Mchoraji (kwa Kilatini na Kiingereza Pictor[1]) ni jina la kundinyota ndogo kwenye angakusi ya Dunia.

Nyota za kundinyota Mchoraji (Pictor) katika sehemu yao ya angani
Ramani ya Mchoraji

Mahali pake

Mchoraji lipo jirani na makundinyota saba za Njiwa (Columba) upande wa kaskazini, Shetri (Puppis) na Mkuku (Carina) upande wa mashariki, Patasi (Caelum) kwenye kaskazini-magharibi, Panji (Dorado) na Panzimaji (Volans) upande wa kusini.

Nyota angavu ya Suheli (Canopus, Alfa Carinae) iko karibu inasaidia kukuta Mchoraji angani.

Jina

Mchoraji ni kati ya makundinyota yaliyoobuniwa katika enzi ya kisasa. Kama ilivyo kwa nyota nyingine zinazoonekana kwenye angakusi pekee haikujulikana kwa Wagiriki wa Kale wala kwa Waarabu kwa hiyo wataalamu wa Ulaya hawakuwa na habari nazo. Kundinyota hili lilielezwa mara ya kwanza na Mfaransa Nicolas-Louis de Lacaille wakati wa karne ya 18 kwa jina la Equuleus Pictorius yaani “kifarasi/punda wa mchoraji” kwa maana ya "Kiegemeza cha kushikilia picha cha Mchoraji" iliyofupishwa baadaye kuwa "Pictor" yaani "Mchoraji".

Lacaille alikaa miaka miwili kwenye Rasi ya Tumaini Jema (Afrika Kusini) akitazama nyota za angakusi ambazo wakati ule zilianza tu kujulikana kati ya wanaastronomia wa Ulaya. Alipima nyota 10,000 akazipanga katika makundinyota na kutunga majina kwa kundinyota mpya 14[2]. Jina la Kifaransa lilitafsiriwa kwa Kilatini na kufupishwa kama "Pictor“(Mchoraji).

Chaguo la jina lilikuwa dalili ya kipindi cha Zama za Mwangaza ambako Lacaille alitumia majina ya zana za siku zake kwa kutaja nyota, si tena majina ya mitholojia ya kale.

Mchoraji (Pictor) iko kati ya makundinyota 88 yaliyoorodheshwa na Umoja wa Kimataifa wa Astronomia [3] kwa jina la Pictor. Kifupi chake rasmi kufuatana na Ukia ni 'Pic'.[4]

Nyota

Nyota za Mchoraji ni chache na dhaifu; kwa jumla kuna nyota 49 zenye mwangaza wa mag 6.5 yaani zinaonekana kwa macho matupu mahali penye giza kabisa. Nyota angavu zaidi ni α Alfa Pictoris yenye mwangaza unaoonekana wa mag 3.3 ikiwa umbali wa miakanuru 97 kutoka Dunia[5].

Beta Pictoris ilitambuliwa kuwa nyota yenye sayari kubwa iliyo na masi mara nane kuliko Mshtarii katika mfumo wetu inayozunguka nyota kwa umbali wa vizio astronomia 8. [6]

Tanbihi

  1. Uhusika milikishi (en:genitive) ya neno "Pictor " katika lugha ya Kilatini ni "Pictoris” na hili ni umbo la jina linaloonekana katika majina ya nyota za kundi hili kama vile Alfa Pictoris, nk.
  2. Histoire de l'Académie royale des sciences ; taarifa ya Lacaille katika "Historia ya Akademia ya Kifalme ya sayansi", uk. 588, Tovuti ya Bibliothèque nationale de France (BnF), iliangaliwa Julai 2017
  3. The Constellations, tovuti ya International Astronomical Union , iliangaliwa Julai 2017
  4. Russell, Henry Norris (1922). "The New International Symbols for the Constellations". Popular Astronomy 30: 469–71. Bibcode:1922PA.....30..469R. 
  5. [ http://simbad.u-strasbg.fr/simbad/sim-id?Ident=Alpha+Pictoris&NbIdent=1&Radius=2&Radius.unit=arcmin&submit=submit+id Alpha Pictoris] kwenye tovuti ya Simbad, iliangaliwa Oktoba 2017
  6. Exoplanet Caught on the Move, tovuti ya ESA ya 10 June 2010, iliangaliwa Oktoba 2017

Viungo vya Nje

  Makala hii kuhusu mambo ya sayansi bado ni mbegu.
Je, unajua kitu kuhusu Mchoraji (kundinyota) kama historia yake au mahusiano yake na mada nyingine?
Labda unaona habari katika Wikipedia ya Kiingereza au lugha nyingine zinazofaa kutafsiriwa?
Basi unaweza kuisaidia Wikipedia kwa kuihariri na kuongeza habari.