Satyajit Ray (2 Mei 1921–23 Aprili 1992) alikuwa muongozaji muigizaji filamu kutoka jimbo la Bengal Magharibi nchini Uhindi. Watu wengi humhesabu kati ya waongozaji muhimu sana wa sinema katika karne ya 20.[1]

Satyajit Ray

Satyajit Ray
Amezaliwa (1921-05-02)2 Mei 1921
Amekufa 23 Aprili 1992 (umri 70)

Alizaliwa mjini Kolkata mnamo 1921 katika familia ya wasanii na waandishi wengi. Ray alisoma kwenye shule ya upili ya serikali ya Ballygunge akaendelea kuchukua B.A. ya uchumi kwenye chuo kikuu cha Kolkotta. Akaendelea kusoma sanaa kwenye chuo kikuu cha Visva-Bharati kilichoanzishwa na Rabindranath Tagore. Alisema baadaye ya kwamba alijifunza mengi kutoka wachoraji mashuhuri Nandalal Bose na Benode Behari Mukherjee. Baada ya chuo alianza kufanya kazi katika kampuni ya matangazo ya kibiashara kama mchoraji msaidizi. Akahamia kampuni ya uchapishaji alipochora picha za vitabu. Mwaka 1947 aliunda klabu ya filamu za Kolkota alipoanza kuangalia filamu nyingi za kigeni.

Baada ya kufunga ndoa na Bijoya Das alikutana na mwongozaji Mfaransa Jean Renoir akamsaidia kupata mahali pa kupiga picha akaweza kujailiana naye juu ya mipango ya kufanya filamu mwenyewe. 1950 Ray alitumwa London kikazi alipoangalia filamu 99 katika muda wa miezi 3. Alivutwa sana na filamu ya Vittorio de Sica "Ladri di biciclette" (wezi wa baisikeli) (1948); alisema baadaye alipotoka sinema alikata shauri kuwa mwongozaji katika maisha yake.

1952 alianza kazi kwa filamu yake ya kwanza Pather Panchali inayofuata riwaya yenye jina hili ikisimulia safari ya kijana Apu anayetoka kijijini kutafuta maisha ya mjini. Alianza filamu kwa pesa kidogo na kuendelea polepole. Akakamilika baada ya miaka 3 na filamu ilikuwa na mafanyikio makubwa pamoja na tuzo kwenye Tamasha la Filamu la Cannes. Akaendelea kutoa filamu mbili nyingine juu ya maisha ya Apu akashinda tuzo la tamasha la filamu la Venisi.

Filamu za Mahanagar (1963) na Charulata (1964 - hii alitazama kama kazi yake bora) zilipokea tuzo la "dubu fedha" kwenye tamasha la filamu Berlin, kwa Ashani Sanket (1973) alipata hapa "dubu dhahabu". 1978 alipata tuzo kuu la Uhindi Filmfare Award kwa filamu yake Shatranj Ke Khilari (wachezaji wa sataranji; filamu ya pekee aliyofanya kwa Kiurdu/Kihindi na Kiingereza) ambako Richard Attenborough aliigiza.

Katika miaka ya 1980 Ray alipaswa kuendelea kutokana na ugonjwa lakini filamu zake za mwisho Shakha Proshakha (1990) na Agantuk (1991) zilisifiwa tena sana.

Msingi wa filamu zake karibu zote ulikuwa vitabu vya fasihi ya Kibengali. Mafanyiko makubwa ya kiuchumi alipata kwa filamu Goopy Gyne Bagha Byne (1968) kutokana na hadithi kwa watoto ya babu yake mwenyewe Upendrakishore Raychowdhury.

Mwaka 1992 aliheshimiwa kwa kupewa tuzo la Oscar kwa kazi ya maisha yake. Akademi ya kutoa tuzo ilisema: „In recognition of his rare mastery of the art of motion pictures, and of his profound humanitarian outlook, which has had an indelible influence on filmmakers and audiences throughout the world.“ Hakuweza kusafiri tena kupokea tuzo akaishika kwenye kitanda chake muda mfupi kabla ya kuaga dunia.

Muongozaji Mjapani Akira Kurosawa alisema juu ya Ray: „Kama hujaona sinema za Ray ni kama kuishi duniani bila kuona jua au mwezi.“

Marejeo hariri

  1. Santas 2002, p. 18