Mkataba wa Versailles
Mkataba wa Versailles ulikuwa mapatano ya kimataifa ya kumaliza Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia (1914 - 1918) upande wa Ujerumani. Mapatano yote yalifikiwa kati ya mataifa washindi pekee na serikali ya Ujerumani ilipaswa kuikubali mwishowe. Ujerumani ikatia sahihi kwa malalamiko lakini ilitishiwa ya kwamba wanajeshi wa washindi wangeingia Ujerumani.
Washiriki wa Mkataba
haririNchi shiriki za mkataba zilikuwa pamoja na Ujerumani hasa Uingereza, Ufaransa na Marekani zilizoitwa "Watatu wakubwa" pamoja na Italia na Japani.
Nchi nyengine upande wa washindi waliotia sahihi lakini hazikuwa na athira katika mapatano yalikuwa Ubelgiji, Bolivia, Brazil, China, Kuba, Ekuador, Ugiriki, Guatemala, Haiti, Ufalme wa Hijaz (Uarabuni), Honduras, Liberia, Nikaragua, Panama, Peru, Poland, Ureno, Romania, Ufalme wa Yugoslavia, Uthai, Chekoslovakia na Uruguay.
Masharti
haririMashariti ya mkataba yalikuwa makali. Ujerumani ilipaswa kukubali ya kwamba ilikuwa na kosa lote kwa vita na kuwa inadaiwa kulipa fidia kwa washindi.
Masharti mengi yalihusu maeneo yaliyotengwa na Ujerumani na kuhamishwa kwa nchi jirani, viwango vya juu kwa jeshi la Ujerumani na madai ya malipo kwa nchi washindi.
Kwa jumla Ufaransa ililenga kuwapa Wajerumani masharti makali sana; Waingereza walitaka kuwa na Ujerumani yenye nguvu ya kiuchumi lakini bila uwezo wa kijeshi; Marekani ilitaka amani ya kudumu.
Maeneo yaliyotengwa na Ujerumani
hariri- Koloni zote zikigawiwa kwa Uingereza, Ufaransa, Marekani na Japani kama maeneo ya kudhaminiwa chini ya mamlaka ya Shirikisho la Mataifa
- Majimbo ya Alsasi na Lorrain yakapelekwa Ufaransa
- Jimbo la Prussia ya Magharibi yakapelekwa Poland
- Maeneo mbalimbali madogo yalitengwa na kupelekwa chini ya Denmark, Poland na Chekoslovakia
- Maeneo yaliyotengwa na kuwekwa chini ya ulezi wa Shirikisho la Mataifa: Danzig kama dola-mji wa pekee, Saarland iliyounganishwa kiuchumi na Ufaransa, Eneo la Memel lililokabidhiwa kwa Ufaransa na kutekwa na Lithuania mwaka 1923
- Eneo la Eupen-Malmedy likapelekwa Ubelgiji
Masharti ya kijeshi
haririUjerumani ilipaswa kupunguza jeshi lake hadi idadi ya wanajeshi 100,000, kubomoa manowari kubwa na kufuta nyambizi zake zote. Eropleni za kijeshi zilikuwa marufuku kwa Ujerumani.
Masharti ya kiuchumi
haririUjerumani ilipaswa kukubali kulipa fidia kubwa kwa hasara zilizotokea kwa nchi washindi kutokana na vita. Kiwango cha fidia hii kilipangwa kuwa Mark bilioni 132 zilizotakiwa kulipwa hadi 1984.
Matatizo ya baadaye
haririWataalamu wengi huona ya kwamba masharti haya makali yalikuwa sababu kuu ya matatizo ya kiuchumi ya Ujerumani yaliyosababisha hali ya kisiasa na kijamii iliyoleta ushindi wa chama cha NSDAP cha Adolf Hitler baada ya 1930.
Sehemu ya mkataba iliunda Shirikisho la Mataifa lililotakiwa kuzia vita zijazo.