Suheli (ing. na lat. Canopus ka-no-pus, pia α Alpha Carinae, kifupi Alpha Car, α Car) ni nyota angavu zaidi kwenye kundinyota la Mkuku (Carina). Ni pia nyota angavu ya pili kabisa kwenye anga baada ya Shira (Sirius).

Suheli (Alfa Carinae, Canopus)
Suheli - Canopus jinsi inavyoonekana pamoja na Wingu Kubwa la Magellan huko Chile
Kundinyota Mkuku (Carina)
Mwangaza unaonekana -0.74
Kundi la spektra A9 II[1]
Paralaksi (mas) 10.55
Umbali (miakanuru) 310 ± 20
Mwangaza halisi -5.71
Masi M☉ 8
Nusukipenyo R☉ 71
Mng’aro L☉ 10.7
Jotoridi usoni wa nyota (K) 6998
Muda wa mzunguko siku 135
Majina mbadala Suhayl, Suhel, Suhail, Alpha Carinae, CD−52°914, FK5 245, GC 8302, HD 45348, HIP 30438, HR 2326, SAO 234480

Jina

Nyota ya Suheli ilijulikana kwa mabaharia Waswahili tangu miaka mingi wakifuata njia yao baharini wakati wa usiku kwa msaada wa nyota. [2]. Walipokea jina hili kutoka Waarabu wanaoijua kama سهیل suhail na katika hadithi moja ya Waarabu hii ni jina la mtu mbaya aliyeishi Uarabuni hadi aliondolewa duniani na Mungu na kupelekwa angani akawa nyota [3]. Pia nyota λ Lambda Velorum inaitwa "Suhail" - hili ni jina lilelile kama Suheli (Canopus). Sababu yake ni ya kwamba Waarabu walitumia jina hili kwa nyota tatu katika kundinyota la Argo iliyovunjika baadaye. Suhail inayotokana na neno سَهُلَ sahula “tambarare, isiyo na matata” ikitumiwa na Waarabu kwa nyota mbalimbali na pia kama jina la mwanaume. [4].

Jina la kimataifa ni Canopus ambalo lilipokelewa na kuthibitishwa na UKIA kama jina maalum.[5]. Asili yake iko katika lugha ya Kigiriki; ilionekana kwa Wagiriki wa Kale kama vile Eratosthenes na Klaudio Ptolemaio waliokaa Misri (maanake haionekanI katika Ulaya penyewe) walioipa jina la Κονοβος ko-no-bos kwa kumbukumbu ya nahodha wa mitholojia yao; kwa uzoefu wa Kilatini jina hili lilikuwa Canopus [6]. Hapa ni mfano ambako UKIA haukufuata kawaida ya kupokea majina ya Kiarabu kwa sababu « Suhail » ilitumiwa kwa nyota mbalimbali.

Alfa Carinae ni jina la Bayer. Nyota za Mkuku (Carina) zilikuwa sehemu ya kundinyota la kale la Argo na Alfa ilikuwa na mwangaza mkuu. Hapo Nicolas Louis de Lacaille alitoa herufi za Kigiriki kwa nyota za Argo lakini baadaye aligawa Argo kwa makundinyota matatu ya Shetri (Puppis), Mkuku (Carina) na Tanga (Vela). Mkuku ni kundi la pekee kati ya hizi tatu iliyo na nyota ya "Alfa" lakini haina "Beta" au "Gamma" maana hizi ziligawiwa baadaye kwa Tanga na Shetri.

Tabia

Suheli ina mwangaza unaoonekana wa -0.74, mwangaza halisi ni -5.71.Umbali wake na Dunia ni miakanuru 509 [7].

Miaka mingi ilikuwa vigumu kukadiria umbali wa Suheli na tabia nyingine. Tangu kupatikana kwa vipimo vya darubini ya angani Hipparcos umbali wake ulipimwa kuwa miakanuru 309-310 kutoka Jua letu. Ni kubwa kuliko Jua letu, kipenyo chake ni mara 70 cha Jua na kama ingekuwepo katika mfumo wa Jua letu ingefikia karibu hadi obiti ya sayari Utaridi. Mwangaza halisi ni mara 13,000 kushinda Jua.

Tanbihi

  1. tazama Lopez (1993), uk. 66; lakini katika orodha ya Hiparcos inatajwa kuwa F0 Ib ([1])
  2. ling. Knappert 1993
  3. Lane, Arabic‐English Lexicon: ُ سھيل A certain star [well known; namely, Canopus]; (TA:) it is said that سھيل was a tyrannical collector of the tithes on the road to El‐Yemen, and God transformed him into a star (uk 1469 toleo la pdf)
  4. Allen, Star-Names (1899), uk. 72
  5. Naming Stars, tovuti ya Umoja wa Kimataifa wa Astronomia (Ukia), iliangaliwa Novemba 2017
  6. linganisha Allen uk 67
  7. CANOPUS (Alpha Carinae), tovuti ya Prof Jim Kaler, University of Illinois, iliangaliwa Oktoba 2017

Viungo vya Nje

Marejeo

  • Allen, Richard Hinckley: Star-Names and their Meanings; kwa G. E. Stechert New York, Leipzig, London, Paris 1899, ukurasa 437 (online kwenye archive.org)
  • Cruzalèbes, P.; Jorissen, A.; Rabbia, Y.; Sacuto, S.; Chiavassa, A.; Pasquato, E.; Plez, B.; Eriksson, K.; Spang, A.; Chesneau, O. (2013). "Fundamental parameters of 16 late-type stars derived from their angular diameter measured with VLTI/AMBER". Monthly Notices of the Royal Astronomical Society. 434: 437 online hapa
  • Lopez-Cruz, O.; Garrison, R. F. (1993). "A Spectroscopic Study of High Galactic Latitude F Supergiant Stars". Luminous High-Latitude Stars. the International Workshop on Luminous High-Latitude Stars. 45: 59 online hapa
  • Knappert, Jan: The Swahili Names of Stars, Planets and Constellations; The Indian Ocean Review September 1993 Volume 6 No. 3 September 1993, kurasa 6-7, ISSN 1031-2331
  • Ptolemy's Almagest, translated and annotated by G.J. Toomer, London 1984, ISBN 0-7156-1588-2 online hapa