwa huru kutoka vifungo vyote vya binadamu (mali, familia na mawazo finyu), Yesu aliweza kuwashughulikia wote akiwaletea uzima wa milele. Injili yake haizeeki, ni mpya daima, vile Mungu alivyo. Hivyo katika Bwana tunaona urekebisho wa ulinganifu wa asili pande zote tatu, urekebisho bora kuliko ukamilifu wa Adamu: “dhambi ilipozidi, neema ilikuwa nyingi zaidi” (Rom 5:20).

Urekebisho huo unatakiwa kuendelea katika Kanisa, linalopaswa kung’aa kwa utakatifu. Sifa yake hiyo inatakiwa kuwa ya ajabu na kuonekana, si tu mara mojamoja katika watu shujaa (k.mf. wafiadini na watakatifu waliotangazwa rasmi), bali mfululizo katika familia za kitawa ambamo idadi kubwa ya watu inafuata shule ya utakatifu na kutamka hadharani nia ya kumfuata Bwana kwa kuungana na Mungu wasiambatane na malimwengu. Lakini kuna tofauti kubwa kati ya Bwana na watu hao, hata wakiwa na juhudi nyingi namna gani: yeye alitoka juu, hao wametoka chini, katika dhambi na udanganyifu, na wanapaswa kujitenga navyo zaidi na zaidi ili kujitoa kwa Mungu kwa ndani zaidi na zaidi. Mwokozi anawapendekezea waliopokea wito huo maalumu waishi si tu kwa kufuata roho ya mashauri matatu ya Kiinjili, bali kwa kuyatekeleza kweli katika maisha ya pekee, akiwaahidia mara mia zaidi. Anawaalika wajitenge pande tatu ili kuwekwa wakfu pande tatu na hivyo kuhakikisha ustawi wa maadili hadi muungano na Mungu. Katika kutumia malimwengu anawashauri wajibanie wasije wakavutwa kuzidisha.

Anawaalika kutekeleza ufukara, kujitenga na matumizi huru na hata umilikaji wa vitu ili kuviweka wakfu kwa Mungu, visiwe tena vizuio, bali vyombo kwa safari ya kuelekea uzima wa milele. Anawaalika kuishi kwa usafi kamili, yaani kujinyima furaha za jinsia na kuuweka moyo wao wakfu kwa Mungu, usiwe tena kizuio, bali chombo kinachohuishwa na neema. Hatimaye anawaalika kuwa na utiifu mtakatifu, kujikomboa kutoka matakwa yao yote, yaliyojaa ugeugeu na ukaidi, ili utashi wao usiwe tena kizuio, bali chombo ambacho upendo unazidi kukifanya cha Kimungu ili kuungana na Mungu kwa undani na nguvu kila siku zaidi.

Utekelezaji wa maadili hayo matatu na wa nadhiri zake una shida, lakini unaondoa shida nyingine nyingi. Ndege anainua mabawa, lakini ni kweli zaidi kuwa mabawa yanamuinua ndege. Vilevile maadili ya kitawa na nadhiri zake vinamletea mtu wajibu wa pekee, lakini hasa vinamleta kwenye ukamilifu wa upendo kwa kasi na hakika zaidi.

Maadili ya ufukara, useja na utiifu yako chini ya adili la ibada ambalo linampa Mungu heshima inayotupasa, kwa hiyo ni kuu kuliko maadili mengine ya kiutu, likifuata mara yale ya Kimungu. Ndilo linalomtolea Mungu vitendo vya kitawa. Ili mtawa awe na msimamo wa kutorudi nyuma anajifunga kwa nadhiri, akiwajibika kutekeleza hayo matatu kwa mfano wa Bwana mpaka kufa: anajitoa pamoja naye kwa maisha mazima ya sadaka; na kwa kuwa anapaswa kutoa yote (vitu, mwili na moyo, matakwa) asijichukulie tena, jina la sadaka ya kuteketezwa linafaa kweli.

Sadaka hiyo itimizwe kwa dhati kila siku; hapo itatupatia mara mia zaidi. “Amin, nawaambieni: hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele” (Mk 10:29-30).

Tanbihi hariri

Viungo vya nje hariri

  Makala hii kuhusu dini ya Ukristo bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mashauri ya Kiinjili kama historia yake, matokeo au athari zake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.