Wakabwa

Makabila kutoka Mkoa wa Mara nchini Tanzania

Wakabwa (au Wakabhwa, matamshi ambayo ni sahihi zaidi) ni kabila la watu wa Tanzania linaloishi katika Mkoa wa Mara. Lugha yao ni Kikabwa.

Idadi yao ni takribani watu 6000.

Wanapatikana katika vijiji vya Bukabwa, Mmazami (hapa wamechanganyika na Wazanaki, au 'Abhazanake', au 'Abhashanake'), Kamugendi (hapa wamechanganyika na Wazanaki na Wairege), na Kirumi (hapa wamechanganyika na Wakiroba au 'Abhakerobha').

Kama ilivyo kwa wakazi wengi wa Mkoa wa Mara, Wakabwa ni jamii au ukoo wa kabila kubwa la Wakurya. Mila na desturi zao zinaelekeana na koo nyingine za Kikurya. Lugha yao haina tofauti na makabila yanayojiita makabila ya Kikurya ijapokuwa ni koo tu. Matamshi yao yanaelekeana na Wasweta ambao hupatikana kwa wingi wilaya ya Tarime kando ya ziwa Victoria, jirani na Wasimbiti (Abhasimbete).

Kuna koo kubwa za Warimba, Washora na Waruhu.

Shughuli zao kubwa ni ukulima wa uwele, mtama, mhogo na ufugaji wa wanyama mbalimbali kama ng'ombe, mbuzi na kondoo.

Ni watu wanaomini sana kuhusu uchawi, ndiyo maana hata vijiji vyao vimeshindwa kufanya maendeleo ya haraka kwa kuhofia kulogwa.

Wengi wao wanapatikana katika kijiji cha magana na kirumi. Wanatahiri wanaume na kukeketa wasichana, ingawa mila hii ya kukeketa wasichana inaelekea kwisha.

Kuna milima kama Kimange, Magana, Misisya na Kweswa na kuna mito kama Nyamirama.

Watu maarufu katika jamii ya Wakabwa hariri

Miongoni mwa watu maarufu katika jamii ya Wakabwa ni yule aliyekuwa "Chifu/Mwanangwa" wao, Matambalya wa Wandibha. Kutokana na uchache wao, 'Mwanangwa' ndiye aliyekuwa kama 'Chifu' wa Wakabwa, na aliripoti kwa Chifu wa Wazanaki.

Jina la mama mzazi wa Matambalya ni Nyesa. Ndugu zake walikuwa Makongoro (kaka zake), na Nyakubhoga (dada yake). Hata hivyo Matambalya wa Wandibha alifariki dunia bila kufikia umri mpevu.

Mtawala huyo, yaani Matambalya wa Wandibha, ndiye babu wa kibiolojia (kwa upande wa baba) wa msomi maarufu kutoka Mkoa wa Mara, Prof. Francis Shasha (hutamkwa pia Chacha) Matambalya, aliyepata kufundisha Chuo kikuu cha Dar es Salaam, Chuo Kikuu cha Bonn (Ujerumani), Chuo Kikuu cha Leipzig (pia Ujerumani), n.k.

Pia mchezaji maarufu wa timu za Taifa (Tanzania) za netiboli na Basketball kwa wanawake, na pia timu za jeshi Stars katika michezo hiyo, Bhoke Matambalya ni mjukuu wa "Chifu/Mwanangwa" Matambalya wa Wandibha.

Kadhalika, babu wa Prof. Sarungi, msomi na daktari maarufu wa mifupa ni Mkabwa, aliyehamia Wilaya ya Rorya, Mara Kaskazini.

  Makala hii kuhusu utamaduni wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Wakabwa kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.