Wapangwa ni kabila la watu kutoka Milima Livingstone karibu na pwani ya mashariki ya Ziwa Nyasa, wilaya ya Ludewa, Mkoa wa Njombe, kusini mwa nchi ya Tanzania.

Mwaka 2002 idadi ya Wapangwa ilikadiriwa kuwa 150,000.

Lugha yao ni Kipangwa.

Historia hariri

Wapangwa wamekusanyika pamoja hasa katika maeneo ya Ludewa (Madunda, Mawengi, Mahorong'wa, Mlangali, Masimbwe, Mkiu, Ulayasi, Lupanga, Madilu, n.k.) kuelekea Njombe. Chanzo cha wao kuwa karibukaribu kiukoo, ni vita, maana wao walitokea katika maeneo mbalimbali, kama vile Malawi na Msumbiji, kwa ajili ya vita.

Uchumi hariri

Wapangwa hulima mazao mbalimbali ya chakula katika maeneo ya miinuko na mabondeni kandokando ya mito. Hulima kwa ushirika unaoitwa njhiika au mkove. Pia hulima mazao ya biashara kama kahawa, chai, pareto, mahindi. Kabila hili pia hupata matunda ya asili kama vile: masada, savula, makuhu, mahofita, mafudo, minhingi, madongadonga, vudong'o na nisongwa.

Pia ni wafugaji wa makundi madogomadogo ya ng'ombe, mbuzi, kondoo na nguruwe (kitimoto). Tena Wapangwa ni hodari sana kwa utegaji na uwindaji wa wanyamapori kama vile (kwa lugha yao) nyhaluchi, mahtu ngwehe, sudi, ng'ese, ng'wali ni videke.

Utamaduni hariri

Chakula chao ni ugali wa mahindi, ulezi na mtama kidogo. Kitoweo cha vyakula hivyo ni maharage, samaki, nyama na jamii ya mbogamboga.

Kinywaji chao ni pombe (ukhimbi) yaani kangala, komoni, ulanzi ambao hugemwa kutoka katika mmea uitwao mlanzi. Ulanzi ni pombe ya asili sana kwa Wapangwa, maana ni jadi kwao kunywa ulanzi, na hata watoto wadogo hupewa ulanzi kama juisi. Ulanzi, kwa Wapangwa ni pombe ambayo inaheshimika sana, maana hata wanapokwenda shambani, huenda na ulanzi, na kama ukimpeleka mfanyakazi shambani bila ulanzi, huwa anakaidi kufanya kazi, mpaka apewe ulanzi.

Hata katika harusi na sherehe nyingine za kimila kama vile kujengea makaburi (Mahoka), mila za kumrudisha mjane nyumbani (Ngotora), mila za kuabudu miungu, n.k., ulanzi ndio huwa unatumika zaidi ya pombe nyingine.

Kwa hiyo, Wapangwa wote (kama vile kina Willah, Haule, Muligo, Mtweve, Ngairo, Mwinuka n.k.), ambao bado wanatii mila na desturi zao, ulanzi kwao ni jadi.

Mavazi yao ya asili ni nguo zilizotengenezwa kwa ngozi za wanyama pamoja na magome ya miti ya misambi ambayo hupondwapondwa, hufumwa na kupakwa mono.

Nyumba zao kwa sasa ni za matofali ya udongo ya kuchoma na kuezekwa kwa bati, hata hivyo nyumba zao za asili zinajengwa kwa kutumia miti kugandikwa kwa udongo wa mfinyanzi na kuezekwa kwa nyasi aina ya hunji na lihanu.

Usafiri wao wa asili ni kwa chombo kiitwacho ngwichili ambacho kinatengenezwa kwa kutumia miti asilia.

Viungo vya nje hariri

  Makala hii kuhusu utamaduni wa Tanzania bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Wapangwa kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.