Mbaraka Mwinshehe

Mwanamuziki kutoka Tanzania, Mbaraka Mwinshehe Mwaruka

Mbaraka Mwinshehe Mwaruka (27 Juni 1944 - 12 Januari 1979) alikuwa mwanamuziki maarufu wa muziki wa dansi kutoka nchini Tanzania.

Mbaraka Mwinshehe
Taarifa za awali
Jina la kuzaliwaMbaraka Mwinshehe Mwaruka
Amezaliwa(1944-06-27)Juni 27, 1944
Morogoro,
Tanzania
Amekufa12 Januari 1979 (umri 34)
Mombasa, Kenya
Kazi yakeMwimbaji, mtunzi, mpiga gitaa
Miaka ya kazi1950-1979

Ni mwanamuziki pekee aliyeshinda mashindano ya China miongo iliyopita akamshinda Franco.

Historia

Maisha na muziki

Mbaraka Mwinshehe Mwaruka alizaliwa mjini Morogoro akiwa mtoto wa pili kati ya watoto 12. Baba yake Mwinshehe Mwaruka alikuwa Mluguru msomi na karani katika mashamba ya katani, na mama yake alikuwa Mngoni. Kati ya hao kumi na mbili, ni yeye na wadogo zake Zanda na Matata ndio walikuwa wanamuziki, Zanda alikuwa mwimbaji, akiimba pia nyimbo za Kizungu katika bendi ya Morogoro na Matata alikuwa mpiga drum pia bendi hiyohiyo. Kutokana maelezo ya familia, babu yake Mbaraka alikuwa wa kabila la Wadoe wa Bagamoyo na alipelekwa Mzenga (Kisarawe) akawe chifu wa huko na wakoloni. Huko akaoa wake tisa na kupata watoto zaidi ya hamsini akiwemo baba yake Mbaraka. Mbaraka alisoma mpaka kidato cha tatu na kuacha shule ili awe mwanamuziki.

Kuingia kwake katika ulimwengu wa muziki

 
Bendi ya Super Volcano katika pozi tofauti.

.

Mbaraka Mwinshehe alianza kushiriki katika maonyesho ya Morogoro Jazz tangu akiwa shule, wakati huo alipenda kupiga sana filimbi katika mtindo wa kwela kutoka Afrika ya Kusini ukiwa na wapulizaji maarufu kama Spokes Mashiyan, na ulipendwa sana na vijana haswa wa shule na makundi mengi ya jiving yalikuweko katika shule za sekondari.

Hivyo alishiriki akiwa mpigaji wa filimbi wakati wa wikiendi. Siku moja kwenye mwaka 1965, wakati wanamuziki wa Morogoro Jazz wakiwa wamepumzika nje ya klabu yao Mbaraka alipita akiwa na begi kubwa walipomuuliza anaenda wapi muda ule ambao anatakiwa kuwa shule, aliwaambia kuwa hataki tena shule anaenda Dar es Salaam kutafuta maisha, walimsihi alale pale klabuni kwanza awaze hatima yake.

Kesho yake wanamuziki walishangaa kumkuta Mbaraka akifanya mazoezi ya gitaa kwani walikuwa wakimfahamu kama mpiga filimbi, kwa kuwa walikuwa na shida ya mpiga rhythm walimsihi aache safari ya Dar na abaki kwenye bendi kama mpiga rhythm, akakubali. Wakati huo ni wapiga tarumbeta, saxaphone na gitaa la solo pekee waliokuwa wanalipwa kwa mwezi, wengine wote walipata posho kidogo kila lilipopigwa dansi. Siku moja walialikwa Dar es Salaam kwa ajili ya mashindano na Kilwa Jazz, kabla ya kuondoka Mbaraka aligoma kwenda kwa kuwa alikuwa halipwi, wazee wa bendi wakakubali kumlipa shilingi 120 kwa mwezi, mpiga solo ambaye alikuwa akilipwa sh150 akagoma kwenda Dar kwa kutetea kuwa mpiga rhythm hastahili malipo, hivyo Mbaraka akasema angepiga pia solo, bendi ikaenda Dar ikiwa na mashaka kwani Kilwa Jazz Band wakati huo ilikuwa ni tishio, na wao walikuwa wakienda bila mpiga solo.

Mbaraka alilipiga vizuri sana solo katika mashindano hayo na bendi ikashinda. Akapandishwa mshahara hadi shilingi 250 ambazo zilikuwa ni kiwango cha juu sana, na kuanzia hapo mpaka alipoacha bendi na kwenda kuanzisha bendi yake Super Volcano, Mbaraka akawa mpiga solo wa Morogoro Jazz Band.

Upigaji wake wa gitaa, ni somo zuri sana kwa mpigaji anaetaka kujiendeleza katika upigaji wa gitaa la solo. Katika vipindi vyake vya kuanzia Morogoro Jazz hadi Super Volcano alipitia staili nyingi za muziki, baadhi kama Sululu, Likembe, Masika Zolezole na kadhalika. Tofauti na bendi nyingi ambazo hubadili majina ya mitindo bila kubadili muziki wenyewe, staili za Mbaraka zilionyesha mabadiliko. Nyimbo katika staili ya Likembe zilikuwa tofauti na zile za Masika Zolezole. Kipindi hicho wapenzi wa muziki waliweza kuondoka Dar es Salaam na kwenda Morogoro kufaidi wiki endi ya muziki aidha wa Cuban Marimba, au Morogoro Jazz.

Kifo cha Mbaraka

Siku ya 12 Januari 1979 ulimwengu wa muziki Tanzania ulitikisika kwa simanzi baada ya kusikika kifo cha mwanamuziki huyo, mpiga gitaa, muimbaji, mtunzi na kiongozi wa bendi wa miaka mingi na ambaye bendi yake ilikuwa imepiga karibu kila wilaya ya nchini Tanzania. Taarifa ziliingia jioni ya siku ile kupitia redio ya Taifa kuwa nguli huyu alifia hospitali katika jiji la Mombasa nchini Kenya muda wa saa 1:55 jioni kufuatia ajali ya gari.

Kwa maelezo ya Zebedee Japhet Kinoka (maarufu kama Super Zex) tarehe 12 Januari 1979 alikuwa anatoka maeneo ya Kisauni kumtembelea Mtanzania mwenzake aliyekuwa na hoteli huko, ambaye pia walitoka kijiji kimoja Maramba huko Tanga. Alipofika karibu na Kongoya Church aliona gari aina ya Peugot 404 nyeupe ikitoka upande wa Bush Bar na kwa spidi kali ikaenda na kuligonga lori moja lililokuwa likitokea upande mwingine.

Ilikuwa mchana kiasi kama saa 7 hivi. Watu wakakimbilia kungalia ajali akiwemo yeye. Na mara moja akamtambua Mbaraka na kuwambia watu kuwa huyo ni mwanamuziki Mtanzania anaitwa Mbaraka Mwinshehe. Katika gari lile kulikuweko watu watatu Mbaraka alikuwa amekaa mbele pamoja na dereva. Dereva (maelezo ya baadaye yalimtambua kuwa alikuwa rafiki wa Mbaraka na mkazi wa Moshi aliitwa Omari Abdi, kuna maelezo mengine kuwa Abdi pia alikuja fia hospitalini si pale kwenye ajali) na abiria aliyekuwa nyuma walikufa palepale, ikalazimika kuanza kukata mabati ili kumuondoa Mbaraka aliyekuwa amebanwa miguu katika gari lile lililoharibika, yeye alikuwa bado hai.

Wakati kazi hiyo inaendelea Zebedee alikimbilia Kengeleni Bar ambapo Jamhuri Jazz Band (Bendi ya Watanzania) ilkuwa ikipiga muziki nakuwambia kuwa mwenzao kaumia sana, nao wakatoka mbio, wakiwemo akina Harrisson Siwale. Mbaraka aliweza kutolewa kwenye gari na kupelekwa kwenye hospitali ya Makadara. Zebedee pia akatumwa kuwafuata wanamuziki wa bendi ya Super Volcano ambao wakati huo walikuwa wakipiga Zambia Bar, wanamuziki walipofika hospitali wakaambiwa watoe damu na wakaanza kukwepa kutoa damu kwa visingizio mbalimbali.

Muda si mrefu Mbaraka Mwinyshehe akafariki. Mbaraka alifarika 12 Januari 1979 akiwa na umri mdogo wa miaka 34 tu. Kwa kuwa mpaka wa Kenya na Tanzania ulikuwa umefungwa wakati huo kutokana na mgogoro kati ya serikali za nchi hizi mbili, mwili wa Mbaraka alisafirishwa mpaka mpakani na kupokelewa na ndugu marafiki na Maafisa wa Wizara ya Utamaduni.

Mbaraka Mwinyshehe alizikwa Mzenga Kisarawe.

Tazama pia

Viungo vya nje

  Makala hii kuhusu mwanamuziki/wanamuziki fulani wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mbaraka Mwinshehe kama wasifu wake, habari za maisha au kazi yake?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.