Thumni (kundinyota)

Thumni (kwa Kilatini na Kiingereza Octans) [1] ni jina la kundinyota dogo kwenye nusutufe ya kusini ya Dunia yetu iliyopo kwenye ncha ya anga ya kusini.

Nyota za kundinyota Thumni (Octans ) katika sehemu yao ya angani
Ramani ya Thumni;

Mahali pake hariri

Ilhali Thumni ni kundinyota ambalo lina ncha ya anga ya kusini ndani yake, ukiwa Tanzania au Kenya haiwezekani kuliona kamili kwa wakati mmoja maana nyota zake ziko karibu na upeo wa anga upande wa kusini. Sehemu ya nyota zake ziko chini ya upeo wa anga kila wakati lakini zinatokea baadaye kadri anga linavyozunguka.

Thumni iko jirani na makundinyota saba ya Ndege wa Peponi (Apus), Meza (en:Mensa), Kinyonga (en:Chamaeleon), Tausi (en:Pavo), Mhindi (en:Indus) , Tukani (en:Tucana) na Nyoka Maji (en:Hydrus).

Nyota iliyo karibu zaidi na ncha ya anga ni σ Sigma Octantis ambayo ni´nyota yenye uangavu wa mag 5.47 hivyo ni dhaifu mno na si msaada kwa mabaharia kama mwenzake Kutubu (Polaris) kwenye nusutufe ya kaskazini.

Jina hariri

Thumni ni kati ya makundinyota yaliyobuniwa katika enzi ya kisasa. Kama nyota nyingine zinazoonekana kutoka nusutufe ya kusini pekee haikujulikana kwa Wagiriki wa Kale wala kwa Waarabu kwa hiyo wataalamu wa Ulaya hawakuwa na habari nazo. Kundinyota hili lilielezwa mara ya kwanza na Mfaransa Nicolas-Louis de Lacaille wakati wa karne ya 18 kwa jina “ Caela Sculptoris“ lililomaanisha “ Thumni za mchongaji“. Lacaille alikaa miaka miwili kwenye Rasi ya Tumaini Jema (Afrika Kusini) alipotazama nyota za anga la kusini ambazo wakati ule zilianza tu kujulikana kati ya wanaastronomia wa Ulaya. Hapo alipima nyota 10,000 na kuzipanga kwa kundinyota na kutunga majina kwa makundinyota mapya 14[2]. Jina la Kifaransa lilitafsiriwa kwa Kilatini na kufupishwa kama "Octans“(Thumni).

Chaguo la jina lilikuwa dalili ya kipindi cha Zama za Mwangaza ambako Lacaille alitumia majina ya zana za siku zake kwa kutaja nyota, si tena majina ya mitholojia ya kale. Hapa alichagua “Octans“ iliyokuwa kifaa cha kibaharia cha kupimia pembe kati ya nyota kwa kusudi ya kukadiria mwelekeo wa safari. Kifaa hiki kinatumia skeli ya nyuzi 45 yaani sehemu ya nane au “thumni“ ya duara kamili.

Thumni - Octans imepokelewa kati ya makundinyota 88 yanayoorodheshwa na Umoja wa kimataifa wa astronomia [3] kwa jina la Octans. Kifupi chake rasmi kufuatana na Ukia ni 'Oct'.[4]

Nyota hariri

Nyota za Thumni ni chache na dhaifu; angavu zaidi ni ν Nu Octantis yenye mwangaza unaoonekana wa mag 3.7 ikiwa na umbali wa miaka nuru 69 kutoka Dunia.

Hakuna nyota iliyopo kikamilifu mahali pa ncha ya angani lakini σ Sigma Octantis iko karibu na hivyo inaitwa wakati mwingine « Polaris Australis » (nyota ya ncha ya kusini ya anga)[5]. Lakini Sigma Octantis haikupata umuhimu sawa kama Kutubu (en:Polaris) ambayo ni nyota inayoonyesha ncha ya anga ya kaskazini ikiwa ni nyota angavu zaidi ya mag 1.98 iliyotumiwa na mabaharia tangu karne nyingi kujua upande wa kaskazini. Kwenye nusutufe ya kusini ya Dunia ni zaidi kundinyota la Salibu iliyotumiwa kwa kusudi hii maana mstari mrefu wa msalaba wake unadokeza upande wa ncha ya kusini angani.

Tanbihi hariri

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Octans " katika lugha ya Kilatini ni "Octantis na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Octantis, nk.
  2. Histoire de l'Académie royale des sciences ; taarifa ya Lacaille katika "Historia ya Akademia ya Kifalme ya sayansi", uk. 588, Tovuti ya Bibliothèque nationale de France (BnF), iliangaliwa Julai 2017
  3. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  4. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R. 
  5. Sigma Octantis Tovuti ya jumk.de Special stars, iliangaliwa Oktoba 2017

Viungo vya Nje hariri

  Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Thumni (kundinyota) kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.