Zekaria (kwa Kiebrania זְכַרְיָה, Zekaria, "YHWH amekumbuka"; kwa Kigiriki Ζαχαρίας, Zakharias; kwa Kilatini Zacharias; kwa Kiarabu زكريا Zakariya au Zakkariya) alikuwa kuhani wa Israeli, pia nabii wa Mungu mjini Yerusalemu kati ya mwaka 520 KK na 518 KK.

Zekaria alivyochorwa na Michelangelo katika dari la Kikanisa cha Papa Sisto, Vatikani.

Habari zake zinapatikana hasa katika kitabu chake, cha 11 kati ya vile 12 vya Manabii Wadogo katika Tanakh (yaani Biblia ya Kiebrania) na kwa hiyo pia katika Agano la Kale la Biblia ya Kikristo.

Humo (Zek 1:1) anajitambulisha kama "mwana wa Berakia, mwana wa Iddo", ingawa kitabu cha Ezra (Ezra 5:1 na 6:14) kinamuita tu "mwana wa Iddo".

Kazi ya nabii huyo, iliyoanza wakati uleule alipotabiri nabii Hagai, ni mwanzo wa kipindi cha mwisho cha unabii katika Israeli kabla ya ujio wa Yohane Mbatizaji na Yesu Kristo.

Tofauti na Hagai, Zekaria hakuishia upande wa ujenzi mpya wa hekalu la Yerusalemu, bali alisisitiza pia utakaso wa waamini na ibada zao.

Tangu kale anaheshimiwa na Wakatoliki na Waorthodoksi kama mtakatifu.

Sikukuu yake huadhimishwa tarehe 6 Septemba[1] lakini pia 8 Februari na 31 Julai.

Mazingira hariri

Kabla ya uhamisho wa Babeli, ujumbe wa manabii ulitishia mara nyingi adhabu ya Mungu kwa uasi wa taifa lake.

Wakati wa uhamisho ujumbe ulikuwa wa faraja zaidi.

Ule wa Hagai na Zekaria ulilenga ustawi wa Wayahudi ambao walikuwa wamerudi Yerusalemu mwaka 538 K.K. ili kujenga upya hekalu, lakini walichelewa kutekeleza azma yao, kutokana na upinzani na mahangaiko ya kujipatia riziki katika mazingira magumu.

Mbaya zaidi, walikaribia kukata tamaa.

Kwa changamoto ya manabii wao, gavana Zerubabeli na kuhani mkuu Yoshua waliongoza wananchi kukazania ujenzi huo na kuukamilisha mwaka 515.

Muhtasari wa kitabu hariri

Kitabu kina sehemu mbili tofauti sana, yaani sura 1-8 halafu 9-14.

Sura nane za kwanza zinaleta njozi kadhaa kuhusu mwanzo mpya wa Wayahudi mjini Yerusalemu.

Sura nyingine sita zinatokana na mazingira tofauti (ya karne ya 4 K.K.) na kuleta njozi juu ya ujio wa Masiya na siku za mwisho.

Sura hizo zina mtindo wa kiapokaliptiko na wataalamu wengi wanasema ni kazi ya nabii mwingine wanayemuita Zekaria wa pili.

Tazama pia hariri

Tanbihi hariri

Marejeo hariri

  • The Student Bible, NIV. Michigan: Zondervan Publishing House, 1992.
  • D. Guthrie, (ed.) New Bible Commentary. New York: Eerdmans Publishing Company, 1970.
  • Stephen G. Dempster, Dominion And Dynasty: A Theology Of The Hebrew Bible. Illinois: Intervarsity Press, 2003. ISBN 978-0-8308-2615-5
  • Carroll Stuhlmueller, Haggai and Zechariah: Rebuilding With Hope. Edinburgh: The Handsel Press Ltd., 1988. ISBN 978-0-905312-75-0.

Viungo vya nje hariri

 
Wikimedia Commons ina media kuhusu: