Unju bin Unuq (pia: Unju bin Unuku, Unzi Bin Ununuk) ni jina la jitu katika masimulizi ya wakazi wa pwani ya Tanzania. Hadithi zake zasimuliwa kuanzia Bagamoyo hadi Kilwa.

Unju bin Unuq akibeba mlima anaotaka kuurusha dhidi ya Musa; picha katika nakala ya Kituruki ya Kitabu ‘Ajā’ib al-makhlūqāt (maajabu ya viumbe) كتاب عجائب المخلوقات وغرائب الموجودات cha Zakarīyā’ ibn Muḥammad al-Qazwīnī.

Historia yake inapatikana katika makumbusho ya Kaole huko Bagamoyo.

Moja ya mambo ya ajabu ya mtu huyu ni urefu wake yaani kimo, inasadikiwa alikuwa na urefu mkubwa ulioweza kumfanya atembee baharini na miguu yake kugusa chini.

Pia alikuwa akitembea kutoka nchi hadi nchi kutokana na urefu wake. Inasimuliwa kuwa mmoja kati ya nyayo zake unapatikana kwenye jiwe alilokanyaga huko Tabora, Tanzania, wayo wa mguu wa kushoto wakati wayo wa mguu wa kulia ulionekana kwenye jiwe alilokanyaga huko Kongo.

Inasimuliwa pia akitaka kula alikuwa akichukua samaki baharini kwa mkono na kuchoma katika jua kisha anakula.

Kuhusu maisha yake inasimuliwa kuwa Unju bin Unuk hakuoa wala kuolewa kutokana na umbo lake.

Sehemu nyingine ya hadithi yake ni alipokufa Unju bin Unuq, aligawanyika vipandevipande kutokana na urefu wake na inasemekana kidole chake chenye urefu wa kilometa moja kasoro ndicho kilichopatikana na kuzikwa pale Bagamoyo, lakini hakuna simulizi mwili wake uliobaki uliangukia wapi.

Unju bin Unuq alikuwa na ndugu yake aliyejulikana kama Geofrey bin Unuk, huyu alipatikana maeneo ya Dodoma. Au kwamba Unuq baada ya kupotea kwa muda wa miaka mingi ndugu zake wa mbali sana wameonekana katika mkoa wa Dodoma.

Asili ya jina la Unju bin Unuq katika Uarabuni na Biblia hariri

Jina lake linatokana na Kiarabu cUdj bin Unuq / ‘Anaq عوج بن عنق anayejulikana katika visa vya nchi nyingi za Uislamu kama jitu kubwa sana. Waislamu walipokea hadithi kutoka kwa Wayahudi anakojulikana kwa jina la Og עוֹג‬.

Asili kabisa ni taarifa za Biblia kuhusu mapigano kati ya Wanaisraeli waliotoka Misri na Ogu mfalme wa Bashani (Hesabu 21,33)[1]; Wanaisraeli walimshinda wakiongozwa na Musa.

Ogu alisemekana kuwa mtu mrefu; Kumbukumbu la Torati 3,11 kinamtaja hivi: "aliyesalia katika mabaki ya Warefai ni Ogu pekee, mfalme wa Bashani; tazama, kitanda chake kilikuwa kitanda cha chuma; kitanda hicho je! Hakiko Raba kwa wana wa Amoni? Urefu wake ulikuwa ni mikono kenda, na upana wake mikono minne, kwa mfano wa mkono wa mtu".

Katika masimulizi ya Wayahudi sifa hiyo iliendelea kuongezeka; katika Kitabu cha Amosi 2,9 anatajwa (bila kusema jina) kama "Mwamori" "nalimwangamiza Mwamori mbele yao, ambaye urefu wake ulikuwa kama urefu wa mierezi, tena alikuwa na nguvu kama mialoni".

Wataalamu Wayahudi wa baadaye waliona ya kwamba vipimo vya Kumb. 3 kuhusu kitanda chake chenye urefu wa mikono yaani dhiraa 10, sawa na mita 4-5, vilihusu mkono wa hilo jitu lenyewe, hivyo walimwona mkubwa zaidi tena.

Kwenye kitabu Berakhot cha Talmudi Ogu anasimuliwa ya kwamba aliweza kuinua mlima aliotaka kurusha dhidi ya Wanaisraeli, lakini Mungu alimzuia[2]. Katika kitabu cha Nidah katika Talmudi Ogu anasemekana ni mtu aliyeishi kabla ya gharika ya Nuhu akiwa ni mmoja wa hao ambao walitunzwa.[3]

Katika Uislamu hariri

Masimulizi ya Kiyahudi yalipokewa na Waislamu na kupanuliwa tena. Ushahidi uko kwa Al Tabari aliyeandika ya kwamba maiti ya cUdj ilikuwa kama daraja juu ya mto Naili.

Al-Thaclabi aliandika ya kwamba cUdj alikuwa na urefu wa dhiraa 23,333 akiweza kunywa kwenye mawingu, kushika ngumi baharini na kuichoma kwenye Jua. Alitembea mbele ya Nuhu wakati wa gharika kuu lakini maji yalifikia magoti yake tu. Aliishi miaka 36,000. Alipoona kambi la Wanaisraeli na Musa alivunja mlima akashika kipande cha kuangamiza kambi lote kwa pigo moja, lakini Mungu alituma ndege waliokula shimo katikati ya mlima uliomuangukia na kumfunga katikati. Hivi Musa aliweza kumshinda kirahisi.[4]

Tazama pia hariri

Tanbihi hariri

  1. Bashani ilikuwa eneo la Syria ya leo, upande wa kusini wa Dameski.
  2. Berakhot 54b, Babylonian Talmud: Tractate Berakoth
  3. Talmud - Mas. Nidah 61a,English Babylonian Talmud, SEDER TOHOROTH, tractate Nida
  4. Angalia makala cUDJ katika Encyclopedia of Islam, uk. 777

Marejeo hariri

  Makala hii kuhusu mambo ya utamaduni bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Unju bin Unuq kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.