Papa Gregori I (Roma, Italia, takriban 540 – Roma, 12 Machi 604) alikuwa Papa kuanzia 3 Septemba 590 hadi kifo chake[1].

Papa Gregori I.
Gregori akishughulikia muziki mtakatifu.
Mchoro wa Andrea Mantegna juu ya Gregori akiwa na Yohane Mbatizaji, Benedikto wa Nursia na Jeromu.
Papa Gregori I.
Kaburi la Gregori I, ndani ya Basilika la Mt. Petro huko Vatikano.

Alimfuata Papa Pelagio II akafuatwa na Papa Sabinian.

Jina lake la kuzaliwa pia lilikuwa Gregorius. Kutokana na umuhimu wake katika historia, hasa ya Kanisa na Italia, aliongezewa lile la Magnus, yaani "Mkuu".

Lakini mwenyewe, aliposikia kuwa Patriarki wa Konstantinopoli alijiita "Patriarki wa ekumene", aliitikia kwa kujiita "Servus servorum Dei" (yaani "Mtumishi wa watumishi wa Mungu"), jina linalotumiwa hata leo na kila Papa. Akijali umoja wa kidugu katika Kanisa lote, yeye aliona unyenyekevu unatakiwa kuwa adili la msingi la kila askofu kama lilivyokuwa kwa Kristo aliyetuosha miguu. Jina hilo alilojichagulia lilidhihirisha kabisa namna yake ya kuishi na kutenda.

Hamu yake ilikuwa kuishi kweli kama mmonaki, akizama daima katika Neno la Mungu, lakini kwa kumpenda alijifunza kuwa mtumishi wa wote katika nyakati za tabu.

Tangu zamani anaheshimiwa kama mtakatifu na babu wa Kanisa.

Mwaka 1298 Papa Bonifasi VIII alimuongezea sifa ya mwalimu wa Kanisa.

Sikukuu yake inaadhimishwa kila mwaka tarehe 3 Septemba[2].

Maisha hariri

Utoto na ujana hariri

Gregori alizaliwa Roma, Italia, mwaka 540 hivi katika familia ya ukoo maarufu ya Anici, akiwa mtoto wa seneta Gordianus na wa Silvia, ambao wanaheshimiwa kama watakatifu. Shangazi zake Emiliana na Tarsila, wakiishi nyumbani mwao kwa sala na toba kama mabikira wa Kristo, walimtia pia hisia za Kikristo kweli. Kati ya mababu wake kulikuwa na Papa Felisi II (483-492) na Papa Agapito I (535-536).

Alipokuwa na umri wa miaka 25 tu alifuata nyayo za baba yake katika shughuli za utawala na mwaka 572 alichaguliwa kuwa mkuu wa jiji la Roma. Kutokana na ugumu wa nyakati hizo, kazi hiyo ilimdai awajibike katika masuala mengi tofauti ikimuandaa kwa majukumu yake ya baadaye.

Kwa namna ya pekee alidumisha hisi ya kuwepo haja ya utaratibu na nidhamu katika mambo yote. Ndiyo sababu baadaye, akiwa papa, alihimiza maaskofu waendeshe shughuli zao kwa kufuata mfano wa uwajibikaji na utekelezaji wa sheria wa watawala wa kisiasa.

Mmonaki na balozi wa papa hariri

Hata hivyo maisha hayo hayakuweza kumridhisha. Kwa hiyo, baada ya muda mfupi aliyaacha, na akivutiwa na mfano wa Benedikto wa Nursia, aligeuza nyumba yake mjini kuwa monasteri na kujifanya mmonaki, halafu akajitahidi katika maisha ya sala na kutafakari Biblia na maandishi ya mababu wa Kanisa. Pia alianzisha monasteri 6 katika kisiwa cha Sicilia. Maisha hayo ya kuhusiana na Bwana tu yalimuandaa kutoa mafundisho yake bora na yalizidi kumvutia hadi mwisho, kama alivyoandika mara nyingi baadaye.

Lakini mapema, kutokana na sifa na mang’amuzi yake, Papa Pelagio II alimfanya shemasi akamtuma kama balozi kwenye ikulu ya Konstantinopoli, alipobaki miaka sita akiendelea kuishi kimonaki na wenzake kadhaa kati ya fahari za mazingira ya Kikaisari. Majukumu yake makuu yalikuwa kukomesha mabaki ya mabishano kuhusu ubinadamu wa Kristo na hasa kupata msaada wa Kaisari dhidi ya uvamizi wa Walombardi nchini Italia. Hata miaka hiyo ilimuandaa kwa kazi zake za baadaye.

Upapa hariri

Aliporudi Roma, mwaka 586, akarejea monasterini, lakini Papa huyo alimfanya katibu wake. Ilikuwa miaka migumu kwa mvua za mfululizo, mafuriko na njaa mjini Roma na sehemu mbalimbali za Italia. Hatimaye tauni ilifyeka watu wengi, Pelaji II akiwa mmojawao.

Hivyo tarehe 3 Septemba 590 alishangiliwa na wakleri, maseneta na umati wa watu kwa kauli moja awe Papa wa 64. Ndiye mmonaki wa kwanza kufikia Upapa, ingawa hakutaka, hata akajaribu kukimbia, lakini bure. Ilimbidi akubali mapenzi ya Mungu, akaanza mara kuwajibika.

Mapema alionekana kuwa na mitazamo na maamuzi sahihi na kujitokeza kama mtendaji bora upande wa Kanisa na hata upande wa jamii na siasa (kwa sababu hiyo aliitwa "Mrumi wa mwisho"), ingawa alikuwa na afya mbovu, kiasi cha kulazimika mwishoni kubaki kitandani kwa siku kadhaa. Hasa mafungo makali ya kimonaki yalikuwa yamesababisha matatizo makubwa ya tumbo.

Tena sauti yake ilikuwa ndogo kiasi kwamba mara nyingi ilimbidi kumpa shemasi kazi ya kutangaza hotuba yake alipoendesha ibada makanisani kati ya waumini waliomheshimu sana kwa kumuona anawafanya wajisikie salama. Hotuba hizo zinaonyesha alivyotekeleza alichoandika: “Ni lazima mhubiri achovye kalamu yake katika damu ya moyo wake; hapo ataweza kufikia masikio ya majirani wake”.

Aliwasiliana na viongozi wa nchi mbalimbali za Ulaya, na hasa wa kabila la Wafaranki ambalo lilikuwa la kwanza kati ya yale ya Kijerumani kuingia Ukatoliki moja kwa moja tena lilijitokeza lenye nguvu kuliko yote.

Vilevile alifanikisha uongofu wa makabila ya aina hiyo yaliyoteka Uingereza, alipomtuma kama mmisionari Augustino wa Canterbury, priori wa monasteri yake ya Mt. Andrea.

Alilinda pia Roma dhidi ya uvamizi wa Agilulf, mfalme wa Walombardi, lakini, kinyume na Kaisari aliyewaona ni washenzi na wavamizi tu ambao wadhibitiwe au kuangamizwa, Gregori, kwa mtazamo wa kichungaji, alijenga nao uhusiano mpya ili kuwaleta kwenye Kanisa Katoliki kutoka uzushi wa Ario, kama alivyofanya pia na Wagoti wa Hispania na walioendelea kufuata dini za jadi.

Akilenga amani ya kudumu nchini Italia, kwa msaada wa Theodolinda, malkia Mkatoliki wa Walombardi, alifanikiwa kwanza kusimamisha mapigano na Walombardi kwa miaka mitatu (598-601), na kuanzia mwaka 603 kwa muda mrefu zaidi.

Lakini mafanikio yake hayo, yaliyoandaa mengine kwa siku za mbele, yalimfanya achukiwe na watu wa Konstantinopoli.

Alipambana na matatizo mengine ya Italia, kama vile mafuriko, njaa, tauni, akisimamia kwa usawa masuala ya kijamii yaliyopuuziwa na wawakilishi wa kaisari. Kwa mapato ya mali ya Kanisa, aliyoisimamia vizuri na kwa kuzingatia haki, kati ya mambo mengine alilisha wenye njaa na kukomboa watumwa. Alishughulikia hata huduma ya maji.

Alirekebisha liturujia ya Kiroma, akipanga matini ya zamani na kutunga mengine mapya, pamoja na kushughulikia muziki wa ibada za Kilatini ambao kwa heshima yake unaitwa wa Kigregori.

Vitabu vyake, hasa vya maadili na vya ufafanuzi wa Maandiko matakatifu unaolenga utekelezaji, barua 848 zilizotufikia pamoja na hotuba mbalimbali vinashuhudia kazi zake nyingi na ujuzi wake wa Biblia.

Pia aliandika maisha ya watakatifu kadhaa wa Italia walioishi si zamani sana, kama vile Benedikto wa Nursia ambaye tunamfahamu kwa njia hiyo tu. Ni kwamba rafiki yake, Petro shemasi, alidhani wakati ule maadili yameharibika kiasi cha kuzuia upatikanaji wa watakatifu kama walivyotokea zamani. Basi, Gregori alimuonyesha kwamba, kinyume chake, utakatifu unawezekana daima, hata katika mazingira magumu. Masimulizi ya maisha yao yanaendana na hoja za kiteolojia zinazofafanua masuala mbalimbali.

Kitabu kingine kilichoacha athari kubwa ni "Mwongozo wa Kichungaji" kwa ajili ya maaskofu, ambao ulitafsiriwa mapema hata kwa Kigiriki na kwa Kisaksoni. Alikiandika mwanzoni mwa Upapa wake akautekeleza mwenyewe. Humo anasisitiza ukuu wa cheo hicho na majukumu yanayoendana nacho, ambayo yanadai askofu awe kielelezo kwa wote. Kwa ajili hiyo anapitia kwa makini aina mbalimbali za waumini na saikolojia zao ili kuonyesha namna ya kuwasaidia. Hatimaye anakazia unyenyekevu wa kutojiona sawa mbele ya Hakimu mkuu kutokana na mafanikio fulanifulani: “Mtu anaporidhika kwa kutimiza maadili mengi, ni vema afikirie mapungufu yake na kujinyenyekesha: badala ya kuzingatia mema aliyofanya, ni lazima azingatie yasiyofanyika”. Kwake uchungaji ni “ars artium”, yaani sanaa kuu kuliko zote.

Katika maandishi yake, hakukusudia kamwe kutoa mafundisho mapya, bali kuwa mwangwi mnyenyekevu wa mapokeo ya Kanisa. Alieneza mafundisho ya Augustino wa Hippo, akisisitiza kama yeye hali ya dhambi ya binadamu, nafasi ya kwanza ya neema katika wokovu pamoja na imani katika uteuzi wa watakaookoka uliofanywa na Mungu.

Pia alichangia ustawi wa fundisho la uwepo wa toharani.

Mtu huyo alikuwa wa ajabu kuliko kazi zake, akivutia kwa nguvu na upendevu wa tabia. Ndani mwake upana wa moyo na roho ya Kikristo vilitegemeza yote.

Inawezekana kusema ndiye Papa wa kwanza kutumia mamlaka upande wa siasa pia, lakini bila kuweka pembeni majukumu yake ya kiroho kama mtu aliyeungana kweli na Mungu na hivyo aliweza kuona la kufanya. Kwake ilikuwa muhimu kila mmoja atafakari matukio ya maisha katika mwanga wa Neno lake kwa sababu historia ya wokovu haikumalizika zamani, bali inaendelea moja kwa moja hata katika nyakati ngumu kama zile alizopitia mwenyewe.

Alifariki Roma tarehe 12 Machi 604.

Tazama pia hariri

Tanbihi hariri

Maandishi yake hariri

Vyanzo hariri

  • Cantor, Norman F. (1993). The Civilization of the Middle Ages. New York: Harper. 
  • Cavadini, John, ed. (1995). Gregory the Great: A Symposium. Notre Dame: University of Notre Dame Press. 
  • Dudden, Frederick H. (1905). Gregory the Great. London: Longmans, Green, and Co. 
  • Ekonomou, Andrew J. 2007. Byzantine Rome and the Greek Popes: Eastern influences on Rome and the papacy from Gregory the Great to Zacharias, A.D. 590-752. Lexington Books.
  • Richards, Jeffrey (1980). Consul of God. London: Routelege & Keatland Paul. 
  • Straw, Carole E. (1988). Gregory the Great: Perfection in Imperfection. Berkeley: University of California Press. 
  • Leyser, Conrad (2000). Authority and Asceticism from Augustine to Gregory the Great. Oxford: Clarendon Press. 
  • Markus, R.A. (1997). Gregory the Great and His World. Cambridge: University Press. 
  • Ricci, Cristina (2002). Mysterium dispensationis. Tracce di una teologia della storia in Gregorio Magno. Rome: Centro Studi S. Anselmo. . Studia Anselmiana, volume 135.

Viungo vya nje hariri