Proxima Centauri ni nyota iliyo karibu kabisa na Jua hivyo pia na Dunia. Ni sehemu ya mfumo wa Rijili Kantori inayojulikana kama Alpha Centauri. Umbali wake na Jua ni miakanuru 4.22.

Nyota mbili angavu ni Alpha na Beta Centauri; nyota hafifu katika duara nyekundu ni Alpha Centauri C = Proxima Centauri

Majina hariri

Proxima Centauri ni jina rasmi la nyota hii. Inajulikana pia kama "Alfa Centauri C" maana ni nyota ya tatu katika mfumo wa Alfa Centauri inayoitwa kwa Kiswahili "Rijili Kantori". Rijili Kantori (Alfa Centauri) inaonekana kama nyota moja angavu lakini kwa darubini kubwa inaonekana kuwa mfumo wa nyota 3 zinazoshikamana kwa kuzunguka kitovu cha graviti cha pamoja. Nyota hizi zinatofautishwa kwa kuziita Alfa Centauri A, B, na C.

"Proxima Centauri" ni jina la Kilatini lenye maana "proxima"= karibu zaidi na "Centauri" katika makundinyota ya Centaurus inayojulikana kwa Kiswahili kama "Kantarusi" au Kantori.

Tabia hariri

Proxima Centauri ni nyota kibete nyekundu inayofuata wenzake Alfa Centauri A na B kwa umbali mkubwa unaobadilika kati ya vizio astronomia 5,270 hadi 12,900. Uangavu unaonekana ni mag 11.05 ilitambuliwa mwaka 1915 tu. Kipenyo chake ni kilomita 200,000 na hii sehemu ya saba ya kipenyo cha Jua letu, au mara mbili kipenyo cha sayari Mshtarii. Masi yake ni asilimia 12.3 za masi ya Jua.

Mwaka 2016 sayari moja ilitambuliwa inayozunguka Proxima Centauri kwa umbali wa vizio astronomia 0.05 katika kipindi cha siku 11 za Dunia. Masi yake ni takriban mara 1.5 ya Dunia.[1]

Tanbihi hariri

  1. Planet Found in Habitable Zone Around Nearest Star Pale Red Dot campaign reveals Earth-mass world in orbit around Proxima Centauri, tovuti ya ESA, iliangaliwa Julai 207

Viungo vya Nje hariri

 
Wikimedia Commons ina media kuhusu: